Sunday, February 15, 2015

Ya Jenerali Ulimwengu, Dk. Slaa, na watawala wetu!

Ya Jenerali Ulimwengu, Dk. Slaa, na watawala wetu!


KWA muda sasa, Jenerali Ulimwengu amekuwa akituletea makala maridhawa katika Raia Mwema kuhusu demokrasia na uongozi (sio utawala) bora, na tumejifunza mengi.
Kwa bahati mbaya sana(?) mafunzo yake katika makala hizo yamekuwa katika kiwango ambacho Watanzania wengi tu wanaweza kuona kama ni nadharia isiyotekelezeka. Wakati mwingine nashawishika kukbaliana nao.
Kwanza kwa sababu yeye si mgeni katika uongozi wa Kiafrika. Kuna wakati yeye Jenerali alikuwa Mkuu wa Wilaya na kwa msingi huo, ‘mteule wa Magogoni’. Naamini anajua vyema utawala wetu ulivyo.
Lakini pili, Jenerali huyu aliwahi kuwemo katika Group of 55 au kundi la wabunge fulani waliopendekeza kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Kwamba kina Jenerali na wenzake wa G55 walibadili msimamo baadaye halikuwa jambo la ajabu kwa Waafrika! Hata sasa wapo wanaharakati wanaosimamia misimamo mikali na yenye mantiki lakini wanapokumbana na vikwazo hubadilika ghafla.
Katika makala zake za hivi karibuni ambazo kwa hakika zinasisimua kusoma, Jenerali amependekeza ajira za Wakurugenzi ziwe zikitangazwa na wapendao waombe, wasailiwe na wakishinda waajiriwe.
Hoja yake ni kwamba hawa watawajibika zaidi kutokana na mikataba yao ya ajira. Kwa bahati mbaya, alisahau kueleza ikiwa watakaowasaili ni ‘malaika’ fulani, wafadhili toka nje, viongozi wa dini au ni hawa hawa watawala na viongozi wetu tunaowafahamu.
Jenerali pia hakutueleza hawa Wakurugenzi walioajiriwa kwa kusailiwa  watawajibika vipi na kwa akina nani (kwa Watanzania au wafadhili)? Kama sikukosea, kuna mahali alipata kuandika kuwa mfumo uliooza huzaa uozo.
Ni kwa msingi huo natofautiana na Jenerali kwamba hata Wakurugenzi hao wawe ni wa kuajiriwa baada ya kusailiwa, matunda tarajiwa ni yale yale kwa sababu mfumo ni ule ule na watawala ni wale wale.  Kwa ufupi, wasailiwe, wateuliwe, hakuna tofauti.
Kuhusu wakuu wa wilaya na mikoa, Jenerali  alipendekeza wachaguliwe na wananchi ili pia wawajibike kwa wananchi. Alisema kuwa kwa sasa
vigezo vya uteuzi wa viongozi mbalimbali nchini vinategemea kilichoko kichwani mwa ‘mpangaji wa Ikulu’ (Rais).
Kwamba ndiyo sababu unaweza kukuta Mkuu wa Wilaya akawa Jenerali wakati Mkuu wa Mkoa akiwa Koplo, Mkuu wa Wilaya akawa na elimu ya udaktari wa falsafa wakati Mkuu wa Mkoa hajui kusoma na kuandika…nk, ili mradi hakuna vigezo vinavyoeleweka katika suala zima la kupata viongozi hapa nchini.
Jenerali anasahau kuwa mazingira yetu hayajafikia kiwango ambacho mwananchi atamchagua kiongozi kutokana na uwezo wake badala ya pilau na pesa zake!
Nimfahamishe Jenerali tu kwamba iko Halmashauri moja mkoani Arusha ambako madiwani, mbunge, mkurugenzi na mkuu wa wilaya – achilia mbali wakuu wa idara, ni wa kabila moja!
Kuhusu suala la kuongeza majimbo, nionavyo mimi ni ubadhirifu usio wa lazima – ni kutafutiana kula na kuifilisi nchi. Hebu fuatilia takwimu zinazotolewa na serikali kuhusu makusanyo ya kodi kwa mwezi (siku hizi hazitangazwi tangazwi tena!) na piga mahesabu mwenyewe.
Majimbo ya ubunge kuongezwa, wabunge wanawake kuongezwa kufikia asilimia hamsini na kuongezewa mishahara kufikia Sh. milioni 12 na kiinua mgongo Sh. milioni 46 (na hawa sasa watafikia 400 na kuzidi), wilaya kuongezwa na mishahara yote kuongezwa.
Na juu ya haya, ongeza mishahara ya viongozi mbalimbali wa serikali, gharama za kuwatunza (magari yao, watumishi wao, safari zao zisizoisha ndani na nje, ukarabati na kodi za nyumba…nk) halafu linganisha na makusanyo ya kodi kisha ujiulize ikiwa Rais anapozunguka duniani kila mara akiwa na kopo lake la kuombea misaada (mikopo?) atakuwa anajituma kuhudumia Watanzania au anaogopa fedheha!
Ni wazi kuwa makusanyo yote ya kodi hayawezi kulipia mahitaji ya uendeshaji wa serikali hii isiyoshiba fedha. Na ikiwa fedha za kodi ni kwa ajili ya wakubwa kugawana, za maendeleo zitatoka wapi!?
Halafu waandishi wa habari wanashangaa ni vipi Maisha Bora Kwa Kila Mtanzania yamekuwa kiini macho!
Vipaumbele vyetu vimepinda. Katika nchi ambayo wananchi wake wanatafuta maisha bora kwa njia za ushirikina, viongozi wanafanya maamuzi wakilenga kusifiwa na Wazungu.
Hapa nchini mwetu, haya mambo wanayoyaita demokrasia hayana uhusiano wowote na neno lenyewe! Kule Zanzibar mbunge huwakilisha jimbo lenye wakazi wasiozidi 10,000. Na karibu kila jimbo huwakilishwa na wabunge wawili – mmoja wa Muungano na mwingine wa Baraza la Wawakilishi na wote hudai mishahara na makandokando mengine kwa kisingizio cha kuwafikia wapiga kura wao kwa urahisi zaidi.
Ikiwa kuyagawa maeneo ili kuongeza wabunge ndio kuongeza demokrasia, basi sote ‘tukajifunze’ demokrasia toka Visiwani .
Katika suala hilo hilo la fedha, nakumbuka alijitokeza Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa fulani akasema malipo na marupurupu walipwayo wabunge ni kufuru kwa Watanzania masikini! Wabunge wenzake na watawala wakakasirika. Wakataka asulubiwe.
Na hili halikubagua vyama.
Kwa hilo la mshahara na marupuupu ya wabunge,wote walijitenga naye. Hilo Iikaonyesha, kwa mara nyingine,  ni jinsi gani ubinafsi ulivyotamalaki katika uongozi Tanzania – kwamba fedha ni sabuni ya roho – kwa mlalahoi na mbunge pia.
Wakati haya yakijitokeza, wafanyakazi wengi pamoja na wazee wastaafu wanaodai haki zao wamekuwa wakikumbana na ‘mkono wa chuma’ wa Serikali – hawalipwi, wanatakiwa waendelee kuzungumza na serikali yao – bila kikomo.
Nimpongeze Dk. Slaa; maana haishi kupiga kelele kuhusu matumizi mabaya mbalimbali ya kodi na kupambana na sera za kibadhirifu, ufisadi na kukosoa matendo yote yanayoleta mapunjo kwa wananchi.
Mtu huyu (Dk. Slaa) amesababisha wananchi kufumbuka macho na kuiona Serikali yao ikifanya maamuzi ya makusudi yanayowaletea wananchi maumivu mbalimbali ya kimaisha.
Bila kutetereka huyu ndugu ameendelea kuwasha moto unaosababisha viongozi mbalimbali kuungua kinyume kabisa na mategemeo yao. Sasa je, si kweli kuwa wote wanaoguswa na mambo ya Dk. Slaa bungeni watakuwa na wanachopenda kumfanyizia?
Kwa bahati mbaya kwao, kila wanalolifanya, ikiwa ni pamoja na kutumia fedha nyingi kujaribu kumdhibiti, linashindikana.  Sasa kumbadilisha inashindikana, kumfunga haiwezekani, kumwua haiwezekani na kumwondoa inabidi kutumia fedha nyingi za kodi za wananchi, kitu ambacho pia, kimeshindikana.
Anaowawakilisha wanampenda na chama tawala CCM kinajutia kilichotokea hadi akakihama.
Kwa upande wake familia na wanaomzunguka wanahofia maisha yake. Mwenyewe anajua kuwa amejiongezea maadui na anajua pia jinsi kazi aliyoianza ilivyo ngumu na kwamba, kwa sasa, hawezi kurudi nyuma tena – atakuwa jiwe la chumvi.
Anajua kuwa amejipambanua na viongozi wengi wa Kiafrika wakati akiwa anaishi kati yao. Ndani ya haya yote,  kuna chuki, wivu na balaa nyingine zinazomkabili – haya ni matatizo makuu kichwani mwake .
Kwa Jenerali Ulimwengu nihitimishe kwa kumwambia kuwa aliyoyaandika na kupendekeza, wasomi wenzake (pamoja na viongozi nchini) wanayafahamu fika. Lakini pia, kama ilivyo katika mapendekezo yanayohusu kubadili katiba, ni masuala yasiyowezekana katika kizazi hiki cha uongozi wa CCM.
Kila kitu kinakwenda hovyo.Vyuo Vikuu vimezalisha wanasheria wasiojua sheria za mikataba zina maana gani kiasi cha kuliuza taifa, wanaohujumu taifa wanajulikana kwa vyeo na majina. Nchi inafilisiwa na viongozi hawajali. Ni harakati za kujenga tabaka la kati.
Tutaendelea kuonekana majuha hapa Tanzania na hata nje, na wale wanaojidai kutusifu kuhusu demokrasia yetu wataendelea kutuona hamnazo (sijui kama viongozi wetu hawalioni hili!).
Watawala wamekalia kasha la dhahabu, kopo mkononi wakiomba misaada kwa wafadhili wa nje (rejea Johnson Mbwambo, Raia Mwema Na. 127), ambayo pia hata wanapoipewa ‘wanailewea’. Haileti maendeleo wala nini.
Narudia tena na tena, wananchi pigieni mahesabu kodi zenu na matumizi ya serikali yenu; halafu amueni wenyewe.
Tumieni kura zenu vyema. Wababaishaji tunawafahamu, wahujumu uchumi tunawafahamu, wasiochangia, watoro na wanaolala bungeni tunawafahamu.  Tuwaweke pembeni mwaka huu – ili watakaochaguliwa wajue kuwa wametumwa kuleta Maisha Bora kikwelikweli