Wanasiasa wanaotajwa kuwa katika wakati mgumu wa kukubwa na kimbunga cha Escrow ni baadhi ya wabunge na mawaziri walioonekana waziwazi ndani ya Bunge kuunga mkono na kutetea uchotwaji huo haramu.
Duru za siasa zinaeleza kuwa tayari utaratibu wa kuwatambua wabunge wote waliounga mkono uchotaji huo imeanza miongoni mwa wanasiasa wenyewe.
Jambo hilo linaelezwa kufanywa pia na kambi ya upinzani Ukawa, ili kuanza mkakati maalumu utakaojulikana kama ‘Operation Delete Wabunge na Mawaziri Escrow’ itakayofanyika kwenye majimbo yote ya wabunge hao.
Hatua hiyo imeelezwa pia kuungwa mkono na wabunge wengine wa CCM waliosimama kidete kupinga na kukemea wizi huo hadi kupatikana ushindi ndani ya Bunge lililomalizika hivi karibuni.
Wanaotajwa kuathirika zaidi ni mawaziri waliojifanya kuwatetea kwa nguvu watuhumiwa huku wakijaribu kupiga kila jambo hata lile lililoonekana kuwa lina ukweli kutoka kwenye Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali.
Katika kundi la wabunge waliopona kimbunga hicho wametajwa Stephen Wasira (Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Utaribu), Profesa Mark Mwandosya (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) na Mwigulu Nchemba (Naibu Waziri wa Fedha) ambao wanaungwa mkono hata na wapinzani kutoka na kuongoza mkakati wa kukemea mawaziri wenzao ndani ya CCM waliotuhumiwa kuchota pesa hizo.
Mawaziri wengi waliobaki wote wapo kwenye joto la kusimamiwa kidete kuhakikisha wanang’olewa kwenye nafasi za ubunge majimboni kwao, ili kuwa funzo la kujali na kutambua maslahi ya taifa badala ya kutetea mambo na kuyachukuliwa kwa ushabiki wa vyama hata pale yanapokuwa na maslahi ya nchi.
Ni dhahiri kwamba wana CCM wa kweli wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Nape Nnauye wamefurahishwa na uamuzi wa Bunge na kusimama hadharani kutangaza kuunga mkono maazimiom hayo ya Bunge ya kuwaweka kando mawaziri hao kutokana na kashfa hiyo iliyotikisa nchi.
CCM imepita katika wakati mgumu kutokana na kashfa hiyo, hivyo wanakijua chama hicho na wanachama wake, wanatambua umuhimu wa kuenguliwa kwa mawaziri hao kama njia mojawapo ya kukisafisha chama wakati huo wa kuelekea uchaguzi wa Serikjali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.
Wanatambua kwamba kashfa ya Escrow imeacha doa kwa chama hicho na endapo hazitachukuliwa hatua kali na za wazi kuwawajibisha watendaji hao, chama hicho kinaweza kujikuta kwenye wakati mgumu na kuadhibiwa na wananchi kwenye masanduku ya kura.
Katika kutambua hili CCM yenye hazina kubwa ya viongozi na watendaji katika kada mbalimbali inaona kwamba haiweza kupoteza lolote kuwatosa mawaziri hao na watendaji wengine waliotajwa kwenye sakata hilo, ili ibaki heshima na imani yake kwa umma wa Watanzania.
Kuna taarifa za uhakika kwamba wananchi kwenye majimbo ya wabunge waliojifanya kusimama na kutetea uchafu huo, hawawahitaji tena wabunge hao na tayari kuna makundi makubwa ya watu kutoka Ukawa na hata ndani ya CCM yenyewe wameanza kunyemelea majimbio hayo huku wakiungwa mkono na wananchi baada ya wabunge wa zamani kupoteza ladha kwa kutetea sukari mbovu ya Escrow.
Ni dhahiri kwamba wanaiasa hao huenda kwa kutotambua au kusoma alama za nyakati walishindwa kujipanga kuona upepo ulipoelekea. Wabunge waliosimama kupinga wizi huo, wamepanda chati ghafla na wanatajwa kutokuwa na hofu kwenye uchaguzi mkuu ujao kwenye majimbo yao.
Inaelezwa wananchi wao wametambua kwamba wabunge hao ni wawakilishi sahihi wenye mtazamo wa kizalendo katika kutetea masuala yenye malahi ya Taifa. Wana imani nao kuendelea kuongoza majimbo hayo. Wabunge kama akina Christopher Sendeka, Kangi Lugola, Deo Filikunjombe na wengine ndani ya CCM waliovaa ujasiri na kuweka kando ushabiki wa chama kukemea wizi wa Escrow wametajwa kuwa ni wabunge wasio na wasiwasi kurudu bungeni mwaka 2015.
Waliojivika kutokuelewa na kupiga kelele kutangaza uhalali wa uovu huo ambao mwisho wa siku bunge limebaini kuwa uliokuwa ni wizi na uchafu na kukabidhi majina ya wahusika wakuu kwa Rais Kikwete kwa hatua zaidi, sasa hivi wanatembelea kwenye kamba nyembamba.
Wabunge hao wana nafasi ndogo ya kushinda, kwani tayari wameshaonekana udhaifu wao katika kuelewa na kutetea masuala yanayogusa taifa. Hawa wote wametajwa kuwa orodha yao itaainishwa na kupelekewa wananchi wao, ili wawakatae kwani wana upofu wa kutojua maslahi ya Taifa na ni watetezi wa watu waliopotoka.
Hivyo siku za kulia na kusaga meno kwa wabunge na wa mawaziri waliotetea Escrow ndani ya mjadala wa Bunge, zinahesabika na adhabu yao hao hakabidhiwi Rais Kikwete, bali wananchi waliowachagua.