Sunday, February 15, 2015

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa

Benjamin Mkapa: Tujadili sifa, tusijadili mtu

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, amejitosa katika kinyang’anyiro cha urais cha mwaka kesho. Amewekeza kwa waziri mkuu Mizengo Pinda.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia fedha za mradi wa kusaidia maboresho ya sekta ya afya vijijini, Jumamosi iliyopita, Mkapa alisema, Pinda ni miongoni mwa viongozi wachache waadilifu ndani ya serikali.
Alisema, Pinda “amefanya kazi nzuri. Anakubalika kwa wananchi na amekuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa viongozi waliopo madarakani.”
Harambee ambako Mkapa alimporomoshea sifa waziri mkuu huyo, iliandaliwa na taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS. Iliendeshwa na Pinda mwenyewe.
Katika hili la kutoa maoni yake katika kumtafuta mrithi wa Rais Jakaya Kikwete; au rais mwingine atakayekuja miaka mitano na hata 10 ijayo, Mkapa yumkini ana sura mbili.
Akiwa raia wa Jamhuri ya Muungano, Mkapa anayo haki ya kutoa maoni katika jambo lolote linalohusu taifa lake. Anayo haki ya kueleza kile kilichomo moyoni mwake.
Anaweza kukielekeza chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – ikiwa chama hicho kitapenda kupokea ushauri wake juu ya mgombea wanayeona anastahili kupeperusha bendera yao.
Aidha, yeye akiwa rais mstaafu – kwa sababu anaishi kwa kodi za wananchi – ana wajibu wa ziada wa kulikumbusha taifa lake juu ya masuala muhinu ya kusimamia. Hakuna shaka kuwa anao wajibu na haki hiyo.
Hata hivyo, kabla ya kutoa maoni yake katika suala zito kama hili; au kujitosa katika kumfanyia kampeni Pinda, Mkapa angeeleza – kwa maoni yake – rais ajaye anatakiwa kulifanyia nini taifa lake. Yapi majukumu yake ya msingi. Zipi changamoto. Yapi matatizo. Na aonyeshe njia zitakazoweza kutumika kutatua matatizo hayo.
Ni kama ilivyokuwa wakati wa uhai wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alipojitosa kujadili mrithi wa Alli Hassan Mwinyi, Nyerere hakujadili mtu. Alijadili sifa za kiongozi anayetakiwa kumrithi Mwinyi. Lakini huyu Mkapa anajadili mtu. Hajadili sifa.
Nyerere alieleza matatizo yanayokabili taifa lake. Akasema, “…rushwa inanuka nchini.” Akataka kiongozi atakayekuja sharti awe mwadilifu. Aliyetayari kupambana na rushwa bila woga wala aibu.
Hivyo basi, changamoto kuu ya sasa, ni kutafuta mgombea urais ambaye atasimamia uadilifu wa kimfumo. Siyo uadilifu wa mtu binafsi.
Rais atakayekuja, ni sharti awe na ubavu wa kukabiliana na ufisadi na mafisadi. Awe na ujasiri wa kuzuia wizi wa mali ya umma; mikataba ya kinyonyaji; ujangili; dawa za kulevya na ufujaji kodi za wananchi.
Kiongozi anayetakiwa ni yule atakayekuwa tayari kutumia mamlaka ya umma kwa maslahi ya umma. Atakayefuata miiko na maadili ya uongozi. Yule ambaye hatatumia madaraka vibaya; au kutumia mamlaka ya umma kulipa fadhila.
Mathalani, kiongozi aliyepo sasa – Rais Jakaya Kikwete – mara baada ya kuingia ikulu, wengi alioteua walikuwa wanachama wa kundi lake la wanamtandao.
Hivyo basi, kitendo cha Mkapa kumpigia kampeni Pinda kwa kujadili mtu badala ya sifa, kinamuondolea fursa adhimu ya kushiriki kulitafutia taifa lake rais bora.
Sura ya pili ya Mkapa ni hii: Hana sifa ya kuwaambia wananchi, yupi ni rais bora na anayeweza kuwa sahihi kukabiliana na matatizo yaliyopo. Kwanini? Kwa kuwa naye hana sifa ya uandilifu.
Ikiwa Nyerere aliyekuwa msafi aliaminisha wananchi kuwa “Mkapa ni Mr. Clean”- Bw. Msafi, lakini ghafla aliyeitwa msafi akawa “mchafu,” Mkapa aliyechafuka hawezi kumjua msafi.
Aliyeitwa msafi, ndiye aliingia Ikulu na kuanza kutelekeza usafi. Akaanzisha kampuni ya biashara – ANBEM Co. Limited – kwa kutumia rasimali za umma.
Akabinafsisha mashirika ya umma, mithili ya shamba lisilo na mwenyewe.
Akaruhusu na, au kunyamazia ukwapuzi wa mabilioni ya shilingi serikalini na ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT).
Miongoni mwa fedha zilizoibwa, ni pamoja na zile zilizochotwa kupitia akaunti ya madeni ya nje (EPA), katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2005.
Hapa ndiko kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., ilipewa “zawadi” ya kiasi cha Sh. 70 bilioni kati ya Sh. 130 bilioni zilizochotwa BoT.
Ushahidi juu ya Mkapa kushiriki au kunyamazia wizi katika akaunti ya EPA, uliwekwa hadharani na Bhyidinka Michael Sanze, wakili katika kampuni ya mawakili ya Malegesi Law Chambers ya Dar es Salaam.
Sanze ndiye alishuhudia mkataba kati ya Kagoda na serikali. Wakili huyo anakiri kuwa ni yeye aliyeshuhudia mikataba ya Kagoda na makampuni mengine ya nje.
Mbali na fedha zilizoibwa katika akaunti ya EPA, mabilioni mengine ya shilingi yalikwapuliwa na makampuni ya Tangold Limited, Deep Green Finance Limited, Meremeta na Mwananchi Gold Ltd.
Hakuishia hapo. Ni Mkapa aliyeingiza nchini kampuni ya kigeni kutoka Afrika Kusini – Net Group Solutions – ili kuikabidhi shirika la umeme la taifa (Tanesco), kuvuna wasichopanda.
Kazi ya Net Group ndani ya shirika la umma, haikuwa kuzalisha; kuwekeza mtaji; au kutafuta vyanzo vipya vya umeme. Kazi ya kampuni ya “makaburu’ ilikuwa kukusanya mapato na kukamua wananchi.
Katika kipindi cha miaka saba ya mkataba kati ya serikali na Net Group, Tanesco ikashindwa kuzalisha umeme unaoendana na mahitaji. Ikashindwa kuwekeza katika miradi mipya ya umeme.
Matokeo yake, miundo mbinu ya umeme ikachakaa. Taifa likatumbukia katika giza la milele na milele. Tanesco iliyokuwa imara, haraka ikatumbukia katika mikataba ya kinyonyaji ya kuzalisha umeme wa dharula.
Tanesco iliyokuwa inajiendesha kwa faida, ikatumbukia katika madeni makubwa yanayohatarisha hata uhai wa shirika lenyewe.
Miongoni mwa mikataba ya kinyonyaji ambayo imefungwa kutokana na shirika kutafunwa na kampuni iliyoletwa na Mkapa, ni pamoja na mkataba wa kinyonyaji wa kuzalisha umeme wa Richmond na dada yake Dowans.
Makampuni mengine, ni Aggreko; Symbion; Songas na “ndoa ya mkeka” iliyofungwa kwa mara ya pili kati yake na kampuni ya Independent Powel Tanzania Limited (IPTL).
Mkataba wa kwanza kati ya IPTL na serikali ulifungwa Septemba 1994. Katika mkataba huu, serikali ilijifunga kulipa IPTL kiasi cha Sh. 6 bilioni kwa mwezi kwa umeme usiokuwepo.
Januari mwaka huu, mkataba mpya kati ya Tanesco na IPTL kupitia anayeitwa mmiliki mpya, kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), ulifungwa katika mazingira yaliyosheheni utata.
Taarifa zinasema, mkataba kati ya Tanesco na PAP, hauna tofauti yoyote kubwa na mkataba kati ya Tanesco na IPTL.
Ni Mkapa na utawala wake waliobinafsisha mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya na kuumilikisha kwa watu waliokaribu na rais. Bunge la Jamhuri lilielezwa na Mtendaji Mkuu wa Kiwira Coal and Power Limited (KCP), Francis Tabaro, kuwa mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na watu walio karibu na Mkapa.
Waliotajwa kwa mujibu wa taarifa hizo, ni mtoto wa kuzaa wa Benjamin Mkapa, Nick (Nicholas) Mkapa na mkewe Foster Mkapa. Hawa wanamiliki kampuni ya Fosnik Enterprises, moja ya makampuni yanayomiliki mgodi.
Mkurugenzi mwingine ambaye pia ni mmiliki ametajwa kuwa ni D. Maembe.
Kampuni ya Mkapa ni miongoni mwa makampuni manne yaliyoungana na “kumilikishwa” mgodi wa Kiwira ambao ulikuwa mali ya serikali kwa asilimia 100. KCP ilianzishwa Julai 2005.
Si hayo tu. Akiwa ikulu ya magogoni, Mkapa alimpa mkewe, Anne Mkapa, mamlaka ya kukusanya fedha na kuendesha kinachoitwa, “Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote” (EOTF). Akautumia mfuko huo, kujilimbikizia mali nyingi.
Hadi wanaondoka ikulu, siyo Mpaka wala mkewe, aliyesema fedha za kuendesha mfuko ya EOTF zilitoka wapi. Mafanikio yaliyofikiwa wala hesabu za mfuko ni siri yao.
“Mfuko wa Mama Mkapa,” ulianzishwa mara baada ya Mkapa kuingia madarakani, Novemba 1995. Kwa muda wote ambao Mkapa alikuwa ikulu, mfuko huu ulikuwa unaendeshea shughuli zake katika majengo ya Ikulu.
Hata gharama za bili ya maji, umeme, simu na mishahara ya wafanyakazi vililipwa na serikali. Misaada na michango iliyotolewa na wafadhili, mingi ilitolewa kwa kuwa mwenyekiti wake ni mke wa rais. Mfuko uligeuka, ingawa siyo rasmi, kuwa wa umma.
Hakika, kuna mengi yamefanyika chini ya utawala wake. Ameingiza nchi katika mikataba ya kinyonyaji katika uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali nchini, ukiwamo mgodi wa Tulawaka, Bulyanhulu, North Mara na Geita Gold Mine.
Ameuza nyumba za serikali. Naye akajimilikisha baadhi ya nyumba hizo. Akaruhusu waziri wake, John Pombe Magufuli, naye kujimilikisha.
Akasimamia uuzaji unaofanana na utoaji bure mashirika ya umma, ikiwamo “utoaji bure” iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Benki iliyokuwa na matawi nchi mzima na mtaji kedekede, iliuzwa kwa bei ya kutupwa kwa benki ya ABSA ya Afrika Kusini.
Leo hii, NBC iliyoelezwa inauzwa kwa watu wenye uwezo wa kuiendesha kuliko wazalendo waliopo, iko hoi kibiashara. Imepoteza mtaji; na sasa inaendeshwa kwa hisani ya BoT.
Ni Mkapa aliyeuza shirika la ndege la taifa (ACT); migodi na mashamba.
Katika muktadha huo, mtu mwenye yote haya, anapata wapi uhalali na ujasiri wa kutupendekezea mtu ambaye anadai ni mwadilifu? Mtu mwenye viwango vya chini vya uadilifu kama Mkapa, anawezaje kumjua mwadilifu wa dhati? Hawezi.
Ni bahati njema kuwa Nyerere alifariki dunia kabla Mkapa hajamaliza ngwe yake ya kwanza ya uongozi, Oktoba 2010. Vinginevyo, asingeruhusu Mkapa kushika madaraka kwa vipindi viwili mfululizo. Nyerere alifariki dunia 14 Oktoba 1999.
Taarifa zinanukuu baadhi ya viongozi waandamizi nchini wakisema, Nyerere alikuwa amejiapiza kumzuia Mkapa kuwa rais kwa kipindi cha pili. Alimchoka.
Hivyo basi, tukimjadili Mkapa na yule anayempigia chapuo, tunawaona wana sifa moja inayofanana. Wote wawili hawaheshimu utawala wa sheria. Ni wababe.
Mara mbili, Pinda aliagiza ndani ya bunge vyombo vya dola kuchukua sheria mkononi. Mara ya kwanza, ni pale alipoagiza watuhumiwa wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi – Albino – wauawe.
Mara ya pili ni pale Pinda alipoagiza kupigwa kwa wananchi waliokuwa wanatekeleza matakwa yao ya kikatiba kupinga mradi wa gesi kwenye mikoa ya Kusini, wakisema hautawanufaisha – kama ilivyo kwa wanaoishi katika maeneo au karibu na migodi ya dhahabu na alimamsi.
Katika kipindi cha utawala wake, Mkapa aliruhusu vyombo vya dola – jeshi la polisi; vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) vya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM) na makundi mengine ya Janjaweed – kuendesha mauaji makubwa katika Visiwani Pemba na Unguja, 26 na 27 Januari 2001.
Katika tukio hilo lililoweka doa baya taifa hili, wanakaokadiriwa kati ya watu 30 na 75 waliuawa.
Sifa nyingine ambayo Pinda anayo, ni kutojiamini. Yawezekana hiyo ndiyo iliyomsukuma Mkapa kumuunga mkono kutimiza ndoto zake.
Anajua ikiwa Pinda atafanikiwa kuwa rais, atamburuza. Atamyumbisha. Anajua chini ya Pinda machafu yake yatalindwa. Nje ya hapo, Mkapa hana kingine cha kumsifia Pinda.
Tusikubali kuruhusu kuchaguliwa mgombea, kabla ya kukubaliana juu ya sifa za rais tunayemhitaji

Nigeria yahairisha Uchaguzi Mkuu

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan

Nigeria yahairisha Uchaguzi Mkuu

Tume ya Uchaguzu ya Nigeria ilitangaza mabadiliko haya siku ya Jumamosi, na kuna uwezekano mkubwa mabadiliko haya yakasababissha mvutano na vyama vya upinzani.
Maafisa wa serikali ya Rais Goodluck Jonathan kwa wiki kadhaa sasa wamekuwa wakiitaka tume kubadilisha siku ya uchaguzi, huku wakisema tume haipo tayari kusimamia uchaguzi na ni tofauti na ahadi zake  kuwa uchaguzi huo utaandika historia ya demokrasia katika Afrika.
 “Walio wengi wamechukizwa na kukasirishwa” haya yalisemwa na Attahiru Jega  mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi wakati akiongea na vyombo vya habari siku ya jumamosi. “ Ninataka niwahakikishie Wanigeria  kuwa hamna anayetulazimisha kufanya uamuzi huu, uamuzi huu ni mzito”.
Tume imesema katika uchaguzi huu majimbo manne ya kaskazini mashariki hayatafanya uchaguzi kwani ni maeneo yaliyoathirika zaidi na maasi ya Boko Haram.
Kwa historia uchaguzi wa Nigeria unakuwa na machafuko, na tayari kuna watu wameshapoteza maisha yao katika harakati hizo za uchaguzi. Watu 800 waliuwawa mwaka 2011 huko kaskazini kwenye idadi kubwa ya waislamu wakati wa uchaguzi mkuu kati ya Jonathan na Muhammadu Buhari.
Uchaguzi huu utawapambanisha tena Jonatahn na Buhari. Wapambe wote wa wawili hawa tayari wameshaanza kutishia kuwa fujo zitatokea endapo mgombea wao hatashinda uchaguzi huo.
Chama cha Jonathan kimeshatoa maoni yake juu ya usitishaji huo kwa kuilaumu tume.
Muungano wa vyama unaomuunga mkono Buhari inasemekana wamefanya mkutano ili kujadili madhara ya mabadiliko haya “hiki ni kipingamizi kikubwa sana kwa demokrasia ya Nigeria” muungano  huo umewataka wanigeria kuwa watulivu na kujizuia na fujo.
Usitishaji huu umekuja kutokana na hofu ya operesheni kubwa inayofanywa na  majeshi ya Nigeria na Chad dhidi ya BH kwa kutumia wanajeshi wa ardhini na ndege za kivita. Operesheni hii iliyoanza siku 10 zilizopita imeweza kuwaaondoa baadhi ya wanamgambo hao kutoka kwenye vijiji mbalimbali.
Maofisa wa Umoja wa Afrika wamemaliza mkutano wa siku tatu huko Yaounde, Cameroon wakipanga mkakati jinsi ya kupeleka wanajeshi 8,750 huko Nigeria kutoka nchi jirani za za Benin, Cameroon, Niger na  Chad ili kuweza kuwakabili BH.
Mikakati hii imewafanya wanamgambo hao kujibu kwa kufanya mashambulizi  kwenye mji mmoja huko Cameroon na kwenye miji miwili huko Niger. Taarifa zinasema watu takribani 100 wameuwawa na 500 wamejeruhiwa huko Cameroon. Huko Niger wanamgambo 100 na mwananchi mmoja wameuwawa kwenye shambulizi lililofanyika siku ya Ijumaa. Idadi kadhaa ya wanajeshi wa serikali kutoka nchi zote pia waliuwawa.
Wanamgambo wa Boko wamefanya mashambulizi matatu katika kipindi cha wiki moja huko Maiduguri, mji unaoongoza kwa ukubwa huko kaskazini mwa Nigeria ambako maelfu ya watu waliukimbia siku ya Jumamosi huku wakijazana kwenye mabasi, malori na magari madogo wakiwa na mizigo yao kadiri walivyoweza kubeba.
Kujali kwa  swala hili kimataifa kumeongezeka, kwani kwa mwaka jana tu watu 10,000 wameuwawa , idadi hii ni kubwa ukifananisha na watu 2,000 waliopoteza maisha kwa kipindi cha miaka minne kabla ya mwaka jana, takwimu hizi ni kwa mujibu wa Halmashauri ya Mahusiano ya Kimataifa ya Marekani.
Marekani imeiomba Nigeria kuendelea na uchaguzi kama ilivyopangwa awali, haya yalisemwa na John Kerry alipotembelea Nigeria wiki mbili zilizopita. “moja ya njia mzuri kuendelea kupambana na BH ni kufanya uchaguzi halali na wenye amani katika muda muafaka” alisema.
Uchaguzi wa mwaka 2011 ulihairishwa pia na ukafanyika mwezi wa nne.
Uhairishani wa uchaguzi utaipa tume ya uchaguzi muda wa kusambaza karatasi za kupigia kuraa. Mpaka siku ya Ijumaa karatasi za kupigia kura milioni 45.8 tu zilishakuwa tayari kati ya milioni 68.8. Nigeria haina ofisi za posta zinazofanya kazi pamoja na kuwa nchi yenye uchumi mkubwa  katika Afrika.
Chama cha Rais Jonathan (PDP) kimekuwa kikishinda uchaguzi mkuu tangu mwisho wa utawala wa kijeshi ulioisha mwaka 1999. Hata hivyo kushindwa kwa Jeshi la Nigeria kuzima mashambulizi ya Boko Haram kwa miaka 5, ukuaji wa rushwa na uzorotaji wa uchumi wa Nigeria umemuweka Rais kwenye nafasi tete kwenye nchi hii inayozalisha mafuta kwa wingi katika Afrika na yenye watu wengi zaidi wanaofikia milioni 170.
Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika utawapambanisha Rais Jonathan na Muhammadu Buhari. Buhari mwenye umri wa miaka 73 kutoka chama cha CPC, ni mmoja wapo wa wagombea wenye nguvu atakayegombea kupitia muunganiko wa vyama unaoitwa ACN (Action Congress of Nigeria) umoja ulioundwa Februali 2013 ili kupambana na chama tawala cha PDP, unaoundwa na vyama vinne vya upinzani, hii ni mara ya kwanza kwa upinzani kuunda umoja.
Buhari ni Meja Generali mstaafu aliyepata kuwa Rais wa Nigeria kwa takribani miaka miwili baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi. Aliwahi pia kushiriki uchaguzi mkuu mwaka 2003, 2007 na mwaka 2011 alikuwa wa pili baada ya Jonathan kwa kupata kura 12,214,853 huku Jonathan akiongoza kwa kura 22,495,187.
Goodluck Ebele Azikiwe Jonathan (58) amekuwa Rais tangu Mei 2010 kufuatia  ya kifo cha Rais Umaru Yar’Adua. Mwaka 2011 aliingia tena kwenye nafasi hiyo baada ya uchaguzi mkuu. Rais Jonathan ana shahada ya sayansi ya Wanyama na Shahada ya Uzamili ya elimu ya viumbe wa majini na samaki, na inasemekana hakuweza ,kumaliza shahada ya Uzamivu. Kabla ya Siasa Jonathan alijikita kwenye ufundishaji, ukaguzi wa elimu na kama ofisa wa utunzaji wa mazingira.
Huu ni uchaguzi wa tano kwa Nigeria tangu imalize mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 1999, uchaguzi wa mwaka huu ulipaswa kufanyika Februari 14, 2015, na umeahirishwa kwa wiki sita mpaka Machi 28, 2015.

Tunawasubiri waliochota kutoka Stanbic

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisoma ripoti yake kamati yake kuhusu kashfa ya Escrow
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisoma ripoti yake kamati yake kuhusu kashfa ya Escrow

Tunawasubiri waliochota kutoka Stanbic

MJADALA juu ya ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 321 bilioni, kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT), ungali mbichi.
Aliyetegemewa kufunga mjadala huu, kwa kushughulikia wezi halisi wa fedha hizo, ameishia kutetea uhalifu, kuhalalisha wizi, kubeba watuhumiwa na kupotosha umma juu ya waliohusika na kilichotendeka.
Akihutubia taifa juzi Jumatatu kupitia kilichoitwa, “mkutano wa rais na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam,” Rais Dk. Jakaya Kikwete, alikiri kuwapo udanganyifu katika kufikia utoaji wa fedha hizo.
Alikiri baadhi ya nyaraka kughushiwa. Akakiri kuwa kampuni ya Pan African Power Solution (PAP), imekwepa kodi ya serikali baada ya kulipwa fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow.
Akajitetea kuwa serikali inaitafuta kampuni ya MECHMAR iliyodaiwa kuuza asimimia 70 ya hisa zake katika kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa PAP ili iweze kulipa kodi hiyo.
Kampuni ya IPTL ni muungano wa kampuni mbili – VIP ya Rugemalira iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa na MECHMAR ya Malaysia iliyokuwa na asilimia 70 za hisa.
Rais alikiri kuwa aliyepewa fedha na serikali – PAP –hakuwa na sifa za kuvuna alichopata. Akakiri kuwa mmoja wa wanahisa wa IPTL, James Rugemalira, alicholipwa kilikuwa halali kwa mujibu wa sheria.
Akakiri fedha zake zililipiwa kodi ya serikali, tena kama ilivyoainishwa na mahakama.
Rais alikiri kuwa serikali yake haikufanya uchunguzi yakinifu, kuhusu historia, uhalali, sifa na uwezo wa kampuni ya PAP, katika uwekezaji wa umeme, ununuzi wa mitambo na mtaji.
Hata hivyo, pamoja na kukiri yote hayo hadharani, alishindwa kuchukua hatua dhidi ya wazembe na waliovunjaji sheria walioko serikalini.
Rais aliishia kumfuta kazi, Prof. Anna Tibaijuka, waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye kwa namna yoyote ile, hakuhusika na wizi uliotokea.
Haikutarajiwa kiongozi mkuu wa nchi kama hii, ambaye ana mamlaka makubwa ya kidola – awezaye kuvunja Bunge, kumtia mtu kizuizini, kuridhia mtu kunyongwa na kutangaza nchi kuingia vitani – kutishwa na wasiokuwa na dola.
Kitendo cha rais kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wizi huu, kimethibitisha madai ya wananchi, baadhi ya vyama vya siasa makini vya upinzani na taasisi za kiraia (NG’OS), kuwa rais “amekusudia kutenda uhalifu kwa kulinda wezi.”
Kuhusu kitendo cha ukwepaji kodi kilichofanywa na PAP, rais alikiri kuwa mamlaka ya mapato (TRA), walidai kodi kwa barua kwenda BoT.
Bali, kama PAP aliambiwa asilimlipe Rugemalira mpaka atakapolipa kodi, kwa nini hakuambiwa asimlipe MECHMAR mpaka atakapolipa kodi?Rais Kikwete amesema, Prof. Tibaijuka amepokea fedha kutoka kwa Rugamalira. Amethibitisha kuwa fedha hizo zilikuwa mchango kwa ajili ya shule ya Johanssen ya jijini Dar es Salaam.
Rais hakusema Prof. Tibaijuka hana shule. Hakusema fedha hazipelekwa shule. Hakusema fedha zilikuwa chafu. Amekiri fedha za Rugemalira zililipiwa kodi; Katibu Mkuu Kiongozi wa zamani, Balozi Paulo Rupia, amethibitisha kupokelewa kwa fedha hizo katika shule ambayo yeye ni mlezi wake.
Rais Kikwete amesema, mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow yalilipwa kwa PAP baada ya Mahakama Kuu kutoa “amri” tarehe 5 Septemba 2013. Hii siyo kweli.
Hakuna amri ya mahakama inayoelekeza fedha kutolewa. Kinachoitwa amri ya mahakama, kilikuwa ni kumaliza ugomvi wa wanahisa wa IPTL. Siyo mgogoro wa Escrow uliotokana na tozo halali ya uwekezaji na mtaji katika uwekezaji. Hiyo ndiyo amri ya mahakama.
Hakujawahi kutolewa amri nyingine yoyote ya kuruhusu fedha kutolewa katika Akaunti ya Escrow kulipwa PAP au IPTL. Wala mahakama haikuamuru kutolewa fedha hizo na serikali kama “mali iliyotekwa kwenye vita.”
Mahakama haikusema serikali ilipe fedha kutoka Akaunti ya Escrow, bila kujiridhisha na uhalali wa ununuzi wa hisa za kampuni ya IPTL, kwenda kwa PAP.
Haikuzuia serikali kuhoji kufanyika kwa malipo hayo, wakati bado kuna mgogoro kati ya serikali na Benki ya Standard Chartered (SCB) Hong Kong (BSC –HK).
Mahakama haikuagiza, wala haijaagiza serikali kutohoji, kwa nini malipo hayo yafanyike, wakati benki ya Standand Chartered, bado inaendelea kung’ang’ana mahakamani.
Benki inadai kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow, zinastahili kuwa zake. Mpaka sasa, benki hii bado inaendelea kuhangaika mahakamani kudai haki yake.
Aidha, rais anajua kuwa mahakama haikuamuru fedha hizo kutolewa kwa PAP kwa kuwa hilo halikuwa miongoni mwa hoja zilizokuwa kwenye meza mahakamani.
Hata yeye amekiri katika hotuba yake pale aliposema, “…serikali haikuona umuhimu wa kurudi mahakamani kufanya marejeo juu ya uamuzi iliotoa.”
Hakuna shaka kama mahakama ingeelezwa vizuri kuhusu kuwapo kwa mgogoro kati ya IPTL na benki ya Standard Chartered na Tanesco na benki hiyo, isingeruhusu PAP kununua hisa za IPTL.
Amri ya mahakama iliyopo na ambayo rais amekwepa kuzungumzia, ni ile ya 17 Januari 2014.
Katika amri hii, mahakama iliamuru kampuni ya PAP kuilipa VIP Engineering Limited. Hii ni baada ya Rugemalira kushitaki karibu serikali yote mahakamani.
Rugemalira aliiambia mahakama katika hati yake ya kiapo kuwa yote yaliyofanyika, ikiwamo kutolewa kwa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, ulikuwa ni “utapeli mtupu.”
Alisema, utapeli huu ulifanywa na serikali ya rais Kikwete, BoT, Benki ya Stanbic na PAP.
Kutokana na uzito wa madai ya Rugemalira, PAP na serikali zilinywea. Zikakubali kuingia katika usuluhishi wa mahakama.
Habari zinasema, suluhisho hilo halikuwafurahisha baadhi ya watu ndani ya serikali. Zikaandaliwa kampeni chafu dhidi ya Rugemalira na kampuni yake. Akaitwa mwizi.
Kazi ya kusakama wote waliopewa fedha na Rugemalira ikafanyika nchi mzima. Waliopewa mgawo, wakageuzwa wezi. Walioshiriki katika wizi, waliokwapua mabilioni ya shilingi kutoka benki ya Stanbic na waliobeba fedha kwa magunia, mifuko ya plasitiki na vikapu, wakatakatishwa.
Rais Kikwete amerejea kauli ya serikali yake bungeni, mwezi uliopita, kwamba fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow hazikuwa mali ya serikali. Amedai kuwa zilikuwa mali ya IPTL.
Amesema, ziliwekwa kwenye Akaunti ya Escrow na Tanesco badala ya kulipwa moja kwa moja kwa kampuni IPTL, kutokana na kuibuka mgogoro wa tarifu na malipo ya gharama za kuweka mtambo – Capacity Charge. Hili nalo siyo kweli. Sababu ni mbili.
Kwanza, fedha hii zilizokuwa zikisubiri kumalizika mgogoro kati ya Tanesco na IPTL, haziwezi kuwa mali ya IPTL, kabla ya mgogoro kumalizika.
Katika hotuba yake hiyo, rais amekiri kuwa mpaka fedha zinatolewa, mgogoro huo ulikuwa haujamalizika. Tanesco bado inaendelea kudhulumiwa kwa kutozwa kiwango kikubwa cha malipo ya Capacity Charge.
Hakika, hotuba ya Rais Kikwete haina jipya. Imeishia kuchochea mgogoro na kuibua yale ambayo hayakufahamika.
Mathalani, Rais Kikwete amesema azimio la Bunge lililotaka serikali kutaifisha mitambo ya IPTL, halitekelezeki. Amedai kulitekeleza azimio hilo, kutasababisha kukimbiza wawekezaji nchini.
Lakini imefahamika kuwa yule ambaye rais na serikali wanaita “muwekezaji mpya katika IPTL,” hana sifa ya kuitwa mwekezaji. Huyu aweza kuitwa, “mchuuzi.”
Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza Harbinder Singh Sethi, alighushi nyaraka. Siyo mwadilifu. Ni laghai na mdanganyifu.
Harbinder Singh amelipwa fedha asizostahili. Hadi anamaliza kuchota mabilioni hayo ya shilingi na akaunti ya Escrow inaamuriwa kufungwa, alikuwa hajanunua asilimia 30 ya hisa za VIP Engineering katika IPTL.
Wakati analipwa fedha hizo alikuwa hajawa mmiliki halali wa hisa katika MECHMAR.
Hii maana yake ni kwamba, wakati PAP inachotewa mabilioni ya shilingi kutoka Akaunti ya Escrow, hakuwa mmiliki halali wa IPTL.
Hadi fedha zinatolewa, alikuwa hajasajili asilimia 70 ya hisa alizodai amenunua kutoka kampuni hiyo ya Malaysia kwa Wakala wa Serikali na Kampuni (BRELA).
Kwa hali hiyo, uamuzi wa serikali wa kutaifisha mitambo ya IPTL, hauwezi kufukuza wawekezaji nchini.
Badala yake, kitendo hicho kitaongeza wawekezaji, kitarejesha heshima ya nchi na kingerudisha matumaini mapya kwa wananchi kwa serikali na chama kilichoko Ikulu.
Lakini kitendo cha kulea wezi na matapeli wengine wanaokuja kwa kofia ya “uwekezaji,” kitalifanya taifa hili kuendelea kudharauliwa.
Kuhusu azimio la Bunge lilitoka mamlaka ya uteuzi kuchukua hatua dhidi ya Katibu Mkuu wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Rais Kikwete amesema suala hilo ameliacha kwa mamlaka ya nidhamu.
Mamlaka ya nidhamu ambayo rais amesema amekabidhi jukumu hilo, ni Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue.
Lakini uteuzi wa makatibu wakuu, haufanywi na katibu mkuu kiongozi. Unafanywa na rais. Kitendo cha rais kulikabidhi suala la Maswi kwa katibu mkuu kiongozi, ni kukwepa wajibu wake.
Naye Prof. Sospeter Muhongo, aliyetuhumiwa na Bunge kuwa dalali wa kufanikisha wizi huo, rais amedai, uchunguzi bado unaendelea. Ameeleza anayefanya kazi ya uchunguzi dhidi ya Prof. Muhongo, yuko nje ya nchi kikazi.
Ni muhimu Rais Kikwete akafahamu kuwa hakuna sabuni ambayo itaweza kumsafisha Prof. Muhongo katika tuhuma hizi.
Jitihada zozote za kumtetea zitaishia kudhoofisha serikali na rais binafsi.
Si hivyo tu. Sakata la wizi katika akaunti ya Escrow haliwezi kumalizika bila rais kueleza hatua ambazo zitachukuliwa dhidi ya maofisa wa ikulu “waliopata mgawo” kutoka kwa Rugemalira.
Sababu zilezile na makosa yaleyale ambayo rais amemtwisha Prof. Tibaijuka, anapaswa kuwatwisha pia maofisa wake wa ikulu waliolipwa na Rugemalira.
Wala sakata hili haliwezi kufungwa bila kutaja majina ya waliopokea kitita cha kati ya Sh. 800 milioni na Sh. 5 bilioni, kutoka benki ya Stanbic.
Yawezekana wakafichwa leo. Lakini hakuna mwenye ubavu wa kuficha milele na milele.
Ikiwa mkataba wa IPTL uliofungwa miaka 20 iliyopita, wakati Rais Kikwete akiwa waziri wa nishati na baadaye waziri wa fedha – bado unamtafuna mpaka sasa – hakuna awezaye kuzuai kufahamika kwa waliochota fedha Stanbic.

Ya Jenerali Ulimwengu, Dk. Slaa, na watawala wetu!

Ya Jenerali Ulimwengu, Dk. Slaa, na watawala wetu!


KWA muda sasa, Jenerali Ulimwengu amekuwa akituletea makala maridhawa katika Raia Mwema kuhusu demokrasia na uongozi (sio utawala) bora, na tumejifunza mengi.
Kwa bahati mbaya sana(?) mafunzo yake katika makala hizo yamekuwa katika kiwango ambacho Watanzania wengi tu wanaweza kuona kama ni nadharia isiyotekelezeka. Wakati mwingine nashawishika kukbaliana nao.
Kwanza kwa sababu yeye si mgeni katika uongozi wa Kiafrika. Kuna wakati yeye Jenerali alikuwa Mkuu wa Wilaya na kwa msingi huo, ‘mteule wa Magogoni’. Naamini anajua vyema utawala wetu ulivyo.
Lakini pili, Jenerali huyu aliwahi kuwemo katika Group of 55 au kundi la wabunge fulani waliopendekeza kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Kwamba kina Jenerali na wenzake wa G55 walibadili msimamo baadaye halikuwa jambo la ajabu kwa Waafrika! Hata sasa wapo wanaharakati wanaosimamia misimamo mikali na yenye mantiki lakini wanapokumbana na vikwazo hubadilika ghafla.
Katika makala zake za hivi karibuni ambazo kwa hakika zinasisimua kusoma, Jenerali amependekeza ajira za Wakurugenzi ziwe zikitangazwa na wapendao waombe, wasailiwe na wakishinda waajiriwe.
Hoja yake ni kwamba hawa watawajibika zaidi kutokana na mikataba yao ya ajira. Kwa bahati mbaya, alisahau kueleza ikiwa watakaowasaili ni ‘malaika’ fulani, wafadhili toka nje, viongozi wa dini au ni hawa hawa watawala na viongozi wetu tunaowafahamu.
Jenerali pia hakutueleza hawa Wakurugenzi walioajiriwa kwa kusailiwa  watawajibika vipi na kwa akina nani (kwa Watanzania au wafadhili)? Kama sikukosea, kuna mahali alipata kuandika kuwa mfumo uliooza huzaa uozo.
Ni kwa msingi huo natofautiana na Jenerali kwamba hata Wakurugenzi hao wawe ni wa kuajiriwa baada ya kusailiwa, matunda tarajiwa ni yale yale kwa sababu mfumo ni ule ule na watawala ni wale wale.  Kwa ufupi, wasailiwe, wateuliwe, hakuna tofauti.
Kuhusu wakuu wa wilaya na mikoa, Jenerali  alipendekeza wachaguliwe na wananchi ili pia wawajibike kwa wananchi. Alisema kuwa kwa sasa
vigezo vya uteuzi wa viongozi mbalimbali nchini vinategemea kilichoko kichwani mwa ‘mpangaji wa Ikulu’ (Rais).
Kwamba ndiyo sababu unaweza kukuta Mkuu wa Wilaya akawa Jenerali wakati Mkuu wa Mkoa akiwa Koplo, Mkuu wa Wilaya akawa na elimu ya udaktari wa falsafa wakati Mkuu wa Mkoa hajui kusoma na kuandika…nk, ili mradi hakuna vigezo vinavyoeleweka katika suala zima la kupata viongozi hapa nchini.
Jenerali anasahau kuwa mazingira yetu hayajafikia kiwango ambacho mwananchi atamchagua kiongozi kutokana na uwezo wake badala ya pilau na pesa zake!
Nimfahamishe Jenerali tu kwamba iko Halmashauri moja mkoani Arusha ambako madiwani, mbunge, mkurugenzi na mkuu wa wilaya – achilia mbali wakuu wa idara, ni wa kabila moja!
Kuhusu suala la kuongeza majimbo, nionavyo mimi ni ubadhirifu usio wa lazima – ni kutafutiana kula na kuifilisi nchi. Hebu fuatilia takwimu zinazotolewa na serikali kuhusu makusanyo ya kodi kwa mwezi (siku hizi hazitangazwi tangazwi tena!) na piga mahesabu mwenyewe.
Majimbo ya ubunge kuongezwa, wabunge wanawake kuongezwa kufikia asilimia hamsini na kuongezewa mishahara kufikia Sh. milioni 12 na kiinua mgongo Sh. milioni 46 (na hawa sasa watafikia 400 na kuzidi), wilaya kuongezwa na mishahara yote kuongezwa.
Na juu ya haya, ongeza mishahara ya viongozi mbalimbali wa serikali, gharama za kuwatunza (magari yao, watumishi wao, safari zao zisizoisha ndani na nje, ukarabati na kodi za nyumba…nk) halafu linganisha na makusanyo ya kodi kisha ujiulize ikiwa Rais anapozunguka duniani kila mara akiwa na kopo lake la kuombea misaada (mikopo?) atakuwa anajituma kuhudumia Watanzania au anaogopa fedheha!
Ni wazi kuwa makusanyo yote ya kodi hayawezi kulipia mahitaji ya uendeshaji wa serikali hii isiyoshiba fedha. Na ikiwa fedha za kodi ni kwa ajili ya wakubwa kugawana, za maendeleo zitatoka wapi!?
Halafu waandishi wa habari wanashangaa ni vipi Maisha Bora Kwa Kila Mtanzania yamekuwa kiini macho!
Vipaumbele vyetu vimepinda. Katika nchi ambayo wananchi wake wanatafuta maisha bora kwa njia za ushirikina, viongozi wanafanya maamuzi wakilenga kusifiwa na Wazungu.
Hapa nchini mwetu, haya mambo wanayoyaita demokrasia hayana uhusiano wowote na neno lenyewe! Kule Zanzibar mbunge huwakilisha jimbo lenye wakazi wasiozidi 10,000. Na karibu kila jimbo huwakilishwa na wabunge wawili – mmoja wa Muungano na mwingine wa Baraza la Wawakilishi na wote hudai mishahara na makandokando mengine kwa kisingizio cha kuwafikia wapiga kura wao kwa urahisi zaidi.
Ikiwa kuyagawa maeneo ili kuongeza wabunge ndio kuongeza demokrasia, basi sote ‘tukajifunze’ demokrasia toka Visiwani .
Katika suala hilo hilo la fedha, nakumbuka alijitokeza Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa fulani akasema malipo na marupurupu walipwayo wabunge ni kufuru kwa Watanzania masikini! Wabunge wenzake na watawala wakakasirika. Wakataka asulubiwe.
Na hili halikubagua vyama.
Kwa hilo la mshahara na marupuupu ya wabunge,wote walijitenga naye. Hilo Iikaonyesha, kwa mara nyingine,  ni jinsi gani ubinafsi ulivyotamalaki katika uongozi Tanzania – kwamba fedha ni sabuni ya roho – kwa mlalahoi na mbunge pia.
Wakati haya yakijitokeza, wafanyakazi wengi pamoja na wazee wastaafu wanaodai haki zao wamekuwa wakikumbana na ‘mkono wa chuma’ wa Serikali – hawalipwi, wanatakiwa waendelee kuzungumza na serikali yao – bila kikomo.
Nimpongeze Dk. Slaa; maana haishi kupiga kelele kuhusu matumizi mabaya mbalimbali ya kodi na kupambana na sera za kibadhirifu, ufisadi na kukosoa matendo yote yanayoleta mapunjo kwa wananchi.
Mtu huyu (Dk. Slaa) amesababisha wananchi kufumbuka macho na kuiona Serikali yao ikifanya maamuzi ya makusudi yanayowaletea wananchi maumivu mbalimbali ya kimaisha.
Bila kutetereka huyu ndugu ameendelea kuwasha moto unaosababisha viongozi mbalimbali kuungua kinyume kabisa na mategemeo yao. Sasa je, si kweli kuwa wote wanaoguswa na mambo ya Dk. Slaa bungeni watakuwa na wanachopenda kumfanyizia?
Kwa bahati mbaya kwao, kila wanalolifanya, ikiwa ni pamoja na kutumia fedha nyingi kujaribu kumdhibiti, linashindikana.  Sasa kumbadilisha inashindikana, kumfunga haiwezekani, kumwua haiwezekani na kumwondoa inabidi kutumia fedha nyingi za kodi za wananchi, kitu ambacho pia, kimeshindikana.
Anaowawakilisha wanampenda na chama tawala CCM kinajutia kilichotokea hadi akakihama.
Kwa upande wake familia na wanaomzunguka wanahofia maisha yake. Mwenyewe anajua kuwa amejiongezea maadui na anajua pia jinsi kazi aliyoianza ilivyo ngumu na kwamba, kwa sasa, hawezi kurudi nyuma tena – atakuwa jiwe la chumvi.
Anajua kuwa amejipambanua na viongozi wengi wa Kiafrika wakati akiwa anaishi kati yao. Ndani ya haya yote,  kuna chuki, wivu na balaa nyingine zinazomkabili – haya ni matatizo makuu kichwani mwake .
Kwa Jenerali Ulimwengu nihitimishe kwa kumwambia kuwa aliyoyaandika na kupendekeza, wasomi wenzake (pamoja na viongozi nchini) wanayafahamu fika. Lakini pia, kama ilivyo katika mapendekezo yanayohusu kubadili katiba, ni masuala yasiyowezekana katika kizazi hiki cha uongozi wa CCM.
Kila kitu kinakwenda hovyo.Vyuo Vikuu vimezalisha wanasheria wasiojua sheria za mikataba zina maana gani kiasi cha kuliuza taifa, wanaohujumu taifa wanajulikana kwa vyeo na majina. Nchi inafilisiwa na viongozi hawajali. Ni harakati za kujenga tabaka la kati.
Tutaendelea kuonekana majuha hapa Tanzania na hata nje, na wale wanaojidai kutusifu kuhusu demokrasia yetu wataendelea kutuona hamnazo (sijui kama viongozi wetu hawalioni hili!).
Watawala wamekalia kasha la dhahabu, kopo mkononi wakiomba misaada kwa wafadhili wa nje (rejea Johnson Mbwambo, Raia Mwema Na. 127), ambayo pia hata wanapoipewa ‘wanailewea’. Haileti maendeleo wala nini.
Narudia tena na tena, wananchi pigieni mahesabu kodi zenu na matumizi ya serikali yenu; halafu amueni wenyewe.
Tumieni kura zenu vyema. Wababaishaji tunawafahamu, wahujumu uchumi tunawafahamu, wasiochangia, watoro na wanaolala bungeni tunawafahamu.  Tuwaweke pembeni mwaka huu – ili watakaochaguliwa wajue kuwa wametumwa kuleta Maisha Bora kikwelikweli

Hivi ndivyo bangi inavyoingizwa katika magereza

Hivi ndivyo bangi inavyoingizwa katika magereza

BANGI ni dawa ya kulevya iliyopo kwenye kundi la dawa za kulevya lenye kuleta Njozi (Hellucinogences).
Vileta njozi huathiri ubongo na kumfanya mtumiaji kutoa tafsiri potofu ya hisia na kujisikia kama vile yuko nje ya dunia.
Mtumiaji wa bangi huzalishwa na kutumiwa kwa wingi barani Afrika kwa sababu hustawi maeneo mengi.
Nchini Tanzania kanda ya nyanda za juu kusini, mkoani Njombe wilayani Makete hustawi zaidi.
Wakati Serikali ikiamini kuwa gerezani ni mahala salama hata kuwatunza wanaokamatwa na dawa za kulevya, hali si shwari katika baadhi ya magereza hapa nchini, kutokana na ongezeko la matumizi ya dawa hizo.
Baadhi ya askari Magereza, wafungwa na mahabusu katika magereza mbalimbali hapa nchini, wanahusishwa na biashara ya dawa za kulevya ndani ya magereza, imebainika.
Uchunguzi uliofanywa kwa miezi miwili sasa, umebaini kuwepo kwa dawa za kulevya katika magereza mengi hapa nchini, hususani Bangi.
Baadhi ya askari ambao hawakutaka kutajwa majina yao na vyeo katika Gereza la Ruanda na Songwe mkoani Mbeya, walithibitisha kuwepo kwa uingizwaji wa bidhaa hiyo ambayo inafanyika kwa siri kubwa katika magereza hayo.
Biashara hiyo inahusisha baadhi ya askari, wafungwa na mahabusu wenye kesi mbalimbali, wanaokaa muda mrefu gerezani huku kesi zao zikiahirishwa mara kwa mara.
Baadhi ya waliowahi kuwa mahabusu wa gereza la Ruanda mkoani Mbeya, wanaeleza kuwa wahusika wakubwa ni baadhi ya wafungwa wanaofanya kazi nje ya gereza, kisha kurejeshwa alasiri na baadhi wanaopelekwa mahakamani kusomewa mashitaka ya kesi zinazowakabili.
Wanasema njia ambazo zinatumika kuingiza dawa hizo gerezani ni kujiingiza katika sehemu ya haja kubwa wakiwa nje ya gereza na wakati wa ukaguzi unapofanyika kwa kila anayeingia gerezani hapo, askari wanashindwa kubaini.
“Baadhi ya wafungwa ambao wanakaribia kumaliza muda wao, wanatolewa kwenda kufanya kazi za nje ikiwemo kwenda kukata nyasi za Ng’ombe na kurejeshwa mchana na wale wanaoenda kusaga mashine wanaweka kwenye unga. Hao wana mtandao na wauza bangi uraiani, wanaingia nazo na kufanya biashara ndani ya gereza, mle kuna biashara nyingi” anaeleza mmoja wa aliyekuwa mahabusu katika gereza hilo na kuachiliwa huru hivi karibuni baada ya Mahakama kuona hana hatia.
Baadhi ya askari mgambo wanaotumwa kuwachukua mahabusu na kuwapeleka katika mahakama za mwanzo, ambao nao waliomba hifadhi ya majina yao, walikiri kuwepo kwa biashara hiyo ambapo walisema kuwa, biashara hiyo inafanyika kutokana na vipato vidogo vya Mgambo na askari Magereza kutokuwa na mianya ya rushwa tofauti na askari polisi.
Mbali na bangi, wanasema kuwa, katika magereza pia kuna uvutaji mkubwa wa sigala ambazo huingizwa kwa njia za haja kubwa kisha kutolewa vyooni na kuhifadhiwa katika maeneo mbalimbali ya sero na nje ya sero bustanini.
Wakala wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali, idara ya huduma za sayansi ya makosa ya jinai (GCRLA), inataja madhara yanayowakuta watu wanaotumia dawa hii ya kulevya kuwa ni kuwaza, kuona, kusikia na kuhisi vitu kwa namna tofauti au visivyokuwepo, kupata njozi, kuongezeka kwa hamu ya kula, kuwa kama kichaa, kutapika, wasiwasi, hamaki na kupumbaa.
Madhara yatokanayo na matumizi ya muda mrefu
Madhara hayo ni kupata ugonjwa wa akili, mabadiliko ya maono, hisia na mtizamo yasiyoisha, kuharibika kwa ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kukumbuka na kufikiri na kukosa ari ya maendeleo na mabadiliko ya aina yoyote ile.
Sheria inasemaje kuhusu bangi
Kutumia, kuhamasisha matumizi, kuuza, kusafirisha, kuhifdhi au kujihusisha kwa namna yeyote ile na bangi ni kosa la jinai. Adhabu kwa makosa haya hufikia hadi kifungo cha maisha.
Sheria inasemaje kuhusu bangi
Kutumia, kuhamasisha matumizi, kuuza, kusafirisha, kuhifdhi au kujihusisha kwa namna yeyote ile na bangi ni kosa la jinai. Adhabu kwa makosa haya hufikia hadi kifungo cha maisha.
Mbali na tatizo la Bangi, moja ya matatizo yanayotajwa ni suala la kutumia kwa kubadilishana vitu vyenye ncha kali zikiwemo nyembe.
“Nilikamatwa na kupelekwa gerezani mwaka 2011, nikakuta watu wananyolea wembe mmoja ambapo kilichoniuma ni kwamba kuna rafiki yangu aitwaye Jack, alikuwa anaishi  na VVU, alinyolea wembe akajikata, akampa jamaa anaitwa Kamugisha akajikata, naye akampa Side, naye akajikata na Side alimpa Chidi akatie kucha naye akajikata, virusi vikasambaa kwa wote”anasema Frank Kaitaba, kijana ambaye alikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya Jijini Dar es Salaam na sasa anahudumiwa na shirika la Medecin De Munde la Temekelinalopunguza athari za madawa ya kulevya..
Anasema baada ya hapo akaamua kuwafuata madaktari wa gereza hilo na kuanzisha kikundi cha uelimishaji rika ndani ya gereza na kwamba tangu hapo ndani ya gereza hilo mtu anapotaka kunyoa anampa taarifa kiongozi aitwaye Onyango, ambaye anatoa wembe na kumwamuru nyapala  asimamie matumizi ya nyembe.
- http://www.jamiiforums.com/blog/riport-maalum-hivi-ndivyo-bangi-inavyoingizwa-katika-magereza/#sthash.jDeFJgHl.dpuf