Thursday, March 12, 2015

Wanawake wataishi kwa hofu vijijini hadi lini


ChapaDunia inapoadhimisha Siku ya Wanawake duniani mamia ya wanawake vijijini wanaishi kwa hofu kwani ni walengwa wakuu wa kila sababu ya mauaji. Wanasingiziwa kuwa wachawi, wanadaiwa wasababisha mikosi, maadui wa mvua lakini pia wanageuzwa viambato vya kutengeneza dawa kwani miili yao inachanganywa mambo mengine kuleta utajiri na mafanikio.  

Mauji ya wanawake yamekithiri maeneo ya Ukanda wa Ziwa mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Kagera na Simiyu na kila mara imeshuhudiwa wazee, mabinti na hata walemavu wakiuawa kwa visingizio mbalimbali vinavyohusisha uchawi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (HLRC) cha jijini Dar es Salaam, kinasema wanawake zaidi ya 1,000 wameuawa mwaka jana na kwamba kuanzia mwaka 2010 hadi sasa zaidi ya wanawake 3,000 wanaotuhumiwa kuwa ni wachawi wamepoteza maisha wakiwa na umri kati ya miaka 50 hadi 80.

Wauaji huwashambulia kwa mapanga, visu, kuwachoma moto wakiwa hai mabaki ya miili yao huteketezwa pia wala asitokee mtu wa kuwatetea.

Taarifa zinaeleza kuwa mauji hutokea usiku wa manane, milango huvunjwa kwa mawe makubwa ama wauaji huvizia na kuingia vyumbani wanapolala wanawake, ambao bila msaada wanakatwa kwa mapanga, visu, kuchomwa moto na nyumba zao kupigwa kiberiti.

Wanadaiwa ni wauaji wa watoto  Mikoa ya Kanda ya Ziwa ni kitisho mwanamke anaweza kunyanyaswa akatumiwa radi au mvua ikanyesha juu ya paa lake, akang’olewa mazao shambani, mifugo yake ikauliwa na pia anaweza kuchomwa ndani ya nyumba pamoja na wajukuu zake nyakati za usiku.

Yote hufanyika kwa wasio na hatia kwa vile hakuna ukweli kuwa ni wachawi. Mwalimu Mbuke Mayala wa mkoani Tabora, anasema katika mahojiano ya simu kuwa mauji haya yanachochewa na serikali kushindwa kudhibiti wauaji na kukomesha matendo hayo maovu kwa vile haitafuti kiini cha watu kuendelea kuamini uchawi na kuwa watumwa wa imani za kishirikina.

“Muda wote imeendelea kuwatumia polisi, mahakama na sheria lakini bila kukomesha tabia zilizo ndani ya mioyo ya watu kuendekeza uchawi na kuamini kulogwa kwa muda mrefu.”

Mwalimu Mbuke mkazi wa kijiji cha Witangh’olo mkoani Tabora, anaeleza zaidi kuwa ushirikina umejikita zaidi kwenye ukanda huu ambao wengi hawana elimu , wanaamini imani za kimila na matambiko ya kijadi na pia hakuna huduma za afya zinazoweza kutumiwa kupunguza vifo na kukabiliana na maradhi kama Virusi Vya Ukimwi (VVU), vifo vya watoto na wazazi wao, malaria na pia magonjwa yanayoweza kuepukwa.

Anasema waganga ndiyo wanaotegemewa lakini hawafahamu chanzo wala hawana tiba za magonjwa ambayo kama kungekuwa na huduma za afya wananchi wangehudumiwa na kupona.

Mbuke anasema elimu duni inasababisha jamii kuamini mambo kama kuzaa watoto mapacha ni mkosi, mtoto anayezaliwa akitanguliza makalio analeta balaa na wanalazimika kufanyiwa matambiko.

Kadhalika watu wanaendeleza mila za kurithi wajane , kuwatakasa na kuoa wanawake kwa imani mbalimbali wengine wakiamini wana mikono ya pesa au wanazaa watoto wa kiume.

Ushirikina wa kuua albino umewaumiza zaidi wanawake na watoto wadogo. Hivi karibuni Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, ilitoa taarifa ya kuionya Tanzania kuhusu mauaji ya albino na kulaani kitendo cha kuwateka na kuwaua watoto albino.

 Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN Zeid Ra’ad Al Hussein, katika taarifa hiyo alisema mauaji yataongezeka kwa vile kinakaribia kipindi cha uchaguzi Oktoba mwakani. Idadi ya wanawake albino waliouliwa ni wengi ikilinganishwa na wanaume.

Hawa huuliwa kwa vile hawawezi kujitetea na hawana nguvu. Lakini pia ni ukweli kuwa wanaonewa na jamii muda wote.

Kwa mujibu wa Chama cha Albino Tanzania kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita zaidi ya albino 75 wameuliwa licha ya kwamba hazikutolewa takwimu kijinsia lakini idadi kubwa ni wanawake na wanaweza kufikia karibu 40.Hawa wanaozungumziwa ni wale ambao taarifa zao zinafahamika.

Wapo waliochinjwa kwa siri na haikujulikana hadi leo hatima yao.
Lakini cha kushangaza zaidi waliotiwa hatiani ni wafungwa 10 pekee kati yao wapo waliohukumiwa kifungo cha maisha na wenye adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Ili kutokomeza mauaji ya albino, kuua wanawake na kuendeleza imani za kishirikina serikali inawajibika kutoa elimu shuleni na ile ya kuhamasisha jamii kuachana na ushirikina.

Kadhalika kujenga miundo mbinu na kutoa huduma za afya na kushirikiana na wadau wengine kutokomeza mauaji ya Watanzania wasio na hatia kwa kisingizio chochote.

Mauaji ya wanawake na wazee huambatana na watu wanaowalisha watuhumiwa dawa za kubaini ‘wachawi’ waganga wanadai ukitumia dawa hizo lazima utaonyesha dalili zinazohusiana na matendo hayo.

Kupitia elimu serikali na wadau wakomeshe tabia za baadhi ya watu wanaozurura mitaani kujidai wanaumbua wachawi. Pia sheria ziwepo na mienendo hiyo idhibitiwe ili kuwanusuru wanawake wengi wanaouliwa bila hatia.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI