Monday, December 29, 2014

Tusipokemea rushwa tutaiangamiza nchi yetu


TANZANIA hivi sasa inakabiliwa na rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kusuasua kwa maendeleo.
Baaadhi ya Watanzania wenzetu wamekuwa na tabia ya kuwakejeli viongozi wanaosimama majukwaani kukemea vitendo viovu vya rushwa na ufisadi.
Tatizo la rushwa na ufisadi liliota pembe ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hususani pale ilipojitokea kashfa ya Richomond na kumwondoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na viongozi wengine waandamizi wa Serikali wakimwemo mawaziri, Naziri Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.
Rushwa na ufisadi ni mambo makuu mawaili yanayotajwa na Watanzania wengi kwamba yataiangusha CCM. Viongozi wengi wa CCM wamekuwa hodari wa kutaja rushwa, lakini matendo yao hayaendani na maneno yao. Hata hivyo kuna kundi lingine ndaninya CCM linaloona kuwa kutaja rushwa ni kama kuichuria mkosi CCM. Kundi hili pamoja na kujua kwamba rushwa na ufisadi upo halidiriki hata siku moja kwa ndimi zao kukemea na kutaja neno “rushwa” au “ufisadi”.
Kundi hili linaona kana kwamba kutaja neno rushwa au ufisadi ni kujidhalilisha bila kujua kwamba kufanya hivyo kwa vitendo , ndio kukijenga na kukitakia mema chama. Kumbukumbu zipo pale Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliposimama hadharani na kukemea vitendo vya rushwa na ufisadi ndani ya  chama chake.
Kilichofuata baada ya hatua hiyo ya ujasiri, ni kiongozi huyo kupingwa  na hata viongozi wa juu wa chama, wakati huo Katibu Mkuu wa CCM akiwa Luteni mstaafu , Yusuf Makamba aliyemtaka  atumie vikao vya chama kuzungumza mambo hayo.
Tatizo linaloathiri CCM na huenda likahitimisha zama za uongozi wake ni woga wa viongozi wake kukikosoa chama na kutamka ukweli hadharani kama alivyokuwa akifanya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Kuna viongozi wachache sana ndani ya CCM wenye uwezo wa kusimama na kukosoa chama au serikalipale inapokwenda ndivyo sivyo, mfano mmojawapo wa viongozi hao, ni pamoja na Katibu Mkuu wa sasa wa CCM,  Abdulrahman Kinana.
Rushwa  iliponuka ndani ya CCM na baadhi ya viongozi wake kuonekana kero kwa umma na kuanza kukipoteze umaarufu chama hicho, kilianzisha mkakati wa kujivua gamba. Mkakati huo ulioanzishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM , Wilson Mkama ulikuwa  tiba kamili ya kuiponya CCM  na kuiepusha na viongozi wasiofaa, wala rushwa na mafisadi na hata wale wanaotajwa tajwa tu, bali kwa nia njema ya kukinusuru chama, ulikwama matokeo yake Mkama kujikuta akiwa mhanga mwenyewe kwa kuenguliwa kutoka nafasi hiyo.
Viongozi wengi wa CCM huenda ni kwa kulewa madaraka au kiburi tu, hawajitambui hususani pale wanapotembea kwenye ‘reli ya rushwa au ufisadi’. Viongozi hao wamekuwa ni mioyo migumu kama ule wa aliyekuwa mtawala wa Misri Farao, kujiuzulu kwa kosa lolote hata pale wanapohisiwa tu. Kuna hisia mbaya  ambazo wakati mwingine zinakuwa hazina ukweli, lakini kwa kiongozi madhubuti mwenye maadili ya dhati, haoni shida kujiuzulu wadhifa wake hata pale tu anapohisiwa.  Huo ndio usafi wa viongozi wenye nia na dhamira ya dhati kutumikia umma.
Tumeona  mifano ya namna viongozi wa dola nchini Kenya walivyojiuzulu akiwemo Mkuu wa Jeshi la polisi la nchi hiyo kutokana na matatizo ya kiusalama . Tukiangalia mfano huo mwema tunaoanisha na viongozi wetu hapa nyumbani  ambao hivi karibuni walizua mtafaruku mkubwa ndani ya Bunge kiasi cha kutaka kumponza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuachia nafasi yake. Viongozi hapo pamoja na mapendekezo ya kiungwana kabisa ya wabunge wa pande zote chama tawala CCM na wale wa upinzani kuwataka waachie kazi, bado wanasubiri eti mpaka  Rais awaachishe kazi!
Inasikitisha! Kwa kiongozi muungwana mtafaruku unapofikia kiwango cha juu kama ilivyotokea ndani ya mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni, hana sababu ya kusubiri eti akabidhiwe kwa mamlaka ya juu ili imwajibishe, ni wajibu wake kufanya hivyo hata kama hakufanya kosa hilo, lakini zogo pekee ndani ya Bunge linatosha kumfikisha kwenye maamuzi ya kujiuzulu, ili kulinda heshima yake na umma wa Watanzania kwa ujumla.
Kujiuzulu kwa wanasiasa ni heshima na kielelezo cha maadili mema ya utumishi wa umma, sio kusubiri utolewe ndani ya chumba wakati unaona umesabaisha ‘moshi wa kutisha’ na ili chumba kiwe salama ni wewe kutoa nje, bado unang’ang’ania.  Hapa tunapata picha na kilelezo thabiti kwamba tuna viongozi wa namna gani ambao hawawezi hata kumhurumia Rais wetu mpendwa ambaye hivi karibuni ametoka hospitali kwa matibabu makubwa.
Watu wa namna hii wanamjaribu nini Rais wetu? Rais ana watu wengi na Tanzania ina hazina kubwa ya watendaji wenye uwezo wa kutukuka na kamwe mtu mmoja hawezi kuwa bora kuliko watu wengine. Njia bora ya kiungwana ni kuchukua hatua ya kuondoka mapema kabla ya kusubiri maka Rais akuambie kufanya hivyo.
Viongozi shupavu wa kukemea rushwa kama Sumaye na wengine akina Kinana na Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye,  wameuwa wakiimba juu ya tatizo la rushwa kila wakati, lakini  baadhi ya watendaji hawasikii. Mfano Sumaye karibu kila hotuba yake amekuwa akikosoa na kuonya kuhusu rushwa na ufusadi, badala ya viongozi kutuliza masikini na kutafakari hayo baadhi wanaishia hata kudhihaki maneno yake.  Kinachotia moyo ni kwamba mtu mkweli daima huwa hachoki kusema  kupigania na kusimamia kile anachoona ni kweli.
Viongozi wetu wangekuwa watu wenye kujali na kusikia maneno kama hayo naamini haya yaliyotokea ya viongozi kuchota mapesa kwa ‘lumbesa’ yasingetokea. Inasikitisha kwamba watu wa kunena na wenye maono tunao, wanaonya na kukemea lakini watu wana macho  lakini hawaoni, wana masikio lakini hawasikii, matokeo yake ni kuwa na  vongozi wa ovyo wanaoingia au kuhusishwa na mambo machafu kinyume cha maadili ya viongozi.
CCM ifike mahali sasa ikubali kukosolewa kujikosoa na kuwapa nafasi viongozi wake wanaikosoa, ili kuonyesha njia sahihi na mwelekeo wa chama badala ya kubeza wakati kuna tatizo linalotengeneza ‘kansa’ kubwa ndani ya chama.  Kama maneno ya akina Sumaye na akina Nape yasingebezwa ndani ya chama, CCM ingekuwa na viongzi waadilifu wenye miguu ya kusimama mbele ya Watanzania bila mashaka.
CCM inapokwenda kutafuta mgombea wake mwaka 2015 izingatie suala la usafi  wa kiongozi, uwezo na ujasiri wake wa kukemea, kuonya na kuonyesha mwelekeo wa maadili ndani ya chama , taifa sambamba na kujenga uchumi imara.