Thursday, March 12, 2015

PAC yaagiza CAG uchunguzi wa milioni 699/- za Tanesco.

12th March 2015
Chapa
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemwagiza Mdhibti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi kubaini zilikopotelea Sh. milioni 699 zilizotolewa na Wizara ya Fedha kwenda Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambazo hazijulikani ziliko sasa.
 
Aidha, PAC imeagiza Tanesco kuwasilisha katika ofisi ya Bunge mikataba yote ya kampuni zinazozalisha umeme nchini ambazo zimeingia nayo mikataba ili kupitiwa upya na kuwa kumbukumbu kwa Bunge.
 
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alitoa maelekezo hayo jana katika kikao baina ya kamati hiyo na menejimenti ya Tanesco na kusema kumekuwa na mvutano kuhusu Sh. milioni 699 zilizotolewa na Hazina kwenda Tanesco.
 
Zitto alisema inawezekana fedha hizo zimetolewa kwa Tanesco, lakini zimetumika vibaya au Hazina wamezitoa kwa mtu tofauti, hali ambayo imekuwa ikileta mkanganyiko ambao unahitaji kufanyiwa uchunguzi.
 
Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha Tanesco, Anetha Chegula, alisema fedha hizo zinadaiwa kutolewa na Hazina tangu mwaka 2012 kwenda Tanesco kwa ajili ya kusaidia miradi ya umeme, lakini hazijafika katika shirika hilo licha ya Hazina kuonyesha kuwa zilishatolewa.
 
Chengula alisema wamekuwa wakiitaka Hazina kuonyesha vielelezo vinavyoonyesha kuwa fedha hizo zimepelekwa Tanesco, lakini hadi mwaka jana Hazina haikufanya hivyo huku Tanesco ikifanya uchunguzi katika akaunti zake bila kuziona fedha hizo.
 
Akizungumzia mikataba ya makampuni ya Agrecco, Symbion, Songas na IPTL , alisema ipelekwe haraka ofisi za Katibu wa Bunge ili iwe kumbukumbu kwa Bunge.
 
Wabunge walisema tozo ya uendeshaji wa mitambo (capacity charge) iangaliwe upya kwa sababu inaingiza gharama kubwa kwa Tanesco, hivyo kushindwa kufikia malengo ya kujiendesha badala yake kuendelea kutegemea serikali kulisaidia.
 
Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy, alisema ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini ni kwa Tanesco kuchukua hatua ya kuinunua mitambo ya umeme inayomilikiwa na kampuni zinazozalisha umeme na kuiuzia Tanesco kwa bei ya juu.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba (pichani), alisema Songas inalipwa Sh. bilioni 8.562 za tozo ya uendeshaji, IPTL Sh. bilioni 4.302 na Aggrecco Sh. bilioni 1.600 kwa mwezi. Mramba alisema Aggreco imekuwa ikiiuzia Tanesco umeme kwa Dola za Marekani senti 40 na IPTL senti 23 huku Tanesco ikiuza umeme huo kwa senti Dola za Marekani 26.
 
CHANZO: NIPASHE