- Ataka Watanzania kuchukua maamuzi magumu
- Asema dawa ni kuiondoa CCM, si kubadili viongozi
Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika ‘Operesheni Amsha Amsha Mzizima’, kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.
Dk. Slaa, alisema kwamba katika kipindi cha miaka 53, CCM imeshindwa kuwaletea maendeleo ya kweli na baadala yake imekuwa ikiwanyonya wanachi kutokana baadhi viongozi wake kuendekeza rushwa katika kila huduma za kijamii.
“Viongozi wote wa CCM kuanzia ngazi ya kitongoji ni wala rushwa, mfano ni pale mtu anapotaka hata kuwekewa saini kwenye barua na Mwenyekiti wa Kitongoji au Mtaa anatakiwa atoe rushwa na kwa upande wa vigogo ndio balaa,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa, aliongeza kuwa, CCM ni chama cha rushwa kwa sababu hakuna mahali popote hapa nchini mtu anaweza kupata mkopo bila kuwa na kadi ya CCM, kitendo ambacho kinawanyima baadhi ya wananchi haki.
“Tatizo la CCM sio la mtu mmoja mmoja ni tatizo la mfumo wa Chama hicho na halitaondolewa kwa kubadilisha viongozi, bali litaondoka kwa kubadilisha mfumo mzima hususani kuwachagua viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Watanzania ni walalamikaji na wanung’unikaji sana, lakini uamuzi upo mikononi mwenu… miaka 53 bado mnachagua mapanya, ukiweka chakula chako kwenye gunia la mchele hukuweka Paka, akiingia Panya anakula nusu kila gunia,” alisema Dk Slaa.
Alisema nchi haisogei mbele kutokana na watu wachache ambao ndio wanaopata kihalali huku akidai kuwa, mwaka 2007 hata Rais Kikwete alikuwepo miongoni mwa waliohusika na suala la Kampuni ya IPTL.
“CCM haina ‘shoo’ tena ya kubadilisha nchi, miaka 53 hakuna kipya kilichotokea, kuanzia sasa michango ya kipuuzi kama michango ya mwenge tunaipiga marufuku, mwenge wa Nyerere ulileta maendeleo, lakini mwenge wa Kikwete ni chanzo cha mambukizi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi,” alisema.
Naye Diwani wa Sinza, Renatus Pamba (CHADEMA), alisema mwaka 2010 wakati wanaingia madarakani, katika Manispaa ya Kinondoni walikuta mapato ya ndani yalikuwa sh bilioni 4, lakini wameweza kuziba mianya yote ya upotevu wa fedha, hali iliyofanya mapato hayo kuongezeka na kufikia sh bilioni 36 hadi sasa.
Alisema hatua walizochukuwa ni kufuta mihuri yote ya wenyeviti wa serikali za mitaa na kuandaliwa ya maofisa watendaji, na walifanya hivyo kwa sababu mihuri hiyo ilikuwa ikisababisha migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake, Maulidi Mkandu, ambaye ni mgombea wa nafasi ya uenyekiti kupitia CHADEMA katika mtaa wa Mnazi Mmoja Manzese Tip top, alisema katika mtaa huo wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo uchafu, michango ya sungusungu na ujenzi wa maabara ambayo yamesababishwa na CCM kwa kuwa wabadhirifu wa fedha na kutoweka wazi mapato ya umma.
“Kama mtaniweka madarakani nitahakikisha nawafichua wabadhirifu wa fedha, hapa kuna tatizo la taka ngumu, sungusungu na maji, hatuelewi mapato yanapelekwa wapi, nawahakikishia kuwa nitafuatilia mapato na nitakuwa muadilifu,” aliwahikishia wananchi.