MIAKA ya nyuma kulikuwa na kitabu kimoja cha hadithi chenye hadithi ya kusisimua ya “Muwa uliozamisha Meli” kilichoelezea Manaodha wa meli walionogewa na utamu wa muwa waliokuwa wanakula ndani ya meli kiasi cha kusahau kuongoza meli hadi ikazama.
Manahodha hawa wanafanana na viongozi wetu wa leo wanaoliongoza taifa letu na kushika nyadhifa nyeti wanaonekana kunogewa na utamu wa madaraka kiasi cha kutowajibika na kuizamisha nchi katika dimbwi la umasikini, upotevu wa rasilimali za nchi, huduma mbovu za kijamii bila kujali.
Fahari za uongozi, magari ya kifahari, posho lukuki na bahasha za bashasha zimewavua uzalendo na uwajibikaji wamebaki watupu, wameishiwa japo ni waheshimiwa.
Wamekua waking’ang’ania na kupigania, kutetea utamu wa uongozi kuliko kuwatetea wananchi na kulinda maslahi ya nchi, jambo ambalo linazidi kuizamisha meli ya Tanzania.
Ili kuendelea kufaidi utamu huu, wamewaka mifumo ya kulindana na kubebana na kutengeneza makundi ndani ya vyama vyao vya siasa, ili wabaki kuwa juu zaidi pasiwepo na kuwashusha hata kama wanaizamisha nchi.
Viongozi hawa wanafurahia na kuona fahari ya utamu wa viongozi kuliko kuwatumikia wananchi. Uongozi kwao si mzigo bali ni dili ni sehemu ya kutajirikia.
Ni wazi kuwa manahodha kama hawa wataendelea kuizamisha Tanzania yetu kama wataendelea kuachiwa uskani ilhali wako bize wanakula muwa wameshasahau uskani wao. Hawajui hata ulipo sijui wamewaachia wawekezaji, matajiri na wafanyabiashara.
Siku zote utamu ukizidi unakua sumu, Waingereza wanasema “too much of everything is harmful” utamu huu unageuka sumu na kuuwa maadili ya uongozi, uwajibikaji, usimamizi wa rasilimali za nchi unakua mbovu kwa sababu kila mtu anataka utamu.
Utamu huu wa madaraka umesababisha ulevi wa madaraka, kulewa kiasi cha kutojali wananchi ambao kibiashara ama kimtaji wanaitwa wapiga kura.
Ulevi huu ukizidi unasababisha uteja wa uongozi, kiongozi anaona kuwa hawezi kuishi bila kuwa kiongozi kwa sababu ya utamu wanataka kuwa viongozi mpaka kufa, yuko tayari kung’ang’ana kwa gharama yoyote hata kama amelisababishia taifa hasara.
Uongozi wa namna hii unafananishwa na hotcake umesababisha watu wawe na uroho wa madaraka na uchu usiopimika hawako tayari kuukosa wanaupigania kwa gharama yoyote hata kwa rushwa, mbinu chafu, umwagaji damu, kuchakachua na aina zote za udanganyifu wanazozijua.
Utamu wa madaraka unawazidia viongozi mpaka wanasahau kuwa wameshikilia uskani wa nchi, nchi inakosa mwelekeo matokeo yake inaanza kuzama polepole.
Ulevi huu wa madaraka umesababisha athari nyingi viongozi kufanya maamuzi ambayo yanaligharimu taifa kwa kiasi kikubwa mfano msamaha wa kodi kwa wawekezaji wanaovuna mabilioni ya rasilimali za watanzania na kuhodhi mamilioni ya hekari ilhali mmachinga analipa kodi licha kipato chake kidogo.
Utamu wa madaraka umewasahaulisha viongozi wengi wajibu na majukumu waliyonayo kwa nchi kiasi cha kuufanya uongozi uonekane kuwa ni ulaji ambao umekua ni dawa ya usingizi inayowafanya viongozi walale fofofo, wajisahau.
Viongozi wamelemewa na utamu wa uongozi hawataki kubeba jukumu la kujiwajibisha wala kuwawajibisha wengine kwa manufaa ya wananchi.
Kumekua na vitendo vingi vya ubadhirifu, ufisadi na wizi wa fedha za walipa kodi, lakini viongozi hawataki kuwajibika wamenogewa na utamum bora nchi izame waendelee kufaidi utamu.