Vilio, vilio, vilio.
12th March 2015
B-
Kontena laangukia basi, 42 wafa papo hapo, 23 hoi, JK atuma salamu za pole.
Vilio na simanzi jana vilitawala kwenye mji wa Mafinga, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, kufuatia watu 42 kufariki dunia na wengine 23 kujeruhiwa, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupata ajali.
Ajali hiyo ilitokana na basi hilo la kampuni ya Majinje Express lenye namba za usajili T.438 CDE kugongana uso kwa uso na lori la mizigo ‘semitrela’ namba T698 APJ na kisha kontena lililokuwa kwenye lori hilo kulifunika basi lilokuwa na abiria.
Miongoni mwa waliofariki ni pamoja na dereva wa basi hilo, huku dereva wa lori akielezwa kuwa mahututi katika Hospitali ya Wilaya ya Mafinga.
Waliofariki wametajwa kuwa ni Ester Emmanuel, Lusekelo Enock, Jeremia Watson, Digna Solomon, Frank Chiwango, Luten Sanga, Teresia Kamiyage na Dotto Katuga.
Wengine ni Esta Fide, Pauline Justine, Mbamba Ipyana, Catherine Mwajengo, Zera Kasambala, Rebeka Kasambala Mr. Musa, Shadrack Msigwa, Mathias Justine, Mr. Elias na Juliana Bukuku.
Wamo pia Christina Lyimo, Martin Haulo, Dominick Mashauri, Esta Willy, Lucy Mtega, Erick Shitind, Edwaga Kamiyage, Frank Mbale, Mustafa Ramadhani, Kelvin Odubi, Mr. Osward, Omega Mwakasege, Upendo William, Iman Mchange, Charles Lesenga, Mr. Neto Sanga, Pili Vincent, Mr. Hamad, Ed Erick, Daud so Stones na Jacob Doketa.
Lori hilo linalomilikiwa na kampuni ya Cipex, lilikuwa kiliendeshwa na Baracka Gabriel, kutoka Iringa kwenda Mbeya.
Ajali ilitokea majira ya 3:30 asubuhi, eneo la Changarawe katika barabara kuu ya Iringa-Mbeya.
Basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam na lori hilo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda nchi jirani ya Zambia.
Habari kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa ajali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ubovu wa barabara na mwendo kasi wa basi hilo.
Kwa mujibu wa habari hizo, eneo ambako ajali hiyo imetokea kuna shimo kubwa.
Habari hizo zinaeleza kuwa, dereva wa lori alifanikiwa kulikwepa shimo hilo, lakini dereva wa basi alipojaribu, alishindwa kulimudu basi hilo na hivyo kutumbukia.
Baada ya kutumbukia kwenye shimo hilo, magari hayo yalijaribu kupishana na wakati yakipishana, kontena lililokuwa kwenye lori hilo lililiangukia basi na kusababisha vifo hivyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alithibitisha kutokea ajali hiyo mbaya.
Alisema ajali hiyo kama zilivyo nyingine, zimechangiwa na uchakavu wa miundombinu ya barabara.
“Ndugu zangu wanahabari, hii ni ajali kama ilivyo ajali nyingine. Kwa sababu, imetokea sehemu mbaya. Na pia uchakavu wa barabara unachangia na siyo ajali ya kujitakia,” alisema Kamanda Mungi.
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo, waliliambia NIPASHE kwamba, awali basi hilo lilikuwa katika mwendo kasi.
Kutokana na hali hiyo, walimuita kondakta wa basi hilo na kumtaka amwambie dereva apunguze mwendo, lakini hakufanya hivyo.
Kevin Hamfrey, ambaye alikuwa akitokea Mbeya kwenda jijini Dar es Saalam aliitaka serikali kuangalia upya suala la miundombinu kwani imekuwa chakavu na ndiyo iliyochangia ajali hiyo.
Musa Mwasega alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, ambao ulisababisha dereva kushindwa kulimudu gari na hivyo kusababisha kugongana uso kwa uso na lori hilo.
“Kiukweli ajali hii ni mbaya sana. Na sisi wenyewe baada ya kuona dereva anajaribu kulimudu, tulijua lazima kuna kitu kitatokea kwa sababu awali mwendo kasi ulikuwa siyo wa kawaida,” alisema Mwasega.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, Boaz Peter, alithibitisha kupokea miili ya watu 42 na majeruhi 23.
Alisema hadi sasa wanafanya jitihada ili ndugu watambue miili ya marehemu na kwenda kuichukua.
Peter alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Mufindi, wakati majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.
Alisema kati ya miili 42, 32 ilipelekwa Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuhifadhiwa kutokana na chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Mufindi kuwa finyu.
Kutokana na hali ya majeruhi wengine kuwa mbaya, wawili walichukuliwa na gari la wagonjwa ya wilaya hiyo na kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Kati ya waliofariki dunia, wanaume ni 37, wakati wanawake ni watano.
Baadhi ya wananchi wa mji mdogo wa Mafinga, ambao hawakupenda majina yao kuandikwa gazetini, walisema mara kwa mara wamekuwa wakitoa kilio chao kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na baadhi ya viongozi wa ujenzi wa barabara wilaya ya Mufindi, lakini kimekuwa hakisikilizwi.
Badala yake, wamekuwa wakijibiwa kuwa suala hilo litapelekwa kwa viongozi husika.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, aliiagiza Tanroads kuanza kushughulikia uchakavu wa barabara hiyo mara moja.
“Msiba huu ni wa watu wote, siyo wa mtu mmoja, nimesikitika sana kusikia kuwa asubuhi kuna ajali ilitokea eneo la Changarawe nje kidogo ya mji wa Mafinga na nilivyosikia nimekuja mara moja kuangalia ni jinsi gani tutafanya ili kuwasaidia ndugu hawa, ”alisema Masenza.
CHANZO: NIPASHE