RAIS anayeondoka madarakani nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba
Huyu ndiye Rais Pohamba mshindi wa tuzo ya Mo Ibrahim
RAIS
anayeondoka madarakani nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba (79),
ameingia kwenye historia ya washindi wa tuzo ya dola milioni tano ya Mo
Ibrahimu ya uongozi wa Afrika.
Rais huyo ambaye anatarajiwa kumkabidhi madaraka yake kwa rais
mteule, Hage Geingob, anakuwa kiongozi wan ne kukwaa tuzo hiyo,
akitanguliwa na Joachim Chissano wa Msumbiji (2007), Festus Mogae wa
Botswana (2008) na Pedro Pires wa Cape Verde (2011).
Tuzo hiyo ya dola milioni 5 hutuzwa kiongozi wa Kiafrika
aliyechaguliwa na anayeongoza kwa njia bora na kuinua maisha ya watu na
kuondoka madarakani.
Rais mtaafu wa Msumbiji mwaka 2005, Chissano ndiye alikuwa wa kwanza
kutunukiwa tuzo hii ya heshima mwaka 2007, huku miaka mingine ikipita
bila kupata mshindi kutokana ugumu wa vigezo.
Salim Ahmed Salim- Mwenyekiti wa kamati inayotafuta mshindi wa tuzo
hiyo iliyotolewa Nairobi nchini Kenya, anasema Namibia chini ya Pohamba
imeweza kuwa na utawala mzuri na kujiletea heshima. Anaongeza kuwa
Namibia chini ya Pohamba ina demokrasia ya kweli, imekuwa imara na
inayoheshimu uhuru wa habari na haki za binadamu,
Tuzo hii ni malipo ya awali ya dola za Marekani milioni 5 (sawa sh.
bilioni 8.3) zinazotolewa kwa awamu kwa kipindi cha miaka kumi, zaidi ya
malipo haya Pohamba atapewa dola laki 2 kwa kila mwaka kwa maisha yake
yote.
Pia tuzo hii inaaminika kuwa kubwa na yenye thamani zaidi duniani
ikiipiku Tuzo ya Nobeli ya Amani (Nobel Peace Prize) kwa zaidi ya mara
tatu na nusu. Mshindi wa Tuzo ya Nobel anapewa kiasi cha dola za
Marekani milioni 1.3.
Tuzo ya Mo Ibrahim inatolewa kwa Rais aliyemaliza muda wake Afrika na
mchakato wa kumpata unafanywa na kamati maalumu ya watu mashuhuri;
kamati hii pia inajumuisha watu wengine wawili waliowahi kupata tuzo ya
Nobel.
WASHINDI
2007-Joachim Chissano (Msumbiji)
2008-Festus Mogae (Botswana)
2009- Hamna tuzo iliyotolewa
2010- Hamna tuzo iliyotolewa
2011-Pedro Pires (Cape Verde)
2012-Hamna tuzo iliyotolewa
2013-Hamna tuzo iliyotolewa
2014- Hifikepunye Pohamba (Namibia)
Tuzo hii inatolewa ili kutambua na kusherehekea viongozi wa Afrika
waliotumia uwezo wao kuzijenga nchi zao kwa kuimarisha uchumi na huduma
za kijamii na waliofanya juhudi za kupunguza umaskini na uimarishaji wa
maendeleo endelevu yenye usawa kwa wote.
Utolewaji wa tuzo hii unaifanya Afrika iendelee kufaidika na uzoefu
na weledi wa marais waliomaliza muda wao wa kutawala. Tuzo hii
inawawezesha kuendelea kufanya shughuli nyingine za kijamii wanapomaliza
muda wao wa kutawala.
Vigezo vinavyotumika katika kutafuta mshindi ni pamoja na Rais
aliyemaliza muda wake katika nchi mojawapo ya Afrika; awe ameng’atuka
madarakani sio zaidi ya miaka mitatu iliyopita; aliyechaguliwa
kidemokrasia; aliyetumikia muda wake kwa mujibu wa katiba na
aliyeonyesha kwa vitendo kuwa na sifa za pekee za uongozi.
Pohamba ni nani?
Huyu amezaliwa mwaka 1935 huko Namibia ya Kaskazini, eneo lililokuja
kuwa ngombe ya harakati za SWAPO- Chama ambacho tangu uhuru 1990
kimekuwa kikitawala na kushinda chaguzi kwa ushindi wa kishindo.
Pohamba alipata elimu yake kwa wamisionari na akaajiriwa na mgodi wa
Shaba akiwa kijana. Ni mwenza wa uanzilishi wa SWAPO na rafiki yake Sam
Nujoma, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Namibia.
Aliwahi kufungwa kwa sababu za harakati na utawala uliosaidiwa na
makaburu. Amekuwa Waziri wa Ardhi baada ya uhuru, aliyeleta mabadiliko
kwenye sekta ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuigawa kwa wananchi.
Pohamba alipendekezwa na Nujoma kurithi mikoba ya urais mwaka 2004 na sasa mikoba hiyo anamwachia Hage Geingob.
Tuzo hii inafadhiliwa na Mo Ibrahim mzaliwa wa Sudan lakini ana uraia
wa Uingereza; ni mjasiriamali na bilionea anayemiliki biashara ya
mawasiliano ya simu kwakuwekeza katika nchi za Afrika.
Tuzo hii inatolewa kila mwaka lakini tangu 2007 ilipoanza ni marais
watatu tu walizawadia, huku Nelson Mandera akizawadia kwa heshima.
Chanzo cha habari mwanahalisi online