Friday, January 23, 2015

Ni majanga tena Polisi

Ni majanga tena Polisi

23rd January 2015

  Wengine hoi kwa kipigo


   Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda.

Jeshi la Polisi limekubwa na dhahama nyingine baada ya  askari wake wawili wa mkoani Tabora, kupewa kipigo kwa madai ya kusababisha kifo cha kijana mmoja wa mjini humo.
 
 Tukio hilo lilitokea juzi sambamba na tukio la kuuawa kwa askari wawili wa kituo polisi cha Ikwiriri, wilayani Rufiji, Pwani.
 
 Aidha, Jeshi la Polisi limeungana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuwasaka watu waliovamia Kituo cha Polisi Ikwiriri wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani na kuwaua askari hao na kupora silaha mbalimbali zikiwamo bunduki na risasi.
 
 Katika tukio la Tabora, kijana huyo anadaiwa kufa wakati akifukuzwa na askari hao wa Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora kwa lengo la kutaka kumtia mbaroni kwa tuhuma za  kushiriki mchezo wa kamari.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, akizungumza na NIPASHE alisema tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu  saa 10.30 jioni katika mtaa wa Kadinya kata ya Ng’ambo.
 
Kamanda Kaganda aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni  PC Yohana na MW Daniel Isonda na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kitete  kutokana na kujeruhiwa kwa kipigo na wananchi.
 
Alisema wananchi walianza kuwashambulia askari hao walipotaka kuwakamata vijana watatu waliokuwa wakicheza kamari kijiweni katika eneo la Ng’ambo mjini Tabora.
 
Vijana hao baada ya kubaini wanataka kukamatwa na polisi walianza kukimbia na bahati mbaya mmoja wao alitumbukia ndani ya dimbwi la maji na kuzama.
 
Kaganda alisema kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Edwin Kefa (19), baada ya kutumbukia katika dimbwi hilo,  alishindwa kuogelea na hivyo askari waliokuwa wakimfukuza walimuokoa akiwa katika hali mbaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Kitete, lakini alifariki  wakati akipatiwa matibabu.
 
Alisema pamoja na askari hao kushambuliwa, Jeshi hilo litaendelea kufanya msako mkali ili kuvunja vijiwe vyote vya wacheza kamari, wavuta bangi na wanaotumia dawa za kulevya mkoani Tabora.
 
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa wananchi walichukua uamuzi wa kuwashambulia askari hao baada ya kuona wakimpiga  kijana aliyepoteza maisha kabla ya kufikwa na mauti.
 
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Kitete, Dk. Yusuph Bwire, alisema hali za askari hao zinaendelea vizuri na kwamba  Isonda alijeruhiwa begani na kichwani.
 
Dk. Bwire alisema Yohana alijeruhiwa kichwani na kwamba aliruhisiwa jana asubuhi  baada ya hali yake kuwa nzuri.
 
JWTZ YAJITIOSA RUFIJI
Wakati hayo yakitokea, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu waliokiteka na kukivamia kituo cha polisi Ikwiriri na kuwaua askari wawili na kuiba silaha.
 
Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, akizungumza katika mahojiano na Redio One katika kipindi cha Kumepambazuka, alisema wanashirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kuhakikisha waliofanya tukio hilo wanatiwa mbaroni.
 
Kamishna Chagonja alisema hadi kufikia jana jioni hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa na wamebaini kuwa bomu lililorushwa katika kituo hicho halikuwa moja bali yalikuwa mengi.
 
“Uvamizi ulikuwa mkubwa na inaonekana waliofanya tukio hilo  walikuwa si chini ya 15 na baada ya kufanya tukio hilo waliondoka kwa kutumia Noah,” alisema.
 
Alisema mabaki ya bomu lililorushwa yamepekwa kwa wataalam kubaini ni bomu la aina gani.
 
Juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Urich Matei, alisema tukio la kuvamiwa kituo hicho lilitokea saa 8:00 usiku.
 
Kamanda Matei alitaja askari waliouawa kuwa ni PC Judith Timoth na  Koplo Edga Mlinga ambaye ni askari wa kikosi cha usalama barabarani na kwamba miili ya askari  imehifadhiwa katika kituo cha afya Ikwiriri.
 
Alisema baada ya kukivamia kituo hicho waliiba bunduki aina ya SMG mbili, SAR mbili, Shotgun moja, risasi zaidi ya 60 na bunduki mbili za kulipulia mabomu ya machozi.
 
 Matei alisema baadaye walilipua bomu kituoni hapo ambalo liliharibu gari lenye namba PT 1965 linalotumiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kituo hicho (OCCID) kisha kutokomea kusikojulikana.
 
Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alisema jeshi hilo lina idara nyingi, hivyo taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kushirikiana katika uchunguzi wa tukio hilo zinaweza kuwa za kweli

Mwenyekiti kwa Pinda ala kipigo

Mwenyekiti kwa Pinda ala kipigo

23rd January 2015


























Uapishaji wenyeviti wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine umekumbwa na vurugu zilizosababisha aliyekuwa mgombea uenyekiti kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupewa kipigo na wananchi mbele ya askari polisi na kuchaniwa nguo zake kwa madai alitaka kuapishwa kinyemela.
 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda , ametajwa na kulalamikiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo kwa kudaiwa kutoa maagizo ya kuapishwa kada kutoka CCM katika mtaa wake bila kushinda uchaguzi.
 
 Aidha,Mwenyekiti wa mtaa wa Migombani kata ya Segerea, Japhet Kembo, hivi karibuni aliapishwa na wananchi kupitia wakili wa kujitegema baada ya uongozi wa manispaa kushindwa kumuapisha kwa wakati, jana aliapishwa rasmi na Mwanasheria wa Manispaa hiyo.
 
Mwingine aliyeapishwa ni Mwenyekiti mteule wa mtaa Minazi mirefu, Ubaya Chuma.
 
 Wakati wa zoezi hilo, Mariano Bungala ambaye aligombea mtaa wa Kigogo Fresh ‘B’ kata ya Pugu, anakoishi Waziri Mkuu, alipewa kichapo na wananchi wakiwamo wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa madai kuwa hakushinda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini kwa sababu anatoka mtaa anakoishi Pinda, hivyo ulifanyika ujanja ili aapishwe kinyemela.
 
Vurugu hizo ziliibuka katika ofisi za Manispaa ya Ilala saa saa 3:30 asubuhi muda mfupi baada ya Bungala kuitwa na maofisa wa manispaa ili kuingia ukumbini kuapishwa, lakini alipotaka kuingia tu alidakwa na wananchi na kuanza kupewa kichapo.
 
Vurugu hizo zilisababisha watumishi wa Manispaa hiyo kusitisha kwa muda kazi hiyo katika ofisi zao kushudia vurugu hizo ambazo zilizimwa baada ya polisi kumuokoa Bungala aliyekuwa akiendelea kupewa kipigo.
 
Mgombea wa Chadema katika mtaa huo, Patricia Mwamakula, ambaye alipambana na Bungala katika uchaguzi huo, alisema wakati wa uchaguzi Desemba 14, mwaka jana hakuna mshindi aliyetangazwa baada ya kutokea vurugu.
 
Alisema kutotangazwa kwa matokeo hayo kulifuatia wanachama wa CCM kuchoma masanduku baada ya kubaini kadri kura zilivyokuwa zinaendelea kuhesabiwa ushindi ulikuwa unaelekea kwa mgombea wa upinzani.
 
“Hakuna aliyeshinda kwenye uchaguzi kwenye mtaa wetu, tatizo tunakaa mtaa anaoishi Waziri Mkuu ambaye amesema kuwa hawezi akaongozwa na mwenyekiti anayetoka chama cha upinzani,” alisema.
 
Mwanachama mwingine wa Chadema, Mayama Mkwizu, alisema wananchi wa mtaa wa Kigogo Fresh “B” hawako tayari kuongozwa na mwenyekiti wa CCM ambaye hakushinda kwenye uchaguzi kwa sababu tu ya shinikizo la Waziri Mkuu.
 
“Kura zilipigwa vizuri, lakini CCM walichoma masanduku kabla ya matokeo kutangazwa, kutaka kuapishwa Bungala, ni shinikizo la Waziri Mkuu, kama wanataka kusema alishinda wa CCM walete majivu hapa yaliyotokana na kuchomwa kwa masanduku ya kura au kama Pinda anaona chama chake kimeshinda aje yeye aapishwe,” alisema.
 
Hata hivyo, Bungala akizungumza na waandishi wa habari huku akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa wamemzunguka huku mkono wa shati lake ukiwa umechanwa na kuondolewa kabisa, alisema ana uhakika alishinda uchaguzi huo.
 
KAULI YA BUNGALA
“Nilishinda kwa kupata kura 233 na matokeo yalitangazwa na Afisa Mtendaji Kata ya Pugu ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi na ndiye aliyeniambie nije niapishwe,” alisema Bungala huku akichechemea kutoka na kipigo alichokipata.
 
Bungala alisema tukio lililompata la kupigwa na ataliwasilisha kwa viongozi wake wa chama na kwamba waliomfanyia vurugu hizo ni wahuni ambao wanataka kuendesha siasa za vurugu.
 
Alipoulizwa kama kuna shinikizo kutoka kwa Waziri Mkuu na kuamua kuja kuapishwa wakati anafahamu kuna utata katika matokeo kwenye mtaa wake, alisema hizo taarifa ni za uongo. 
 
MWANASHERIA WA MANISPAA ANENA
Naye Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Mashauri Musimu, alisema licha ya mwenyekiti wa mtaa Kigogo Fresh “B’ kupigwa na kusababisha asiapishwe, lakini manispaa itahakikisha inafanya kila liwezekanalo aapishwea kwa sababu ndiye mshindi halali katika uchaguzi huo.
 
“Anayetambuliwa na Manispaa kuwa ndiye mshindi ni Mariano Bungala na kama kuna mtu hajaridhika anaruhusiwa kwenda mahakamani kudai haki,” alisema.
 
Nao wananchi na wafuasi wa Chadema walitoa thadhari kwamba kama viongozi wa Manispaa watamuapisha mgombea wa CCM na wao watamuapisha  wa Chadema ili mtaa huo uwe na wenyeviti wawili kutoka vyama tofauti.
 
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Kigogo Fresh  ‘B’ kata ya Pugu ambayo NIPASHE ilionyeshwa na  maofisa wa Manispaa ya Ilala yanaonyesha kuwa katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM alipata kura 134, Chadema 127, CUF 17 na mgombea wa NCCR-Mageuzi alipata kura tisa.
 
OFISI YA WAZIRI MKUU
Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Waziri Mkuu, Irene Bwire, alipoulizwa kuhusu madai dhidi ya Waziri Mkuu, hakutaka kueleza zaidi ya kusema kuwa ofisi ya Tamisemi ndiyo inayosimamia masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa hivyo ndiyo inayoweza kutoa jibu kuhusu utata wa matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Kigogo Fresh ‘B’.
 
“Uchaguzi wa serikali za mitaa unasimamiwa na Tamisemi, wasiliana na Katibu Mkuu wa Tamisemi au Waziri watakupa majibu, kwanza mimi sipo ofisini tangu jana,” alisema Irene.
 
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia alipotafuta simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
 
MGOMBEA CCM  SEGEREA  ALALAMIKA
Wakati huo huo;  aliyekuwa  mgombea wa serikali ya mtaa wa Migombani Jimbo la Segerea kupitia CCM, Uyeka Idd, amemtupia lawama Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, kwa kupingana na tangazo lake la kuahirisha uchaguzi.
 
Tangazo hilo la kuahirisha uchaguzi ambao ulitakiwa kufanyika Desemba 14, mwaka jana  lilitaka uahirishwe kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza katika kituo hicho zikiwamo vurugu.
 
Alisema Desemba 16, tangazo lilitoka kwa Mkurugenzi kuwa uchaguzi uairishwe, lakini jana walishangazwa na kitendo cha kuapishwa kwa mgombea wa Chadema kuwa ndiye mshindi wa mtaa huo.
 
“Tangazo lilisema marudio ya uchaguzi ni Desemba 21, uchaguzi ulifanyika, lakini ulifanyika ndani ya dosari za awali na kukwamisha baadhi ya wananchi kupiga kura, ” alisema Idd alipozungumza na waandishi wa habari.
 
Januari 20, mwaka huu, wananchi walimwapisha Japhet Kembo wa Chadema kuwa ndiye mshindi wa mtaa huo  baada ya ukimya wa serikali kitomwapisha.
 
Aliongeza kuwa madai ya shinikizo toka kwa wananchi kuapishwa kwa kiongozi huyo hayana tija kwani cha msingi ni uchaguzi kufanyika na ushindi upatikane kwa haki.
 
“Madai ya wananchi kwamba kuna shinikizo la Mbunge wa Segerea,  Dk. Makongoro Mahanga, kuhusu ushindi wa CCM katika Mtaa huo sio kweli kwani mbunge (Mahanga) anakaa mtaa tofauti na huo,” alisema Idd. Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Christina Mwakangale na Adela Josephat