Mtei na ndoto za Chadema kushika dola 2015
11th March 2015
B-pepe
Chapa
Hiyo ni kauli ya matumaini. Ni kauli inayotoka mdomoni mwa Muasisi na Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Edwin Mtei, akielezea jinsi anavyoona na matarajio yake kwa Uchaguzi Mkuu ujao.
“Nakukaribisha siku hiyo na huu ndio mwaliko wako, uje kusherehekea ushindi wa Chadema hapa nyumbani, kabla ya viongozi hao kwenda kuapishwa Dodoma.”
Alikuwa akizungumza na mwandishi wa makala hii nyumbani kwake eneo la Shangarai, wilayani Tengeru, Mkoa wa Arusha.
Kauli ya Mzee Mtei imekuja siku chache baada ya Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, mwishoni mwa mwezi ulipita kuwa chama hicho kimeandaa mikakati ya kutwaa dola Oktoba, mwaka huu.
Golugwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, anasema hawataki tu kuwa na chama maarufu ila kuchukua dola, tena sio miaka mingi ijayo ila Oktoba mwaka huu.
Akiweka msisitizo, Mtei anasema uchaguzi mkuu ujao ndio utadhihirisha matakwa ya demokrasia.
Anasema Chadema itachagua mgombea makini mwenye maadili na sifa ya kuongoza nchi. Mtu mwenye upeo na mawazo ya maendeleo kwa wananchi na taifa.
Ukawa
Akizungumzia kuhusu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anasema mgombea wa Chadema atashindanishwa na wagombea wengine kutoka umoja huo kwa mujibu wa makubaliano yao ya kusimamisha mgombea mmoja.
“Mimi ninaamini katika demokrasia ya ushindani, ndiyo demokrasia yenyewe kwamba kila chama kichague mgombea mmoja na kumshindanisha ili kumpata mgombea bora atakayekubalika,” anasema.
Hata hivyo, anasema, “hatutakubali kuangusha wengine ili kumpata mmoja, lakini tukimpata mmoja huyo aliyeachwa tutamweleza aendelee kubaki kwenye chama.”
Anasema anaamini katika siasa au demokrasia za ushindani na kama kuna chama hakina mwelekeo huo basi kinaweza kufa.
Kuhusu uchaguzi mkuu, anasema, “Tunatarajia utakuwa uchaguzi huru, kila lazima ashiriki na kikubwa zaidi kupiga kura ili kuhakikisha kwamba wanatumia uhuru wao,” anasema.
Akitahadharisha kuhusu uvunjifu wa demokrasia katika uchaguzi, haraka haraka anakionya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kutumia pesa za walipakodi ambazo baadhi ya wagombea wao waliziiba zamani.
Anasema kwa muda mrefu chama hicho kimekuwa kikivuruga chaguzi mbalimbali na kuzifanya kuwa sio huru na wakati mwingine kimekuwa kikitumia mbinu za kupeleka mafisadi na watu walioiba fedha za walipa kodi kuhakikisha wagombea wa CCM wanapita.
“Wasitumie pesa zetu ambazo walituibia zamani na wengine ambao wamezificha nje ya nchi kuhonga watu wetu ili wasishiriki,” anasema na kucheka kidogo, na kuongeza, “hata zile fedha za IPTL ni zetu.”
Anasema kuna baadhi ya watu walisema wasusie uchaguzi mkuu, lakini anaona lazima washiriki na kutekeleza demokrasia yao.
Anasema anayo matumaini makubwa ya Chadema kuungwa mkono na watu wengi na hiyo inatokana na jinsi walivyokihamasisha na kukiuza chama hicho kwa wananchi na sasa kinakubalika.
“Kutokana na mwamko wa chama chetu na jinsi tulivyowahamasisha wananchi; na CCM inavyotumia nguvu kubwa kupambana na Chadema, ikiwa ni pamoja na nguvu ya ufisadi kuhonga wanachama ili kuleta mgongano ndani ya chama, nadhani wananchi kwa kuelewa hilo wanaweza kutuunga mkono katika harakati zetu za kutwaa dola Oktoba 2015,” anasema.
Anasema nafasi zote za wagombea katika uchaguzi mkuu kuanzia udiwani, ubunge na urais, wataungwa mkono na wananchi na kushinda na ishara hii inatokana na matokeo mazuri ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ulifanyika Desemba 14, mwaka jana.
Mathalan, anasema, “katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tumeonyesha kuwa sisi ndio chama kinachokubalika na sasa tutaendelea katika ngazi kata, majimbo na taifa.”
Anasema mikakati mingi ya kukinadi chama ndiyo ilisaidia kukifikisha hapa kilipo hali ambayo inawafanya waendelee kusomba watu wote kuanzia ngazi ya mashina, kitongoji, kijiji, mtaa, kata, tarafa, jimbo hadi taifa, na hii ndiyo kielelezo cha ushindi.
Changamoto BVR
Anaangalia changamoto katika mfumo wa kielektroniki wa kuandikisha wapiga kura (BVR) kama teknolojia ambayo haiwezi kuepukika katika nyakati hizi za maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia.
Hata hivyo, anasema matatizo yanayotokana na mfumo huo ni kwa sababu ya uwezo mgogo wa serikali na nchi.
Anasema serikali haikuweza kuandaa wataalam wenye uwezo wa kuzifanyia matengenezo mashine hizo au namna ya kuziendesha.
“Ni lazima na mwelekeo ulivyo, sasa ni lazima tutumie vifaa hivyo, kama shida itakuwa muda hautoshi, wanaweza kuongeza muda hadi Julai au Agosti, ili kuwapa watu wengi nafasi ya kujiandikisha na hivyo kupiga kura.
CCM imeshindwa?
Kuhusu CCM, Mzee Mtei hamung’unyi maneno, anasema moja kwa moja kwamba chama hicho kikongwe kimeshindwa na kupoteza mvuto kwa Watanzania. Kwa kifupi anasema hakikubaliki isipokuwa kwa wale wachache wenye maslahi nacho.
Anataja kwa mfano, Watanzania wanakufa kwa njaa kuanzia Ukerewe, mkoani Mwanza hadi Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Anasema wakati wananchi wanakufa njaa, yapo mashamba mengi na makubwa yameshindwa kulima, huku fedha nyingi ambazo zinatolewa na washirika wa maendeleo haziwafikii wahusika.
Migogoro ndani ya chama
Anasema inapotokea inakiimarisha chama, na inatakiwa kutatuliwa kwa misingi ya kidemokrasia.
“Unajua kila mwanasiasa lazima awe ambitious, atake ukubwa kuliko pale alipo; na hii ni demokrasia, lazima kuwa na ushindani,” anasema.
Pamoja na siasa, Mzee Mtei anajishughulisha na kilimo cha mahindi, kahawa na ufugaji wa nguruwe na ng’ombe wa maziwa.
Anasema kwa mfano, mwaka huu amavuna tani 1, O30 za mahindi katika shamba lake la hekari 95.
Anasema ameuza mahindi hayo na kutenga magunia machache kwa ajili ya chakula chake kwa mwaka mzima, magunia 40 kwa ajili ya chakula cha nguruwe wake 37 yakiwemo madume mawili.
CHANZO: NIPASHE