Mbio za uchaguzi mkuu wagombea watizamwe hivi!
Si mbaya kuwafahamu watakaowaongoza lakini ni vyema kujua zaidi uwezo wa marais, madiwani na wabunge wajao, je historia zao zinasemaje, wana haiba gani (personality/ character) pia uadilifu wao ukoje?
Katika kuwachunguza viongozi watarajiwa kuna baadhi ya vidokezo vinavyowazungumzia viongozi na sifa zao kama vinavyonukuliwa kutoka kwenye machapisho na mihadhara ya Mhubiri wa Kimataifa hayati Dk. Myles Munroe, wa Huduma ya Bahamas Faith Ministry, ambavyo kiongozi kwa mtizamo wake anahisi analazimika kuwa navyo.
Akizungumza katika moja ya mihadhara wakati wa uhai wake (alifariki mwishoni mwa mwaka jana katika ajali ya ndege) aliainisha kuwa kiongozi haimaaniisha kuwa mtu aliyefanya mambo makubwa ya kutisha tena mwenye mafanikio makubwa, kwa mfano pengine tajiri wa kwanza duniani Bill Gates wa Marekani ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Computer ya Microsoft.
Japo ni bilionea na mashuhuri lakini si kwamba unapozungumzia viongozi wote si lazima wawe na sifa za utajiri, umaarufu au kuwa wakipekee duniani sivyo anasema la muhimu ili uwe kiongozi ni lazima uwe na maono, muadilifu mwenye haiba pamoja na karsima au karama.
Akianza na maono anazungumzia suala la kuwa na maono na malengo yanayotekelezeka tena uwezo wa akili za kuyaweka mambo yaende sawa na kuwahamasisha wale anaowaongoza kuleta mafanikio na kutekeleza malengo wanayojiwekea.
Kiongozi awe wa kitaifa, mbunge, diwani, mkuu wa mkoa, wilaya au mkurugenzi wa shirika la umma ama la binafsi ni lazima aweze kufanikisha malengo na maono aliyoyaweka yawe ya kampuni, kiwanda ama serikali au jimbo ni sharti awe na uwezo wa kuyatimiza kwa ushindi unaoonekana.
Unaposema huduma za afya kwa kila Mtanzania, kama ndilo lengo basi watu waone miundombinu, wataalamu, vifaa , dawa na kuhakikisha kuwa wananchi wanapona na kampeni zimefanikiwa kutokomeza maradhi.
Mhubiri huyu wa kimataifa anasema kabla hujajiingiza kwenye kutangaza nia ya kuwa kiongozi chunguza uadilifu wako.
Uadilifu ni ile hali ya ukweli (faithfulness and diligence) kwa nafsi zao, Mungu wao na wale wanaotarajia kuwaongoza. Kadhalika ni kwa kiasi gani wana kasrima.
Haya ni mahojiano yako na Mungu wako.Anataka kiongozi ajiulize yukoje kiuaminifu? “Jipime katika maeneo haya- hofu ya Mungu, kutumia na kulinda mali zako na za umma, fedha unazokabidhiwa, utendaji kazi, uhusiano na wenzako, familia yako na ujue kama ni mwaminifu ama vipi.
Huu mtihani wa uadilifu (diligence) baina yako na Mungu maana unayeyajua majibu ni wewe binafsi.”
Haitoshi watu kusema mgombea huyu amefanya mambo makubwa , ana uwezo huu ama ule. Sifa za wapambe hazijengi wala hazikupi uadilifu huo ni uchunguzi wako binafsi na Mungu unayemwamini.
UONGOZI NI NINI
Dk Myles Munroe anajibu kuwa unajumuisha mambo mengi lakini , ni muhimu katika kuendeleza shughuli na michakato duniani lakini pia unahitajika ili kuwafunza na kuwaandaa wengine watakaoongoza sekta na mapambano ya kuleta mabadiliko na hali bora za maisha ya watu na kuufanya ulimwengu kuwa mahala pazuri pa kuishi.
Anakumbusha kuwa hakuna neno moja linaloweza kutumiwa kumzungumzia anayetakiwa kuwa rais, mbunge, diwani au kiongozi maana mambo ni mengi na hakuna sifa pekee ya kumweleza kiongozi.
Hata hivyo Munroe anaona kuwa kiongozi ni huyo ambaye anateuliwa ama kuchaguliwa kuliongoza kundi timu, shirika na taifa.
Anaelezwa kuwa kiongozi anatakiwa kuwa na karisma au mwenye uwezo wa kufanya maamuzi muhimu, mwenye mvuto na haiba anayeweza kuwashawishi wengine.
Kwa kifupi uongozi ni ‘charism’ au karama ambayo inahusisha haiba kubwa na ni kipaji kutoka kwa Mungu.Kadhalika ni uwezo wa kimamlaka unaoweza kuwasiliana na wengine kikamilifu kuhamasisha wengine kufanya yale yaliyokusudiwa na kuona kuwa yanaleta manufaa.Si kuibuka na kueleza kauli mbiu za kufurahisha lakini zisizotekelezeka. Kwa ujumla kiongozi awe na uwezo wa kushawishi wengine na kuwabadilisha kwa namna bora .
VIGEZO VYA KIONGOZI
Ili uwe kiongozi ni lazima uwe na kundi unaloshirikiana nalo linalofuata maelekezo au nyayo zako na lenye imani na maono, malengo na maongozi yako.Kama kiongozi una jukumu kwa watu wako wawe wapiga kura, wafanyakazi wataasisi la kuwaongoza kwa weledi na haki, uhuru na kwa maadili na uadilifu pia na kuonyesha karama yako.
Vyeo vya kimamlaka vinavyohusisha kutukuzwa kama “mheshimiwa, bosi, chifu,mkurugenzi, baba, mtukufu” hakika havikufanyiwa kuwa kiongozi bora wakati mwingine vyaweza kuwa kejeli.
YAKUFANYA
Kuwa kiongozi bora unahitajika kujiweka sawa na viwango vya juu na vya wakati wa sasa vya marais au viongozi wengine wakuu duniani na kikanda, hivyo fuatilia nyendo za viongozi wenzako duniani wanavyopambana na kuondoa matatizo mbalimbali.
Kwa mfano utasikia Baba Mtakatifu Papa Francis anatembelea makundi ya watu maskini, anazungumza na kujichanganya nao mitaani.
Anafahamu nini anachotakiwa kufanya kuwagusa wote anaowaongoza na ikibidi kuwafikia kwa kuwa kuongoza ni ‘karama’ kipaji alichopewa na Mungu analazimika kwenda kwa watu duni pengine wasiofikiwa wala kukumbukwa na viongozi!
Kama ni rais angalia jinsi wale wa kalba yako (marais wenzako) wanavyofanya, mikakati na mipango ya maendeleo ya kuyawezesha mataifa yao kung’ara kwenye ramani ya dunia.
KUSOMA
Rais, mbunge ama mkurugenzi unalazimika kusoma machapisho ya aina mbalimbali kuanzia ripoti za kimataifa, za kiuchumi za Afrika, Umoja wa Mataifa, habari za mbadiliko ya tabia nchi. Kadhalika jifunze kuwa mkweli siyo kuongea mambo ya kudandia bila kuwa na vyanzo vya uhakika.
Soma magazeti ya kimataifa na ya kitaifa, tizama habari na matukio mbalimbali duniani kwenye televisheni, soma machapisho ya mitandao mbalimbali na unapozungumza kuwa na mamlaka yaani uwe unaelewa mambo. Kuwa mtu wa kutumia watalaamu na kufanya tafiti uwe gwiji la uelewa.
Lazima ufahamu habari za kibiashara na uchumi duniani kupitia machapisho mbalimbali, angalia viongozi , watizame wenzako katika mashirika mbalimbali duniani na katika tasinia za kimataifa na kikanda ujue wanafanyaje? Jipime wewe uko wapi katika ngazi za viongozi kitaifa na kimataifa? Waheshimiwa fanyeni tafiti si kukurupuka na kusema chama chetu kitashinda kwa wimbi la tsunami ama wakati wa kukiondoa chama tawala ni huu, umetafiti? Umezungumza na wananchi?
Kutafiti, kujisomea na kufahamu mambo mengi kutakupa mwelekeo na jinsi ya kuwa kiongozi bora na mweledi huku ukijijengea uzoefu wa kipekee kukabiliana na changamoto unazozifanyia kazi.
Kwa hiyo mnapoelekea kwenye uchaguzi mkuu jaribuni kujichunguza na kujiweka kwenye viwango na mjiulize ninastahili? Na nyie wapambe na mashabiki angalie tunayemtaka anatufaa? Ana vigezo? Au mkishahongwa mmeridhika. Mnawajibu wa kumtafakari kwa viwango hivyo.
CHANZO: NIPASHE