Thursday, March 12, 2015

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe

Chadema yambwaga Zitto mahakamani

SAFARI ya mapambano kati ya Zitto Kabwe-Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Chama chake cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imefika ukiongoni baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali kesi yake namba 1 ya mwaka 2014, ya kuzuia asijadiliwe. Wanaandika Deusdedit Kahangwa na Sarafina Lidwino(endelea).
Uamuzi huo wa mahakama, unamweka Zitto njia panda ndani ya Chadema kutokana na Katiba yao kuzuia wanachama wake kuchukua hatua aliyopitia  badala ya kutumia ngazi za chama; Sasa chama kiko huru kuchukua uamuzi wowote dhidhi yake kuanzia leo.
Kanuni za kusimamia shughuli, mwenendo na maadili ya wabunge wa Chadema (2006), kifungu cha 8.0 (a) (x); zinasomeka ifuatavyo; “Chadema itashughulikia matatizo ya viongozi na wanachama kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa katiba ya chama, wala hata siku moja haitashughulikia mambo kama hayo mahakamani. Mwanachama atakayeshindwa kufuata taratibu na ngazi za chama hatavumiliwa na atafukuzwa uanachama”.
Katika hukumu yake leo asubuhi, Jaji Richard Mziray amekubaliana na hoja za Chadema zilizowasilishwa na mawakili wake, wakiomba kesi hiyo ifutwe kwa madai inakiuka katiba ya chama.
Kwa mujibu wa wakili wa Chadema, Peter Kibatala, katika hukumu yake Jaji Mziray amekubaliana na hoja hizo mbili na kumtaka Zitto kukilipa chama chake gharama zote za kuendesha kesi hiyo.
“Kadiri madai haya mawili yanavyohusika, Jaji Mziray amekubaliana na mawakili wa Chadema kuhusu madai kwamba kesi iliyofunguliwa na Zitto Kabwe ilikuwa imefunguliwa kinyume cha utaratibu wa kisheria,” amesema Kibatala.
Wakili Kibatala hakusema lolote kuhusu msimamo wa Jaji Mziray dhidi ya hoja nyingine tatu walizowasilisha Mahakama Kuu. Nakala ya hukumu ya leo haikuweza kupatikana mara moja ili kutoa picha kamili ya maamuzi husika.
Katika kesi hiyo, Zitto kupitia kwa mwanasheria wake, Arbert Msendo alifungua malalamiko dhidi ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa pamoja na Bodi ya Wadhamini.
Mapema mwaka jana, Zitto Kabwe aliitwa na Kamati Kuuya Chadema akitakiwa kujibu tuhuma za usaliti dhidi ya chama lakini hakuitikia wito huo.
Badala yake, alifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, akiiomba itoe amri ya kuzuia vikao vya Kamati Kuu ya Chadema kutojadili uanachama wake mpaka hapo kikao cha Baraza Kuu la Chadema kuitishwa, kupokea na kujadili na kuamua rufaa yake.
Katika rufaa yake, Zitto alikuwa anapinga uamuzi wa Chadema kumvua cheo chake cha Unaibu Katibu Mkuu.
Mnamo 21 Februari 2014, Mahakama Kuu kupitia hukumu ya Jaji John Utamwa, ilitoa zuio kwa Kamati Kuu ya Chadema kujadili na kuamua suala lolote linalomhusu Zitto.
Katika hukumu yake, Jaji Utamwa alidai kwamba, “itakuwa ni haramu kumtia hatiani mlalamikaji kwanza na kisha kumsikiliza baadaye.
Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili wa Chadema waliomba mapitio ya hukumu na leo maombi yao yamezaa matunda.
Awali, Wakili wa Zitto, alijibu kupinga uhalali wa maombi haya. Na baadaye, mawakili wa Chadema, Tundu Lissu na Peter Kibatala, waliwasilisha majibu yao.
Katika majibu yao ya 08 Agosti 2014 na 09 Oktoba 2014, mawakili Lissu na Kibatala, waliibua hoja tano kupinga mashitaka yaliyofunguliwa na Zitto dhidi ya uongozi wa Chadema.
Katika hoja ya kwanza, Lissu na Kibatala walidai kwamba, mashitaka ya Zitto dhidi ya uongozi wa Chadema yalikuwa ni batili kisheria kwa kuwa, yamekiuka kifungu cha 13 cha Sheria ya Kanuni ya Mwenendo wa Kesi za Madai, Sura ya 33, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
Kwa maoni yao, Zitto alipaswa kusajili kesi yake katika Mahakama ya Wilaya na sio Mahakama Kuu, kama alivyofanya.  
Na katika hoja ya pili, walidai kwamba, mashitaka ya Zitto dhidi ya uongozi wa Chadema yalikuwa ni batili kisheria kwa kuwa, yamekiuka kifungu cha 7(1) cha Kanuni za Masjala ya Mahakama Kuu za mwaka 2009.
Kwa maoni yao, Zitto alipaswa kusajili kesi yake katika Masjala ya Mahakama ya Wilaya na sio Masjala ya Mahakama Kuu, kama alivyofanya.
Kwa mujibu wa Kibatala, katika hukumu iliyotolewa leo na Mahakama Kuu, Jaji Mziray amekubaliana na hoja hizo mbili.
Uanachama wake
Katika mkutano wake na waandishi, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, amesema kwa sasa Chadema haina mahusiano yoyote ya kisiasa na Zitto.
“Kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chadema zilizopo sasa hivi, mwanachama anayewashitaki viongozi wa chama mahakamani badala ya kufuata ngazi za kimadaraka ndani ya chama anakuwa amefanya usaliti na hivyo kupoteza sifa ya kuendelea kuwa mwanachama. Kwa hiyo, Chadema ilishamwondolea udhamini Zitto,”amesema Lissu.
Hata hivyo, mwanasheria wa Zitto, ameandika kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram kuwa taarifa kuhusu maamuzi ya Mahakama Kuu leo wamezipata kupitia mitandao ya kijamii.
“Taarifa kuhusu maamuzi ya Mahakama Kuu leo tumezipata kupitia mitandao ya kijamii kwa sababu kesi awali ilikuwa imepangwa tarehe 12.03.2015 lakini inaonekana kwenye rekodi imerudishwa nyuma na maamuzi hayo kusomwa leo bila sisi kuwa na taarifa.
“Tunafanya utaratibu tupate nakala ya maamuzi hayo ili kujua nini cha kufanya. Hatuna taarifa rasmi ya kufukuzwa Mh. Zitto Kabwe uanachama. Taratibu zote zitafuatwa pindi tukipokea taarifa rasmi kutoka mahakamani na kwenye chama. Ni matumaini yetu jambo hili halitaendeleza chuki zisizokuwa na sababu au kujenga kati ya wahusika,” amesema Msando.
Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa

Dk. Slaa afichua mauaji dhidi yake; awataka TISS, Kikwete waachie ngazi

KIONGOZI mkuu wa upinzani nchini, Dk. Willibroad Slaa, amekoleza moto kuhusu madai ya kutokomeza maisha yake. Wanaandika Sarafina Lidwino na Deusdedit Kahangwa … (endelea).
Dk. Slaa amelieleza jeshi la polisi jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi) kuwapo mpango wa kumuua uliokuwa unasukwa na baadhi ya viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).
Katibu mkuu huyo wa Chadema, ameiambia MwanaHALISI Online, muda mfupi baada ya kusajili maelezo yake kituo cha Polisi cha Kati, “Mungu bado ananipenda na anakipenda Chadema.”
Alisema, “Tumepata ushahidi usio na shaka kuhusu mpango wa kutaka kuniua. Kumekuwa na mawasiliano mazito sana kati ya maafisa usalama, viongozi wakuu wa CCM na mlinzi wangu. Mawasiliano haya yalilenga kudhuru maisha yangu.”
Amesema, “Tumebaini kwamba Idara ya Usalama wa Taifa walikuwa wanafanya ujasusi dhidi ya Chadema. Walikuwa wanatoa fedha kwa mlinzi wangu binafsi ili kumshawishi kuvujisha siri za chama. Jambo hili ni kinyume cha sheria ya kuanzishwa idara ya usalama wa taifa.
Amesema, kutaka kufanya au kutishia kuua, ni kosa la jinai, hivyo analitaka jeshi la polisi kuhakikisha mhalifu huyo, anakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Taarifa zinasema, aliyekuwa anashirikiana na TISS na viongozi wa CCM kutokomeza maisha ya Dk. Slaa, ametajwa kuwa ni Khalid Kagenzi.
Kwa mujibu wa mawasiliano katika simu ya Kagenzi, aliyekiri kushiriki njama za kumuua Dk. Slaa, waliokuwa wanawasiliana na Kagenzi, ni pamoja na Philiph Mangula, makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara; Gwamaka Mwang’onda na wengine kadhaa, ambao watachapishwa katika mtandao huu katika toleo lake la Jumamosi.
Akizungumza kwa uchungu na mwandishi wa gazeti hili, Dk. Slaa amesema, “Idara ya usalama wa taifa imepoteza heshima katika jamii na kuwataka viongozi wake wajiuzulu.”
Ametoa mfano wa nchini Marekani, kwamba “…ilipothibitika Rais Nixon na chama chake cha Republican walikuwa wamefanya ujasusi dhidi ya chama cha democrats, Rais Nixon alilazimika kujiuzulu. Hata CCM na idara yao ya usalama wa taifa wanafanya kosa kama hilo.”
Mwenyekiti wa CCM na ambaye ni Rais wa Jamhuri, ni Jakaya Kikwete.
Dk. Slaa amesema yeye alifika polisi kama mlalamikaji. Alitoa maelezo yake ili kuwawezesha kufanya kazi yao ya uchunguzi.
Amesema, “Sikuhojiwa kama baadhi ya watu wanavyofikiri. Mimi sio mtuhumiwa. Mimi ni mlalamikaji.”
Amesema haki zake zote zimezingatiwa alipokuwa polisi. Aliongozana na wanasheria watatu wa Chadema, Prof. Abdallah Safari, Nyaronyo Kicheere na John Mallya.
Prof. Safari, pia ni makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara.
Zoezi la kuandika maelezo yake, lilitanguliwa na majadiliano kati yake na polisi ili kujenga picha ya pamoja kuhusu jambo litakalo andikwa.
Anasema, polisi waliuliza kama nataka waandike maelezo yangu wao au nataka kuyaandika mwenyewe. Nilichagua kuyaandika mwenyewe. Sheria inaruhusu hili pia.
Malalamiko yake yana kurasa tisa.
Akizungumzia wanachama watatu wa Chadema wanaoshikiliwa na polisi, Ahmed Sabula, Benson Mramba na Jacob Boniface (Diwani wa Ubungo), Dk. Slaa amesema, “Ni jambo la kusikitisha, muuaji yuko nje na waliozuia mauaji ndiyo wanaoshikiliwa.”
Habari ambazo zimepatikana baadaye zinasema, jeshi la polisi limeahidi kuwapa dhamana “makachero” hao wa Chadema kesho.

Zitto: Mimi bado mbunge.

12th March 2015
Chapa
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Zitto amesema hajapewa taarifa rasmi, hivyo ataendelea kuwa mbunge.
 
Pamoja na kauli hiyo ya Zitto, viongozi wa Chadema wamesema hawatahangaika kumwandikia barua kumjulisha hatua zilizochukuliwa na chama hicho dhidi yake.
 
Zitto akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, alisema ataendelea na kazi yake ya ubunge kwasababu hajapewa taarifa rasmi na Chadema kuhusu uamuzi uliochukuliwa wa kumvua uanachama.
 
“Sina taarifa rasmi kilichotokea na kama mnavyoona naendelea na vikao vya kamati kama kawaida na leo (jana) nitakuwa na watu wa Benki Kuu (BoT), TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na AG  (Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Ijumaa nitakwenda Kigoma jimboni kwangu kwa ajili ya kazi zangu, niliwahidi wananchi wangu nitakwenda kabla ya kwenda bungeni, kimsingi mimi bado ni mbunge,” alisema.
 
Licha ya Chadema kutangaza kumvua uanachama, Zitto jana aliendesha vikao vya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kama kawaida.
 
Zitto alisema hawezi kujibishana na chama chake kwani hajalelewa katika maadili kama hayo na kwamba kitu muhimu kwake ni kazi ya kuwatumikia Watanzania.
 
“Mimi huwezi ukanilinganisha na mbunge yeyote katika kazi ambazo nimekuwa nikizifanya, siasa kwangu ni ‘issues’ tofauti na watu wengine ambao siasa zao ni kugombana na watu, kwangu hizi ni changamoto, nakomazwa,” alisema.
 
Alisema ifahamike kuwa maamuzi yoyote lazima yafanywe kwa kikao na hayawezi yakaamuliwa na mtu mmoja.
 
“Maamuzi yoyote yanayotolewa ni ‘process’ (mchakato) kwa sababu hata kwa maamuzi ya chama kuna suala la kumwandikia barua Spika wa Bunge naye ajiridhishe, kwa hiyo mimi bado ni mbunge ambaye nilichaguliwa kuanzia mwaka 2005 hadi sasa na nitaendelea kuwatumikia Watanzania,” alisema. 
 
LISSU; HATUTAMWANDIKIA BARUA ZITTO 
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema chama hicho hakitahangaika kumwandikia barua Zitto kumjulisha uamuzi wake kwa kuwa anajua alishakiuka Katiba ya chama kwa kushtaki hivyo uanachama wake unakoma mara moja.
 
Lissu alisema jana kuwa: “Sisi hatuhitaji kumfahamisha kwa sababu anajua adhabu ya kukiuka Katiba, tutaandika barua kwenye mamlaka husika siyo kwake.”
 
Alisema Chadema kitamwandikia barua Katibu wa Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuwafahamisha uamuzi huo.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alipoulizwa na NIPASHE jana alisema, hadi jana jioni alikuwa hajapokea barua ya Chadema juu ya kumtimua uanachama Zitto.
 
 WABUNGE WAMLILIA
Baadhi ya wabunge wamezungumzia kuvuliwa uanachama kwa Zitto, wengine wakimshauri kuwa kama hajaridhika anaweza kukata rufaa zaidi mahakamani.
 
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema hawezi kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kuwa ndiyo mhimili wa kutoa haki.
 
Hata hivyo, alisema Zitto ana nafasi ya kukata rufaa ngazi ya juu ya Mahakama kama hajaridhika na uamuzi huo. 
 
LUGOLA: CHADEMA WAMEKOSEA  
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema amepokea kwa mshtuko taarifa za Mahakama kutupa shauri la Zitto, akieleza kuwa Chadema nayo haijatumia busara kumfukuza. 
 
“Nimeshtushwa na kusikitishwa zaidi kwa kitendo cha Chadema kumvua uanachama kwa sababu mahali ambapo sisi CCM tumefika tulikuwa tunahitaji upinzani imara ambao unatunyima usingizi ili  tuisimamie vyema serikali, katika mazingira ambayo tunahitaji upinzani imara kama Chedema sidhani kama wamechukua uamuzi wa busara,” alisema. 
 
Lugola alisema uimara wa Chadema hautapatikana kwa kumfukuza Zitto, bali kwa kuvumiliana na kutafuta muafaka ndani ya chama hicho pale zinapotokea. 
 
Alisema CCM inahitaji Chadema imara ili iwe makini katika kuwatumikia wananchi na kwamba kwa kumfukuza Zitto, Chadema na CCM vitadhohofika kwa kuwa vitakosa mtu makini wa kuikosoa.
 
“Mchango wake ulikuwa ni mkubwa na wangeweza kuiga CCM ambayo ina watu ambao walianza kampeni za urais mapema, lakini hatujawafukuza, tumewaonya. Chadema isiangalie mabaya ya CCM iyachukue mazuri tuliyonayo,” alisema. 
 
SERUKAMBA: INADIDIMIZA DEMOKRASIA 
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba, alisema uamuzi wa Chadema unadhohofisha demokrasia nchini.  
 
Alisema Katiba ya nchi ilipaswa kuyatazama ili kukomesha udikteta wa demokrasia nchini, akisema kwa Zitto ni miongoni mwa wabunge wenye ushawishi mkubwa, hivyo Chadema walipaswa kutomtimua. 
 
MWIGULU: NIMESIKITISHWA
 Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema amesikitishwa na taarifa za kuenguliwa uanachama Zitto ndani ya chama alichoanzia siasa, alichokitumikia kwa jasho na mali, alichowekeza muda na akili yake kwa zaidi ya miaka 19.
 
Mwingulu ambaye aliandika taarifa hiyo katika mtandao wake wa Facebook, alisema Zitto amekuwa chachu ya mabadiliko kwa vitendo kwa Taifa.
 
“Uwezo wa kisiasa wa Zitto adhabu yake siyo kumfukuza, demokrasia ni lazima itumike, nakusihi kijana mwenzangu, mwanasiasa mwenzangu na mchumi mwenzangu kuwa, Taifa linakuhitaji sana wakati huu tunapopambana na ufanyaji kazi kwa mazoea na kuleta mabadiliko kwa vitendo, usikate tamaa Watanzania watakuhesabia mema kwa yote unayoyafanya kwa ajili ya Taifa letu,” alisema Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi.
 
MZIRAY: CHADEMA WAMEFANYA MAAMUZI YA JAZBA
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray, alisema Chadema imefanya maamuzi ya kumvua uanachama Zitto kwa jazba kwa sababu hali hiyo haiwezi kusaidia kuviimarisha vyama vya upinzani kupambana na chama tawala.
 
“Inaonekana kumekuwa na jazba na kutafutana katika maamuzi haya, siasa za kuviziana na kukomoana siyo nzuri, Zitto amefanya kazi nzuri sana ndani ya Chadema kulikuwa na sababu gani kufanya maamuzi haraka ya kumvua uanachama,” alisema
Mziray  pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha APPT Maendeleo.
 
 ADC : CHADEMA WANGEMSAMEHE ZITTO
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Change (ADC), Doyo Hassan Doo, alisema uamuzi uliochukuliwa na Chadema ni wa haraka kwani wangeweza kulitazama suala hilo kibinadamu na kumsamehe.
 
“Hatukatai  Chadema wamefuata katiba yao kumfukuza Zitto, lakini si vibaya kama wangemsamehe, sisi hatuungi mkono hii tabia mbaya iliyoanza kujengwa na baadhi ya vyama vya siasa kufukuzana fukuzana,” alisema.
 
ACT: TUNAMKARIBISHA ZITTO 
Katibu Mkuu wa Chama cha  Alliance for Change and Transparency (ACT- Tanzania), Samson Mwigamba, alimshauri Zitto asikate rufaa kwa kuwa atapoteza muda, badala yake achukue uamuzi wa kujiunga na ACT.
 
 “Tunatambua mchango wa Zitto katika Taifa hili, siasa zake ni tofauti na siasa za watu wengine, ni za kistaarabu, uzalendo na anapenda maelewano na watu wote, hivi sasa kila chama kitapenda kumkimbilia ila atambue kwamba ACT pekee ndiyo chama kinachoweza kumfanya atimize ndoto zake za kisiasa,” alisema Mwigamba.
 
Juzi Lissu, alitangaza Zitto kuvuliwa uanachama kwa madai ya kukiuka katiba ya chama kifungu cha 8(a) (x) ambacho kinaeleza kuwa, mwanachama yeyote akifungua kesi mahakamani dhidi ya chama akishindwa katika kesi hiyo anakuwa amejifukuzisha uanachama.
 
CHANZO: NIPASHE

PAC yaagiza CAG uchunguzi wa milioni 699/- za Tanesco.

12th March 2015
Chapa
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemwagiza Mdhibti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi kubaini zilikopotelea Sh. milioni 699 zilizotolewa na Wizara ya Fedha kwenda Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambazo hazijulikani ziliko sasa.
 
Aidha, PAC imeagiza Tanesco kuwasilisha katika ofisi ya Bunge mikataba yote ya kampuni zinazozalisha umeme nchini ambazo zimeingia nayo mikataba ili kupitiwa upya na kuwa kumbukumbu kwa Bunge.
 
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alitoa maelekezo hayo jana katika kikao baina ya kamati hiyo na menejimenti ya Tanesco na kusema kumekuwa na mvutano kuhusu Sh. milioni 699 zilizotolewa na Hazina kwenda Tanesco.
 
Zitto alisema inawezekana fedha hizo zimetolewa kwa Tanesco, lakini zimetumika vibaya au Hazina wamezitoa kwa mtu tofauti, hali ambayo imekuwa ikileta mkanganyiko ambao unahitaji kufanyiwa uchunguzi.
 
Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha Tanesco, Anetha Chegula, alisema fedha hizo zinadaiwa kutolewa na Hazina tangu mwaka 2012 kwenda Tanesco kwa ajili ya kusaidia miradi ya umeme, lakini hazijafika katika shirika hilo licha ya Hazina kuonyesha kuwa zilishatolewa.
 
Chengula alisema wamekuwa wakiitaka Hazina kuonyesha vielelezo vinavyoonyesha kuwa fedha hizo zimepelekwa Tanesco, lakini hadi mwaka jana Hazina haikufanya hivyo huku Tanesco ikifanya uchunguzi katika akaunti zake bila kuziona fedha hizo.
 
Akizungumzia mikataba ya makampuni ya Agrecco, Symbion, Songas na IPTL , alisema ipelekwe haraka ofisi za Katibu wa Bunge ili iwe kumbukumbu kwa Bunge.
 
Wabunge walisema tozo ya uendeshaji wa mitambo (capacity charge) iangaliwe upya kwa sababu inaingiza gharama kubwa kwa Tanesco, hivyo kushindwa kufikia malengo ya kujiendesha badala yake kuendelea kutegemea serikali kulisaidia.
 
Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy, alisema ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini ni kwa Tanesco kuchukua hatua ya kuinunua mitambo ya umeme inayomilikiwa na kampuni zinazozalisha umeme na kuiuzia Tanesco kwa bei ya juu.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba (pichani), alisema Songas inalipwa Sh. bilioni 8.562 za tozo ya uendeshaji, IPTL Sh. bilioni 4.302 na Aggrecco Sh. bilioni 1.600 kwa mwezi. Mramba alisema Aggreco imekuwa ikiiuzia Tanesco umeme kwa Dola za Marekani senti 40 na IPTL senti 23 huku Tanesco ikiuza umeme huo kwa senti Dola za Marekani 26.
 
CHANZO: NIPASHE

Vilio, vilio, vilio.

12th March 2015
Basi la abiria la Majinje Express lenye namba za usajili T438 CDE likiwa limegongana na lori la mizigo lililokuwa limebeba kontena ambalo liliangukia basi hilo na kuua watu 42, eneo la Changarawe, barabara kuu ya Iringa Mbeya jana. Picha: George Tarimo
Vilio na simanzi jana vilitawala kwenye mji wa Mafinga, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, kufuatia watu 42 kufariki dunia na wengine 23 kujeruhiwa, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupata ajali.
 
Ajali hiyo ilitokana na basi hilo la kampuni ya Majinje Express lenye namba za usajili T.438 CDE kugongana uso kwa uso na lori la mizigo ‘semitrela’ namba T698 APJ na kisha kontena lililokuwa kwenye lori hilo kulifunika basi lilokuwa na abiria.
 
Miongoni mwa waliofariki ni pamoja na dereva wa basi hilo, huku dereva wa lori akielezwa kuwa mahututi katika Hospitali ya Wilaya ya Mafinga.
 
Waliofariki wametajwa kuwa ni Ester Emmanuel, Lusekelo Enock, Jeremia Watson, Digna Solomon, Frank Chiwango, Luten Sanga, Teresia Kamiyage na Dotto Katuga.
 
Wengine ni Esta Fide, Pauline Justine, Mbamba Ipyana, Catherine Mwajengo, Zera Kasambala, Rebeka Kasambala Mr. Musa, Shadrack Msigwa, Mathias Justine, Mr. Elias na Juliana Bukuku.
 
Wamo pia Christina Lyimo, Martin Haulo, Dominick Mashauri, Esta Willy, Lucy Mtega, Erick Shitind, Edwaga Kamiyage, Frank Mbale, Mustafa Ramadhani, Kelvin Odubi, Mr. Osward, Omega Mwakasege, Upendo William, Iman Mchange, Charles Lesenga, Mr. Neto Sanga, Pili Vincent, Mr. Hamad, Ed Erick, Daud so Stones na Jacob Doketa.
 
Lori hilo linalomilikiwa na kampuni ya Cipex, lilikuwa kiliendeshwa na Baracka Gabriel, kutoka Iringa kwenda Mbeya.
 
Ajali ilitokea majira ya 3:30 asubuhi, eneo la Changarawe katika barabara kuu ya Iringa-Mbeya.
 
Basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam na lori hilo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda nchi jirani ya Zambia.
 
Habari kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa ajali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ubovu wa barabara na mwendo kasi wa basi hilo.
 
Kwa mujibu wa habari hizo, eneo ambako ajali hiyo imetokea kuna shimo kubwa.
 
Habari hizo zinaeleza kuwa, dereva wa lori alifanikiwa kulikwepa shimo hilo, lakini dereva wa basi alipojaribu, alishindwa kulimudu basi hilo na hivyo kutumbukia. 
 
Baada ya kutumbukia kwenye shimo hilo, magari hayo yalijaribu kupishana na wakati yakipishana, kontena lililokuwa kwenye lori hilo lililiangukia basi na kusababisha vifo hivyo.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alithibitisha kutokea ajali hiyo mbaya.
 
Alisema ajali hiyo kama zilivyo nyingine, zimechangiwa na uchakavu wa miundombinu ya barabara.
 
“Ndugu zangu wanahabari, hii ni ajali kama ilivyo ajali nyingine. Kwa sababu, imetokea sehemu mbaya. Na pia uchakavu wa barabara unachangia na siyo ajali ya kujitakia,” alisema Kamanda Mungi.
 
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo, waliliambia NIPASHE kwamba, awali basi hilo lilikuwa katika mwendo kasi.
 
Kutokana na hali hiyo, walimuita kondakta wa basi hilo na kumtaka amwambie dereva apunguze mwendo, lakini hakufanya hivyo.
 
Kevin Hamfrey, ambaye alikuwa akitokea Mbeya kwenda jijini Dar es Saalam aliitaka serikali kuangalia upya suala la miundombinu kwani imekuwa chakavu na ndiyo iliyochangia ajali hiyo.
 
Musa Mwasega alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, ambao ulisababisha dereva kushindwa kulimudu gari na hivyo kusababisha kugongana uso kwa uso na lori hilo.
 
“Kiukweli ajali hii ni mbaya sana. Na sisi wenyewe baada ya kuona dereva anajaribu kulimudu, tulijua lazima kuna kitu kitatokea kwa sababu awali mwendo kasi ulikuwa siyo wa kawaida,” alisema Mwasega.
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, Boaz Peter, alithibitisha kupokea miili ya watu 42 na majeruhi 23.
 
Alisema hadi sasa wanafanya jitihada ili ndugu watambue miili ya marehemu na kwenda kuichukua.
 
Peter alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Mufindi, wakati majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.
 
Alisema kati ya miili 42,  32 ilipelekwa Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuhifadhiwa kutokana na chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Mufindi kuwa finyu.
 
Kutokana na hali ya majeruhi wengine kuwa mbaya, wawili walichukuliwa na gari la wagonjwa ya wilaya hiyo na kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
 
 Kati ya waliofariki dunia, wanaume ni 37, wakati wanawake ni watano.
 
Baadhi ya wananchi wa mji mdogo wa Mafinga, ambao hawakupenda majina yao kuandikwa gazetini, walisema mara kwa mara wamekuwa wakitoa kilio chao kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na baadhi ya viongozi wa ujenzi wa barabara wilaya ya Mufindi, lakini kimekuwa hakisikilizwi.
 
Badala yake, wamekuwa wakijibiwa kuwa suala hilo litapelekwa kwa viongozi husika.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, aliiagiza Tanroads kuanza kushughulikia uchakavu wa barabara hiyo mara moja.
 
“Msiba huu ni wa watu wote, siyo wa mtu mmoja, nimesikitika sana kusikia kuwa asubuhi kuna ajali ilitokea  eneo la Changarawe nje kidogo ya mji wa Mafinga na nilivyosikia nimekuja mara moja kuangalia ni jinsi gani tutafanya ili kuwasaidia ndugu hawa, ”alisema Masenza.
 
Rais Jakaya Kikwete amemtuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Masenza, na kuwahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao na kuwaombea majeruhi wote wapone haraka ili waendelee katika shughuli zao za ujenzi wa taifa. 
CHANZO: NIPASHE

Mbio za uchaguzi mkuu wagombea watizamwe hivi!


Watu wakilinda masanduku ya kura,
Wakati Uchaguzi mkuu unakaribia, porojo zilizozagaa mitaani na taarifa za vyombo vya mawasiliano na mitandaoni ni majina ya  wagombea wakijadiliwa na kusifiwa kuwa wana kila sifa ya kuongoza taifa na jimbo hivyo ndiyo wanaohitajika kuipokea kura ya ndiyo.
 
Si mbaya kuwafahamu watakaowaongoza lakini ni vyema kujua zaidi uwezo wa marais, madiwani  na wabunge wajao, je historia zao zinasemaje, wana haiba gani (personality/ character) pia  uadilifu wao ukoje?
 
Katika kuwachunguza viongozi watarajiwa kuna baadhi ya vidokezo vinavyowazungumzia viongozi na sifa zao kama vinavyonukuliwa kutoka kwenye machapisho na mihadhara ya Mhubiri wa Kimataifa hayati Dk. Myles Munroe, wa Huduma ya Bahamas Faith Ministry, ambavyo kiongozi kwa mtizamo wake anahisi analazimika kuwa navyo.
 
Akizungumza katika moja ya mihadhara wakati wa uhai wake  (alifariki mwishoni mwa mwaka jana  katika ajali ya ndege) aliainisha kuwa kiongozi haimaaniisha kuwa mtu aliyefanya mambo makubwa ya kutisha tena mwenye mafanikio makubwa, kwa mfano pengine tajiri wa kwanza duniani Bill Gates wa Marekani ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Computer ya Microsoft.
 
Japo ni bilionea na mashuhuri lakini si kwamba unapozungumzia viongozi wote si lazima wawe na sifa za utajiri, umaarufu au kuwa wakipekee duniani sivyo anasema la muhimu ili uwe kiongozi ni lazima uwe na maono, muadilifu mwenye haiba pamoja na karsima au karama.
 
Akianza na maono anazungumzia suala la kuwa na maono na malengo yanayotekelezeka tena uwezo wa akili za kuyaweka mambo yaende sawa na kuwahamasisha wale anaowaongoza kuleta mafanikio na kutekeleza malengo wanayojiwekea.
 
 Kiongozi awe wa kitaifa, mbunge, diwani, mkuu wa mkoa, wilaya  au mkurugenzi wa shirika la umma ama la binafsi ni lazima aweze kufanikisha malengo na maono aliyoyaweka yawe ya kampuni, kiwanda ama serikali au jimbo ni sharti awe na uwezo wa kuyatimiza kwa ushindi unaoonekana.
 
Unaposema huduma za afya kwa kila Mtanzania, kama ndilo lengo basi watu waone miundombinu, wataalamu, vifaa , dawa na kuhakikisha kuwa wananchi wanapona na kampeni zimefanikiwa kutokomeza maradhi. 
 
Mhubiri huyu wa kimataifa anasema kabla hujajiingiza kwenye kutangaza nia ya kuwa kiongozi chunguza uadilifu wako. 
 
Uadilifu ni ile hali ya ukweli (faithfulness and diligence) kwa nafsi zao, Mungu wao na wale wanaotarajia kuwaongoza. Kadhalika ni kwa kiasi gani wana kasrima.
 
Haya ni mahojiano yako na Mungu wako.Anataka kiongozi ajiulize yukoje kiuaminifu? “Jipime katika maeneo haya- hofu ya Mungu, kutumia na kulinda mali zako na za umma, fedha unazokabidhiwa, utendaji kazi, uhusiano na wenzako, familia yako na ujue kama ni mwaminifu ama vipi. 
 
Huu mtihani wa uadilifu (diligence) baina yako  na Mungu maana unayeyajua majibu ni wewe binafsi.”
 
Haitoshi watu kusema mgombea huyu amefanya mambo makubwa , ana uwezo huu ama ule. Sifa za wapambe hazijengi wala hazikupi uadilifu huo ni uchunguzi  wako binafsi na Mungu unayemwamini. 
 
UONGOZI NI NINI
Dk Myles Munroe anajibu kuwa unajumuisha mambo mengi lakini , ni muhimu katika kuendeleza shughuli na michakato duniani lakini pia  unahitajika ili kuwafunza na kuwaandaa wengine watakaoongoza sekta na mapambano ya kuleta mabadiliko na hali bora za maisha ya watu na kuufanya ulimwengu kuwa mahala pazuri pa kuishi.
 
Anakumbusha kuwa hakuna neno moja linaloweza kutumiwa kumzungumzia anayetakiwa kuwa rais, mbunge, diwani au kiongozi  maana mambo ni mengi na hakuna sifa pekee ya kumweleza kiongozi. 
 
Hata hivyo Munroe anaona kuwa kiongozi ni huyo  ambaye anateuliwa ama kuchaguliwa kuliongoza kundi timu, shirika na taifa.
Anaelezwa kuwa kiongozi anatakiwa kuwa na karisma au  mwenye uwezo wa kufanya maamuzi muhimu, mwenye mvuto na haiba anayeweza kuwashawishi wengine.
 
Kwa kifupi uongozi ni ‘charism’ au karama ambayo inahusisha haiba kubwa na ni kipaji kutoka kwa Mungu.Kadhalika ni uwezo wa kimamlaka unaoweza kuwasiliana na wengine kikamilifu kuhamasisha wengine kufanya yale yaliyokusudiwa na kuona kuwa yanaleta manufaa.Si kuibuka na kueleza kauli mbiu za kufurahisha lakini zisizotekelezeka. Kwa ujumla kiongozi awe na uwezo wa kushawishi wengine na kuwabadilisha kwa namna bora .
 
VIGEZO VYA KIONGOZI
Ili uwe kiongozi ni lazima uwe na kundi unaloshirikiana nalo linalofuata maelekezo au nyayo zako na lenye imani na maono, malengo na maongozi yako.Kama kiongozi una jukumu kwa watu wako wawe wapiga kura, wafanyakazi wataasisi la kuwaongoza kwa weledi na haki, uhuru na kwa maadili na uadilifu pia na kuonyesha karama yako.
 
Vyeo vya kimamlaka vinavyohusisha kutukuzwa kama “mheshimiwa, bosi, chifu,mkurugenzi, baba, mtukufu” hakika havikufanyiwa kuwa kiongozi bora wakati mwingine vyaweza kuwa kejeli.
 
YAKUFANYA
Kuwa kiongozi bora unahitajika kujiweka sawa na viwango vya juu na vya wakati wa sasa vya marais au viongozi wengine wakuu duniani na kikanda, hivyo fuatilia nyendo za viongozi wenzako duniani wanavyopambana na kuondoa matatizo mbalimbali. 
 
Kwa mfano utasikia Baba Mtakatifu Papa Francis anatembelea makundi ya watu maskini, anazungumza na kujichanganya nao mitaani.
 
Anafahamu nini anachotakiwa kufanya kuwagusa wote anaowaongoza na ikibidi kuwafikia kwa kuwa kuongoza ni ‘karama’ kipaji alichopewa na Mungu analazimika kwenda kwa watu duni pengine  wasiofikiwa wala kukumbukwa na viongozi!
 
Kama ni rais angalia jinsi wale wa kalba yako (marais wenzako) wanavyofanya, mikakati na mipango ya maendeleo ya kuyawezesha mataifa yao kung’ara kwenye ramani ya dunia.
 
KUSOMA
Rais, mbunge ama mkurugenzi unalazimika kusoma machapisho ya aina mbalimbali kuanzia ripoti za kimataifa, za kiuchumi za Afrika, Umoja wa Mataifa, habari za mbadiliko ya tabia nchi. Kadhalika jifunze kuwa mkweli siyo kuongea mambo ya kudandia bila kuwa na vyanzo vya uhakika.
 
Soma magazeti ya kimataifa na ya kitaifa, tizama habari na matukio mbalimbali duniani kwenye televisheni, soma machapisho ya mitandao mbalimbali na unapozungumza kuwa na mamlaka yaani uwe unaelewa mambo. Kuwa mtu wa kutumia watalaamu na kufanya tafiti uwe gwiji la uelewa.
 
Lazima ufahamu habari za kibiashara na uchumi duniani kupitia machapisho mbalimbali, angalia viongozi , watizame wenzako katika mashirika mbalimbali duniani na katika tasinia za kimataifa na kikanda ujue wanafanyaje? Jipime wewe uko wapi katika ngazi za viongozi kitaifa na kimataifa? Waheshimiwa fanyeni tafiti  si kukurupuka na kusema chama chetu kitashinda kwa wimbi la tsunami ama wakati wa kukiondoa chama tawala ni huu, umetafiti? Umezungumza na wananchi?
 
Kutafiti, kujisomea na kufahamu mambo mengi kutakupa mwelekeo na jinsi ya kuwa kiongozi bora na mweledi huku ukijijengea uzoefu wa kipekee kukabiliana na changamoto unazozifanyia kazi.
 
Kwa hiyo mnapoelekea kwenye uchaguzi mkuu jaribuni kujichunguza  na kujiweka kwenye viwango na mjiulize ninastahili?  Na nyie wapambe na mashabiki angalie tunayemtaka anatufaa? Ana vigezo? Au mkishahongwa mmeridhika. Mnawajibu wa kumtafakari kwa viwango hivyo.
 
 
CHANZO: NIPASHE

Wanawake wataishi kwa hofu vijijini hadi lini


ChapaDunia inapoadhimisha Siku ya Wanawake duniani mamia ya wanawake vijijini wanaishi kwa hofu kwani ni walengwa wakuu wa kila sababu ya mauaji. Wanasingiziwa kuwa wachawi, wanadaiwa wasababisha mikosi, maadui wa mvua lakini pia wanageuzwa viambato vya kutengeneza dawa kwani miili yao inachanganywa mambo mengine kuleta utajiri na mafanikio.  

Mauji ya wanawake yamekithiri maeneo ya Ukanda wa Ziwa mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Kagera na Simiyu na kila mara imeshuhudiwa wazee, mabinti na hata walemavu wakiuawa kwa visingizio mbalimbali vinavyohusisha uchawi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (HLRC) cha jijini Dar es Salaam, kinasema wanawake zaidi ya 1,000 wameuawa mwaka jana na kwamba kuanzia mwaka 2010 hadi sasa zaidi ya wanawake 3,000 wanaotuhumiwa kuwa ni wachawi wamepoteza maisha wakiwa na umri kati ya miaka 50 hadi 80.

Wauaji huwashambulia kwa mapanga, visu, kuwachoma moto wakiwa hai mabaki ya miili yao huteketezwa pia wala asitokee mtu wa kuwatetea.

Taarifa zinaeleza kuwa mauji hutokea usiku wa manane, milango huvunjwa kwa mawe makubwa ama wauaji huvizia na kuingia vyumbani wanapolala wanawake, ambao bila msaada wanakatwa kwa mapanga, visu, kuchomwa moto na nyumba zao kupigwa kiberiti.

Wanadaiwa ni wauaji wa watoto  Mikoa ya Kanda ya Ziwa ni kitisho mwanamke anaweza kunyanyaswa akatumiwa radi au mvua ikanyesha juu ya paa lake, akang’olewa mazao shambani, mifugo yake ikauliwa na pia anaweza kuchomwa ndani ya nyumba pamoja na wajukuu zake nyakati za usiku.

Yote hufanyika kwa wasio na hatia kwa vile hakuna ukweli kuwa ni wachawi. Mwalimu Mbuke Mayala wa mkoani Tabora, anasema katika mahojiano ya simu kuwa mauji haya yanachochewa na serikali kushindwa kudhibiti wauaji na kukomesha matendo hayo maovu kwa vile haitafuti kiini cha watu kuendelea kuamini uchawi na kuwa watumwa wa imani za kishirikina.

“Muda wote imeendelea kuwatumia polisi, mahakama na sheria lakini bila kukomesha tabia zilizo ndani ya mioyo ya watu kuendekeza uchawi na kuamini kulogwa kwa muda mrefu.”

Mwalimu Mbuke mkazi wa kijiji cha Witangh’olo mkoani Tabora, anaeleza zaidi kuwa ushirikina umejikita zaidi kwenye ukanda huu ambao wengi hawana elimu , wanaamini imani za kimila na matambiko ya kijadi na pia hakuna huduma za afya zinazoweza kutumiwa kupunguza vifo na kukabiliana na maradhi kama Virusi Vya Ukimwi (VVU), vifo vya watoto na wazazi wao, malaria na pia magonjwa yanayoweza kuepukwa.

Anasema waganga ndiyo wanaotegemewa lakini hawafahamu chanzo wala hawana tiba za magonjwa ambayo kama kungekuwa na huduma za afya wananchi wangehudumiwa na kupona.

Mbuke anasema elimu duni inasababisha jamii kuamini mambo kama kuzaa watoto mapacha ni mkosi, mtoto anayezaliwa akitanguliza makalio analeta balaa na wanalazimika kufanyiwa matambiko.

Kadhalika watu wanaendeleza mila za kurithi wajane , kuwatakasa na kuoa wanawake kwa imani mbalimbali wengine wakiamini wana mikono ya pesa au wanazaa watoto wa kiume.

Ushirikina wa kuua albino umewaumiza zaidi wanawake na watoto wadogo. Hivi karibuni Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, ilitoa taarifa ya kuionya Tanzania kuhusu mauaji ya albino na kulaani kitendo cha kuwateka na kuwaua watoto albino.

 Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN Zeid Ra’ad Al Hussein, katika taarifa hiyo alisema mauaji yataongezeka kwa vile kinakaribia kipindi cha uchaguzi Oktoba mwakani. Idadi ya wanawake albino waliouliwa ni wengi ikilinganishwa na wanaume.

Hawa huuliwa kwa vile hawawezi kujitetea na hawana nguvu. Lakini pia ni ukweli kuwa wanaonewa na jamii muda wote.

Kwa mujibu wa Chama cha Albino Tanzania kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita zaidi ya albino 75 wameuliwa licha ya kwamba hazikutolewa takwimu kijinsia lakini idadi kubwa ni wanawake na wanaweza kufikia karibu 40.Hawa wanaozungumziwa ni wale ambao taarifa zao zinafahamika.

Wapo waliochinjwa kwa siri na haikujulikana hadi leo hatima yao.
Lakini cha kushangaza zaidi waliotiwa hatiani ni wafungwa 10 pekee kati yao wapo waliohukumiwa kifungo cha maisha na wenye adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Ili kutokomeza mauaji ya albino, kuua wanawake na kuendeleza imani za kishirikina serikali inawajibika kutoa elimu shuleni na ile ya kuhamasisha jamii kuachana na ushirikina.

Kadhalika kujenga miundo mbinu na kutoa huduma za afya na kushirikiana na wadau wengine kutokomeza mauaji ya Watanzania wasio na hatia kwa kisingizio chochote.

Mauaji ya wanawake na wazee huambatana na watu wanaowalisha watuhumiwa dawa za kubaini ‘wachawi’ waganga wanadai ukitumia dawa hizo lazima utaonyesha dalili zinazohusiana na matendo hayo.

Kupitia elimu serikali na wadau wakomeshe tabia za baadhi ya watu wanaozurura mitaani kujidai wanaumbua wachawi. Pia sheria ziwepo na mienendo hiyo idhibitiwe ili kuwanusuru wanawake wengi wanaouliwa bila hatia.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Mtei na ndoto za Chadema kushika dola 2015

11th March 2015
Chapa
Edwin Mtei.
“Nimeandaa dume la ng’ombe, Oktoba 31, mwaka huu. Ukija hapa siku hiyo nakukaribisha katika sherehe kubwa nitakayoiandaa…nitachinja dume na kuwaaga viongozi wa Chadema watakaokuwa wamechaguliwa kushika dola kusherehekea ushindi.”
 
Hiyo ni kauli ya matumaini. Ni kauli inayotoka mdomoni mwa Muasisi na Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Edwin Mtei, akielezea jinsi anavyoona na matarajio yake kwa Uchaguzi Mkuu ujao.
 
“Nakukaribisha siku hiyo na huu ndio mwaliko wako, uje kusherehekea ushindi wa Chadema hapa nyumbani, kabla ya viongozi hao kwenda kuapishwa Dodoma.”
 
Alikuwa akizungumza na mwandishi wa makala hii nyumbani kwake eneo la Shangarai, wilayani Tengeru, Mkoa wa Arusha.
 
Kauli ya Mzee Mtei imekuja siku chache baada ya Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, mwishoni mwa mwezi ulipita kuwa chama hicho kimeandaa mikakati ya kutwaa dola Oktoba, mwaka huu.
 
Golugwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, anasema hawataki tu kuwa na chama maarufu ila kuchukua dola, tena sio miaka mingi ijayo ila Oktoba mwaka huu.
 
Akiweka msisitizo, Mtei anasema uchaguzi mkuu ujao ndio utadhihirisha matakwa ya demokrasia.
 
Anasema Chadema itachagua mgombea makini mwenye maadili na sifa ya kuongoza nchi. Mtu mwenye upeo na mawazo ya maendeleo kwa wananchi na taifa.
 
Ukawa
 
Akizungumzia kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anasema mgombea wa Chadema atashindanishwa na wagombea wengine kutoka umoja huo kwa mujibu wa makubaliano yao ya kusimamisha mgombea mmoja.
 
“Mimi ninaamini katika demokrasia ya ushindani, ndiyo demokrasia yenyewe kwamba kila chama kichague mgombea mmoja na kumshindanisha ili kumpata mgombea bora atakayekubalika,” anasema.
 
Hata hivyo,  anasema, “hatutakubali kuangusha wengine ili kumpata mmoja, lakini tukimpata mmoja huyo aliyeachwa tutamweleza aendelee kubaki kwenye chama.”
 
Anasema anaamini katika siasa au demokrasia za ushindani na kama kuna chama hakina mwelekeo huo basi kinaweza kufa.
 
Kuhusu uchaguzi mkuu, anasema, “Tunatarajia utakuwa uchaguzi huru, kila lazima ashiriki na kikubwa zaidi kupiga kura ili kuhakikisha kwamba wanatumia uhuru wao,” anasema.
 
Akitahadharisha kuhusu uvunjifu wa demokrasia katika uchaguzi, haraka haraka anakionya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kutumia pesa za walipakodi ambazo baadhi ya wagombea wao waliziiba zamani.
 
Anasema kwa muda mrefu chama hicho kimekuwa kikivuruga chaguzi mbalimbali na kuzifanya kuwa sio huru na wakati mwingine kimekuwa kikitumia mbinu za kupeleka mafisadi na watu walioiba fedha za walipa kodi kuhakikisha wagombea wa CCM wanapita.
 
“Wasitumie pesa zetu ambazo walituibia zamani na wengine ambao wamezificha nje ya nchi kuhonga watu wetu ili wasishiriki,” anasema na kucheka kidogo, na kuongeza, “hata zile fedha za IPTL ni zetu.”
 
Anasema kuna baadhi ya watu walisema wasusie uchaguzi mkuu, lakini anaona lazima washiriki na kutekeleza demokrasia yao.
 
Anasema anayo matumaini makubwa ya Chadema kuungwa mkono na watu wengi na hiyo inatokana na jinsi walivyokihamasisha na kukiuza chama hicho kwa wananchi na sasa kinakubalika.
 
“Kutokana na mwamko wa chama chetu na jinsi tulivyowahamasisha wananchi; na CCM inavyotumia nguvu kubwa kupambana na Chadema, ikiwa ni pamoja na nguvu ya ufisadi kuhonga wanachama ili kuleta mgongano ndani ya chama, nadhani wananchi kwa kuelewa hilo wanaweza kutuunga mkono katika harakati zetu za kutwaa dola Oktoba  2015,” anasema.
 
Anasema nafasi zote za wagombea katika uchaguzi mkuu kuanzia udiwani, ubunge na urais, wataungwa mkono na wananchi na kushinda na ishara hii inatokana na matokeo mazuri ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ulifanyika Desemba 14, mwaka jana.
 
Mathalan, anasema, “katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tumeonyesha kuwa sisi ndio chama kinachokubalika na sasa tutaendelea katika ngazi kata, majimbo na taifa.”
 
Anasema mikakati mingi ya kukinadi chama ndiyo ilisaidia kukifikisha hapa kilipo hali ambayo inawafanya waendelee kusomba watu wote kuanzia ngazi ya mashina, kitongoji, kijiji, mtaa, kata, tarafa, jimbo hadi taifa, na hii ndiyo kielelezo cha ushindi.
 
Changamoto BVR
 
Anaangalia changamoto katika mfumo wa kielektroniki wa kuandikisha wapiga kura (BVR) kama teknolojia ambayo haiwezi kuepukika katika nyakati hizi za maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia.
 
Hata hivyo, anasema matatizo yanayotokana na mfumo huo ni kwa sababu ya uwezo mgogo wa serikali na nchi.
 
Anasema serikali haikuweza kuandaa wataalam wenye uwezo wa kuzifanyia matengenezo mashine hizo au namna ya kuziendesha.
 
“Ni lazima na mwelekeo ulivyo, sasa ni lazima tutumie vifaa hivyo, kama shida itakuwa muda hautoshi, wanaweza kuongeza muda hadi Julai au Agosti, ili kuwapa watu wengi nafasi ya kujiandikisha na hivyo kupiga kura.
 
CCM imeshindwa?
 
Kuhusu CCM, Mzee Mtei hamung’unyi maneno, anasema moja kwa moja kwamba chama hicho kikongwe kimeshindwa na kupoteza mvuto kwa Watanzania. Kwa kifupi anasema hakikubaliki isipokuwa kwa wale wachache wenye maslahi nacho.
 
Anataja kwa mfano, Watanzania wanakufa kwa njaa kuanzia Ukerewe, mkoani Mwanza hadi Rombo, mkoani Kilimanjaro.
 
Anasema wakati wananchi wanakufa njaa, yapo mashamba mengi na makubwa yameshindwa kulima, huku fedha nyingi ambazo zinatolewa na washirika wa maendeleo haziwafikii wahusika.
 
Migogoro ndani ya chama
 
Anasema inapotokea inakiimarisha chama, na inatakiwa kutatuliwa kwa misingi ya kidemokrasia.
 
“Unajua kila mwanasiasa lazima awe ambitious, atake ukubwa kuliko pale alipo; na hii ni demokrasia, lazima kuwa na ushindani,” anasema.
 
Pamoja na siasa, Mzee Mtei anajishughulisha na kilimo cha mahindi, kahawa na ufugaji wa nguruwe na ng’ombe wa maziwa.
 
Anasema kwa mfano, mwaka huu amavuna tani 1, O30 za mahindi katika shamba lake la hekari 95.
 
Anasema ameuza mahindi hayo na kutenga magunia machache kwa ajili ya chakula chake kwa mwaka mzima, magunia 40 kwa ajili ya chakula cha nguruwe wake 37 yakiwemo madume mawili.
 
CHANZO: NIPASHE

Wednesday, March 4, 2015

Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi
Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi

Wanawake wataka mafanikio zaidi

WAKATI Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kusherehekea Siku ya Wanawake, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), umeainisha changamoto kadhaa zinazowakabiri wananwake nchini. Anaandika Sarafina Lidwino... (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika maadhimisho ya miaka 20 ya azimio la Ulingo wa Beijing, Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi amesema, siku hii hukutanisha wanaharakati wote wanaotetea haki za wanawake ili kujadili mafanikio na changamoto na jinsi ya kukabiliana nazo.
Liundi amesema, pamoja na mafanikio waliyoyapata hususani katika nyanja za kisiasa ya kuongezeka kwa viongozi wanawake, lakini bado kuna mapungufu katika uwezeshaji katika uongozi wao.
Amesema, mbali na kuongezeka kwa shule, bado hazikidhi mahitaji, majengo yapo lakini waalimu ni wachache na wengi hawana ujuzi, mabweni hakuna, umbali mrefu unaosababisha wasichana kupata mimba.   
Kwa mujibu wa Liundi, Serikali imejitahidi kujenga vituo vya afya, lakini changamoto iliyopo ni wahudumu hakuna wala dawa. Hivyo waathirika wakubwa ni wanawake, haswa wakati wa kujifungua, hukosa huduma na kupoteza maisha.
Lihundi amesema, mzigo wa majukumu unamwelemea sana mwanamke, hivyo kukosa muda wa kushiriki katika shughuri za kimaendeleo na uchumi.
Ameongeza kuwa bado kuna maendeleo ya vitu wakati wananchi walio wengi wanazidi kuathirika na mfumo uliopo wa kiuchimi; mabenki yapo lakini hakuna anayepata mkopo, soko limekuwa holela, vitu visivyokuwa na viwango vimejaa sokono, wakati bidhaa zetu zinakosa soko.
“Sekta zisizo rasmi, ambapo wanawake wengi ndio wapo huko haijaweza kumkomboa mwanamke na kumtoa katika duru ya umaskini. Ajira bado ni tatizo kubwa kwa wanawake Tanzania,” amesema Liundi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta, (EWURA), Felix Ngamlagosi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta, (EWURA), Felix Ngamlagosi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

EWURA yashusha tena bei ya mafuta

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa ambazo zitaanza kutumika kuanzia Machi 4, 2015. Anaandika Mwandishi wetu… (endelea).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi, bei kikomo kwa rejereja kwa mkoa wa Dar es Salaam zitakuwa sh. 1,652 (petroli), 1,563 (dizeli) na 1,523 (mafuta ya taa) wakati bei kikomo za jumla ni sh. 1,547.19 (petroli), 1,457.58 (dizeli) na 1,547.19 (mafuta ya taa).
Ngamlagosi anasema bei za jumla na za rejareja kwa aina zote za mafuta, yaani, petroli, dizeli na mafuta ya Taa zimeshuka ikilinganishwa na bei katika toleo lililopita la Februari 4, 2015.
“Katika toleo hili, bei za rejareja kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kwa viwango vifuatavyo: Petroli sh. 116/lita sawa na asilimia 6.57, Dizeli sh. 145/lita sawa na asilimia 8.49 na Mafuta ya Taa sh. 134/lita sawa na asilimia 8.08.,” amesema.
Aidha, kwa kulinganisha matoleo haya mawili, bei za jumla zimepungua kama ifuatavyo: Petroli, sh. 119.23/lita sawa na asilimia 7.16, Dizeli, sh. 147.94/lita sawa na asilimia 9.21, na Mafuta ya Taa, sh. 136.79/lita sawa na asilimia 8.80.
Kuendelea kushuka kwa bei za mafuta katika soko la ndani kumetokana na kuendelea kushuka kwa bei za mafuta katika soko la Dunia.
Mkurugenzi huyo anaongeza kuwa, bei za mafuta masafi (refined petroleum products) katika soko la dunia, kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimepungua kati ya Julai 2014 na Januari 2015 kwa Dola 536/tani, Dola 400/tani na Dola 440/tani sawia sawa na punguzo la asilimia 53, 46 na 48 sawia.
“Kati ya Septemba 2014 na Machi 2015 bei za Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa katika soko la ndani zimepungua kwa jumla ya kiasi cha sh. 615/lita, sh. 528/lita na Sh 517/lita sawia ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 27, 25 na 25, sawia,” amesema.
Katika kipindi husika, thamani ya shillingi ya Tanzania kulinganisha na dola ya Marekani ilishuka kwa asilimia 8. Bei ya mafuta kwenye soko la ndani ingeweza kupungua zaidi kama thamani ya shillingi isingeendelea kudhoofu.
Amesema kuwa kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 354 la tarehe 26 Septemba 2014.
Chanzo cha mwanahalisi online

Baadhi ya maafa ya mvua yaliyotokea nchini
Baadhi ya maafa ya mvua yaliyotokea nchini

Mvua ya mawe Shinyanga yaua 38 na kujeruhi 60 

WATU 38 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa vibaya kufuatia mvua kubwa ya mawe iliyonyesha usiku wa kuamkia leo na kusababisha mafuriko katika Kijiji cha Mwakata,  Kata ya Isaka Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga. Anaandika Mwandishi wetu… (endelea).

Awali, MwanaHalisi Online, ilikariri taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, akisema kuwa mvua hiyo imeezua na kuharibu nyumba, kusomba mazao mashambani, mali, vyakula na mifugo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha amethibitisha tukio hilo lilitokea usiku wa Machi 3 mwaka huu, majira ya saa 3:00 usiku.
Kwa mujibu wa Kamugisha, watu 35 walifariki papo hapo huku majeruhi zaidi ya 60 wakikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa ajili ya matibabu. 
MwanaHalisi Online limeelezwa kuwa kati ya majeruhi 60 waliofikishwa hospitali, watatu walifariki wakati wakiendelea na matibabu.
Naye mganga mkuu wa hospitali hiyo, Joseph Ngowi, amesema kuwa idadi kamili ya watu waliojeruhiwa au kufa haikuwa imefahamika na kwamba wametuma madaktari kwenda kijijini hapo kwa ajili ya huduma.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, amesema Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya imekutana kwa ajili ya kutathmini takwimu za uharibifu.
RAIS anayeondoka madarakani nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba
RAIS anayeondoka madarakani nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba

Huyu ndiye Rais Pohamba mshindi wa tuzo ya Mo Ibrahim

RAIS anayeondoka madarakani nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba (79), ameingia kwenye historia ya washindi wa tuzo ya dola milioni tano ya Mo Ibrahimu ya uongozi wa Afrika.
Rais huyo ambaye anatarajiwa kumkabidhi madaraka yake kwa rais mteule, Hage Geingob, anakuwa kiongozi wan ne kukwaa tuzo hiyo, akitanguliwa na Joachim Chissano wa Msumbiji (2007), Festus Mogae wa Botswana (2008) na Pedro Pires wa Cape Verde (2011).
Tuzo hiyo ya dola milioni 5 hutuzwa kiongozi wa Kiafrika aliyechaguliwa na anayeongoza kwa njia bora na kuinua maisha ya watu na kuondoka madarakani.
Rais mtaafu wa Msumbiji mwaka 2005, Chissano ndiye alikuwa wa kwanza kutunukiwa tuzo hii ya heshima mwaka 2007, huku miaka mingine ikipita bila kupata mshindi kutokana ugumu wa vigezo.
Salim Ahmed Salim- Mwenyekiti wa kamati inayotafuta mshindi wa tuzo hiyo iliyotolewa Nairobi nchini Kenya, anasema Namibia chini ya Pohamba imeweza kuwa na utawala mzuri na kujiletea heshima. Anaongeza kuwa Namibia chini ya Pohamba ina demokrasia ya kweli, imekuwa imara na inayoheshimu uhuru wa habari na haki za binadamu,
Tuzo hii ni malipo ya awali ya dola za Marekani milioni 5 (sawa sh. bilioni 8.3) zinazotolewa kwa awamu kwa kipindi cha miaka kumi, zaidi ya malipo haya Pohamba atapewa dola laki 2 kwa kila mwaka kwa maisha yake yote.
Pia tuzo hii inaaminika kuwa kubwa na yenye thamani zaidi duniani ikiipiku Tuzo ya Nobeli ya Amani (Nobel Peace Prize) kwa zaidi ya mara tatu na nusu. Mshindi wa Tuzo ya Nobel anapewa kiasi cha dola za Marekani milioni 1.3.
Tuzo ya Mo Ibrahim inatolewa kwa Rais aliyemaliza muda wake Afrika na mchakato wa kumpata unafanywa na kamati maalumu ya watu mashuhuri; kamati hii pia inajumuisha watu wengine wawili waliowahi kupata tuzo ya Nobel.
WASHINDI
2007-Joachim Chissano (Msumbiji)
2008-Festus Mogae (Botswana)
2009- Hamna tuzo iliyotolewa
2010- Hamna tuzo iliyotolewa
2011-Pedro Pires (Cape Verde)
2012-Hamna tuzo iliyotolewa
2013-Hamna tuzo iliyotolewa
2014- Hifikepunye Pohamba (Namibia)
Tuzo hii inatolewa ili kutambua na kusherehekea viongozi wa Afrika waliotumia uwezo wao kuzijenga nchi zao kwa kuimarisha uchumi na huduma za kijamii na waliofanya juhudi za kupunguza umaskini na uimarishaji wa maendeleo endelevu yenye usawa kwa wote.
Utolewaji wa tuzo hii unaifanya Afrika iendelee kufaidika na uzoefu na weledi wa marais waliomaliza muda wao wa kutawala. Tuzo hii inawawezesha kuendelea kufanya shughuli nyingine za kijamii wanapomaliza muda wao wa kutawala.
Vigezo vinavyotumika katika kutafuta mshindi ni pamoja na Rais aliyemaliza muda wake katika nchi mojawapo ya Afrika; awe ameng’atuka madarakani sio zaidi ya miaka mitatu iliyopita; aliyechaguliwa kidemokrasia; aliyetumikia muda wake kwa mujibu wa katiba na aliyeonyesha kwa vitendo kuwa na sifa za pekee za uongozi.
Pohamba ni nani?
Huyu amezaliwa mwaka 1935 huko Namibia ya Kaskazini, eneo lililokuja kuwa ngombe ya harakati za SWAPO- Chama ambacho tangu uhuru 1990 kimekuwa kikitawala na kushinda chaguzi kwa ushindi wa kishindo.
Pohamba alipata elimu yake kwa wamisionari na akaajiriwa na mgodi wa Shaba akiwa kijana. Ni mwenza wa uanzilishi wa SWAPO na rafiki yake Sam Nujoma, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Namibia.
Aliwahi kufungwa kwa sababu za harakati na utawala uliosaidiwa na makaburu. Amekuwa Waziri wa Ardhi baada ya uhuru, aliyeleta mabadiliko kwenye sekta ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuigawa kwa wananchi.
Pohamba alipendekezwa na Nujoma kurithi mikoba ya urais mwaka 2004 na sasa mikoba hiyo anamwachia Hage Geingob.
Tuzo hii inafadhiliwa na Mo Ibrahim mzaliwa wa Sudan lakini ana uraia wa Uingereza; ni mjasiriamali na bilionea anayemiliki biashara ya mawasiliano ya simu kwakuwekeza katika nchi za Afrika.
Tuzo hii inatolewa kila mwaka lakini tangu 2007 ilipoanza ni marais watatu tu walizawadia, huku Nelson Mandera akizawadia kwa heshima.
Chanzo cha habari mwanahalisi online

Mwili wa Marehemu, John Damiano Komba
Mwili wa Marehemu, John Damiano Komba

Kapteni Komba afa na deni la CRDB

MBUNGE wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba, amefariki dunia kutokana na kuzongwa na mzigo wa madeni, likiwamo mkopo kutoka Benki ya CRDB.
Taarifa zinasema, benki hiyo ilitoa kiasi cha sh. 12 bilioni kwa mwanasiasa huyo mwaka 2009, lakini hadi mauti yanamkuta, alikuwa hajaweza kulipa deni hilo. Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).
Habari zinasema, wakati Komba akihaha kuokoa nyumba yake kutokana na tanganzo la benki ya CRDB kwenye vyombo vya habari; huku akiwa tayari ameonekana kukata tamaa; ghafla Jumamosi jioni alipatwa na shinikizo la damu na kufariki dunia.
Mamilioni hayo ya shilingi yalitolewa na CRD Benki kwa mbunge huyo kwa ajili ajili ya kuendeleza shule zake mbili alizokuwa akizimiliki – shule ya Sekondari ya Bakili Muluzi na Shule ya Msingi ya Coletha – zilizoko jijini Dar es Salaam.
Hadi anafariki dunia, Komba alikuwa amebakiza kiasi cha zaidi ya sh. 78.5 milioni. Deni la Benki linatokana na mkopo pamoja na riba ya asilimia 17 katika kipindi cha miaka mitano ya uhai wa mkopo.
Komba amefariki dunia Jumamosi iliyopita, miezi mitatu baada ya Benki ya CRDB kuuza shule zake.
Mbali na kuuza shule, benki iliuza vifaa mbalimbali, likiwamo eneo la ukubwa wa mita za mraba zaidi ya 34,000 lililotumika kutoa mkopo wa sh. 900 milioni mwaka 2009.
Shule za Komba pamoja na vifaa vyake, vimenunuliwa na mfanyabiashara mmoja mmoja.
Gazeti hili limeelezwa kuwa Komba alijaribu, bila mafanikio, kushawishi serikali kununua shule yake; na kwamba alitinga hadi ikulu na makao makuu ya CCM kuomba msaada ili shule na nyumba yake visiuzwe.
Hata hivyo, taarifa zinasema, Komba hakufanikiwa kupata msaada wa kuzuia shule kuuzwa. Hadi anafariki dunia benki ilikuwa inajiandaa kuuza nyumba yake.
“Yule bwana alifika hadi ikulu kuomba msaada ili nyumba yake isiuzwe. Alitaka serikali imsaidie kununua shule yake; au kuomba benki izuie kwa muda uuzaji kwa kuwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lilikuwa limekubali kununua eneo hilo kwa bei ya soko,” ameeleza mtoa taarifa.
Baada ya shule kuuzwa na deni kushindwa kumalizika, mtoa taarifa anasema, Komba alirudi tena ikulu na CCM kuomba msaada wa kukwamua nyumba yake.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alijaribu kunusuru shule ya Komba kupigwa mnada kwa kuiandikia benki ya CRDB kumpa mwanasiasa huyo muda zaidi wa nyongeza ili kulipa deni lake.
Hata hivyo, pamoja na maombi ya Pinda kupewa nafasi, bado Komba alishindwa kulipa deni hilo.
Komba aliyekuwa anajulikana kwa jina maarufu la “Mzee wa kutoa mitaji kwa vimwana,” alizikwa juzi Jumanne, katika jimbo lake la uchaguzi la Mbinga Magharibi.
Chanzo cha habari mwanahalisi online

Sunday, February 15, 2015

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa

Benjamin Mkapa: Tujadili sifa, tusijadili mtu

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, amejitosa katika kinyang’anyiro cha urais cha mwaka kesho. Amewekeza kwa waziri mkuu Mizengo Pinda.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia fedha za mradi wa kusaidia maboresho ya sekta ya afya vijijini, Jumamosi iliyopita, Mkapa alisema, Pinda ni miongoni mwa viongozi wachache waadilifu ndani ya serikali.
Alisema, Pinda “amefanya kazi nzuri. Anakubalika kwa wananchi na amekuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa viongozi waliopo madarakani.”
Harambee ambako Mkapa alimporomoshea sifa waziri mkuu huyo, iliandaliwa na taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS. Iliendeshwa na Pinda mwenyewe.
Katika hili la kutoa maoni yake katika kumtafuta mrithi wa Rais Jakaya Kikwete; au rais mwingine atakayekuja miaka mitano na hata 10 ijayo, Mkapa yumkini ana sura mbili.
Akiwa raia wa Jamhuri ya Muungano, Mkapa anayo haki ya kutoa maoni katika jambo lolote linalohusu taifa lake. Anayo haki ya kueleza kile kilichomo moyoni mwake.
Anaweza kukielekeza chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – ikiwa chama hicho kitapenda kupokea ushauri wake juu ya mgombea wanayeona anastahili kupeperusha bendera yao.
Aidha, yeye akiwa rais mstaafu – kwa sababu anaishi kwa kodi za wananchi – ana wajibu wa ziada wa kulikumbusha taifa lake juu ya masuala muhinu ya kusimamia. Hakuna shaka kuwa anao wajibu na haki hiyo.
Hata hivyo, kabla ya kutoa maoni yake katika suala zito kama hili; au kujitosa katika kumfanyia kampeni Pinda, Mkapa angeeleza – kwa maoni yake – rais ajaye anatakiwa kulifanyia nini taifa lake. Yapi majukumu yake ya msingi. Zipi changamoto. Yapi matatizo. Na aonyeshe njia zitakazoweza kutumika kutatua matatizo hayo.
Ni kama ilivyokuwa wakati wa uhai wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alipojitosa kujadili mrithi wa Alli Hassan Mwinyi, Nyerere hakujadili mtu. Alijadili sifa za kiongozi anayetakiwa kumrithi Mwinyi. Lakini huyu Mkapa anajadili mtu. Hajadili sifa.
Nyerere alieleza matatizo yanayokabili taifa lake. Akasema, “…rushwa inanuka nchini.” Akataka kiongozi atakayekuja sharti awe mwadilifu. Aliyetayari kupambana na rushwa bila woga wala aibu.
Hivyo basi, changamoto kuu ya sasa, ni kutafuta mgombea urais ambaye atasimamia uadilifu wa kimfumo. Siyo uadilifu wa mtu binafsi.
Rais atakayekuja, ni sharti awe na ubavu wa kukabiliana na ufisadi na mafisadi. Awe na ujasiri wa kuzuia wizi wa mali ya umma; mikataba ya kinyonyaji; ujangili; dawa za kulevya na ufujaji kodi za wananchi.
Kiongozi anayetakiwa ni yule atakayekuwa tayari kutumia mamlaka ya umma kwa maslahi ya umma. Atakayefuata miiko na maadili ya uongozi. Yule ambaye hatatumia madaraka vibaya; au kutumia mamlaka ya umma kulipa fadhila.
Mathalani, kiongozi aliyepo sasa – Rais Jakaya Kikwete – mara baada ya kuingia ikulu, wengi alioteua walikuwa wanachama wa kundi lake la wanamtandao.
Hivyo basi, kitendo cha Mkapa kumpigia kampeni Pinda kwa kujadili mtu badala ya sifa, kinamuondolea fursa adhimu ya kushiriki kulitafutia taifa lake rais bora.
Sura ya pili ya Mkapa ni hii: Hana sifa ya kuwaambia wananchi, yupi ni rais bora na anayeweza kuwa sahihi kukabiliana na matatizo yaliyopo. Kwanini? Kwa kuwa naye hana sifa ya uandilifu.
Ikiwa Nyerere aliyekuwa msafi aliaminisha wananchi kuwa “Mkapa ni Mr. Clean”- Bw. Msafi, lakini ghafla aliyeitwa msafi akawa “mchafu,” Mkapa aliyechafuka hawezi kumjua msafi.
Aliyeitwa msafi, ndiye aliingia Ikulu na kuanza kutelekeza usafi. Akaanzisha kampuni ya biashara – ANBEM Co. Limited – kwa kutumia rasimali za umma.
Akabinafsisha mashirika ya umma, mithili ya shamba lisilo na mwenyewe.
Akaruhusu na, au kunyamazia ukwapuzi wa mabilioni ya shilingi serikalini na ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT).
Miongoni mwa fedha zilizoibwa, ni pamoja na zile zilizochotwa kupitia akaunti ya madeni ya nje (EPA), katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2005.
Hapa ndiko kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., ilipewa “zawadi” ya kiasi cha Sh. 70 bilioni kati ya Sh. 130 bilioni zilizochotwa BoT.
Ushahidi juu ya Mkapa kushiriki au kunyamazia wizi katika akaunti ya EPA, uliwekwa hadharani na Bhyidinka Michael Sanze, wakili katika kampuni ya mawakili ya Malegesi Law Chambers ya Dar es Salaam.
Sanze ndiye alishuhudia mkataba kati ya Kagoda na serikali. Wakili huyo anakiri kuwa ni yeye aliyeshuhudia mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje.
Mbali na fedha zilizoibwa katika akaunti ya EPA, mabilioni mengine ya shilingi yalikwapuliwa na makampuni ya Tangold Limited, Deep Green Finance Limited, Meremeta na Mwananchi Gold Ltd.
Hakuishia hapo. Ni Mkapa aliyeingiza nchini kampuni ya kigeni kutoka Afrika Kusini – Net Group Solutions – ili kuikabidhi shirika la umeme la taifa (Tanesco), kuvuna wasichopanda.
Kazi ya Net Group ndani ya shirika la umma, haikuwa kuzalisha; kuwekeza mtaji; au kutafuta vyanzo vipya vya umeme. Kazi ya kampuni ya “makaburu’ ilikuwa kukusanya mapato na kukamua wananchi.
Katika kipindi cha miaka saba ya mkataba kati ya serikali na Net Group, Tanesco ikashindwa kuzalisha umeme unaoendana na mahitaji. Ikashindwa kuwekeza katika miradi mipya ya umeme.
Matokeo yake, miundo mbinu ya umeme ikachakaa. Taifa likatumbukia katika giza la milele na milele. Tanesco iliyokuwa imara, haraka ikatumbukia katika mikataba ya kinyonyaji ya kuzalisha umeme wa dharula.
Tanesco iliyokuwa inajiendesha kwa faida, ikatumbukia katika madeni makubwa yanayohatarisha hata uhai wa shirika lenyewe.
Miongoni mwa mikataba ya kinyonyaji ambayo imefungwa kutokana na shirika kutafunwa na kampuni iliyoletwa na Mkapa, ni pamoja na mkataba wa kinyonyaji wa kuzalisha umeme wa Richmond na dada yake Dowans.
Makampuni mengine, ni Aggreko; Symbion; Songas na “ndoa ya mkeka” iliyofungwa kwa mara ya pili kati yake na kampuni ya Independent Powel Tanzania Limited (IPTL).
Mkataba wa kwanza kati ya IPTL na serikali ulifungwa Septemba 1994. Katika mkataba huu, serikali ilijifunga kulipa IPTL kiasi cha Sh. 6 bilioni kwa mwezi kwa umeme usiokuwepo.
Januari mwaka huu, mkataba mpya kati ya Tanesco na IPTL kupitia anayeitwa mmiliki mpya, kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), ulifungwa katika mazingira yaliyosheheni utata.
Taarifa zinasema, mkataba kati ya Tanesco na PAP, hauna tofauti yoyote kubwa na mkataba kati ya Tanesco na IPTL.
Ni Mkapa na utawala wake waliobinafsisha mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya na kuumilikisha kwa watu waliokaribu na rais. Bunge la Jamhuri lilielezwa na Mtendaji Mkuu wa Kiwira Coal and Power Limited (KCP), Francis Tabaro, kuwa mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na watu walio karibu na Mkapa.
Waliotajwa kwa mujibu wa taarifa hizo, ni mtoto wa kuzaa wa Benjamin Mkapa, Nick (Nicholas) Mkapa na mkewe Foster Mkapa. Hawa wanamiliki kampuni ya Fosnik Enterprises, moja ya makampuni yanayomiliki mgodi.
Mkurugenzi mwingine ambaye pia ni mmiliki ametajwa kuwa ni D. Maembe.
Kampuni ya Mkapa ni miongoni mwa makampuni manne yaliyoungana na “kumilikishwa” mgodi wa Kiwira ambao ulikuwa mali ya serikali kwa asilimia 100. KCP ilianzishwa Julai 2005.
Si hayo tu. Akiwa ikulu ya magogoni, Mkapa alimpa mkewe, Anne Mkapa, mamlaka ya kukusanya fedha na kuendesha kinachoitwa, “Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote” (EOTF). Akautumia mfuko huo, kujilimbikizia mali nyingi.
Hadi wanaondoka ikulu, siyo Mpaka wala mkewe, aliyesema fedha za kuendesha mfuko ya EOTF zilitoka wapi. Mafanikio yaliyofikiwa wala hesabu za mfuko ni siri yao.
“Mfuko wa Mama Mkapa,” ulianzishwa mara baada ya Mkapa kuingia madarakani, Novemba 1995. Kwa muda wote ambao Mkapa alikuwa ikulu, mfuko huu ulikuwa unaendeshea shughuli zake katika majengo ya Ikulu.
Hata gharama za bili ya maji, umeme, simu na mishahara ya wafanyakazi vililipwa na serikali. Misaada na michango iliyotolewa na wafadhili, mingi ilitolewa kwa kuwa mwenyekiti wake ni mke wa rais. Mfuko uligeuka, ingawa siyo rasmi, kuwa wa umma.
Hakika, kuna mengi yamefanyika chini ya utawala wake. Ameingiza nchi katika mikataba ya kinyonyaji katika uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali nchini, ukiwamo mgodi wa Tulawaka, Bulyanhulu, North Mara na Geita Gold Mine.
Ameuza nyumba za serikali. Naye akajimilikisha baadhi ya nyumba hizo. Akaruhusu waziri wake, John Pombe Magufuli, naye kujimilikisha.
Akasimamia uuzaji unaofanana na utoaji bure mashirika ya umma, ikiwamo “utoaji bure” iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Benki iliyokuwa na matawi nchi mzima na mtaji kedekede, iliuzwa kwa bei ya kutupwa kwa benki ya ABSA ya Afrika Kusini.
Leo hii, NBC iliyoelezwa inauzwa kwa watu wenye uwezo wa kuiendesha kuliko wazalendo waliopo, iko hoi kibiashara. Imepoteza mtaji; na sasa inaendeshwa kwa hisani ya BoT.
Ni Mkapa aliyeuza shirika la ndege la taifa (ACT); migodi na mashamba.
Katika muktadha huo, mtu mwenye yote haya, anapata wapi uhalali na ujasiri wa kutupendekezea mtu ambaye anadai ni mwadilifu? Mtu mwenye viwango vya chini vya uadilifu kama Mkapa, anawezaje kumjua mwadilifu wa dhati? Hawezi.
Ni bahati njema kuwa Nyerere alifariki dunia kabla Mkapa hajamaliza ngwe yake ya kwanza ya uongozi, Oktoba 2010. Vinginevyo, asingeruhusu Mkapa kushika madaraka kwa vipindi viwili mfululizo. Nyerere alifariki dunia 14 Oktoba 1999.
Taarifa zinanukuu baadhi ya viongozi waandamizi nchini wakisema, Nyerere alikuwa amejiapiza kumzuia Mkapa kuwa rais kwa kipindi cha pili. Alimchoka.
Hivyo basi, tukimjadili Mkapa na yule anayempigia chapuo, tunawaona wana sifa moja inayofanana. Wote wawili hawaheshimu utawala wa sheria. Ni wababe.
Mara mbili, Pinda aliagiza ndani ya bunge vyombo vya dola kuchukua sheria mkononi. Mara ya kwanza, ni pale alipoagiza watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi – Albino – wauawe.
Mara ya pili ni pale Pinda alipoagiza kupigwa kwa wananchi waliokuwa wanatekeleza matakwa yao ya kikatiba kupinga mradi wa gesi kwenye mikoa ya Kusini, wakisema hautawanufaisha – kama ilivyo kwa wanaoishi katika maeneo au karibu na migodi ya dhahabu na alimamsi.
Katika kipindi cha utawala wake, Mkapa aliruhusu vyombo vya dola – jeshi la polisi; vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) vya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) na makundi mengine ya Janjaweed – kuendesha mauaji makubwa katika Visiwani Pemba na Unguja, 26 na 27 Januari 2001.
Katika tukio hilo lililoweka doa baya taifa hili, wanakaokadiriwa kati ya watu 30 na 75 waliuawa.
Sifa nyingine ambayo Pinda anayo, ni kutojiamini. Yawezekana hiyo ndiyo iliyomsukuma Mkapa kumuunga mkono kutimiza ndoto zake.
Anajua ikiwa Pinda atafanikiwa kuwa rais, atamburuza. Atamyumbisha. Anajua chini ya Pinda machafu yake yatalindwa. Nje ya hapo, Mkapa hana kingine cha kumsifia Pinda.
Tusikubali kuruhusu kuchaguliwa mgombea, kabla ya kukubaliana juu ya sifa za rais tunayemhitaji