Mwili wa Marehemu, John Damiano Komba
Kapteni Komba afa na deni la CRDB
MBUNGE
wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba, amefariki dunia kutokana na
kuzongwa na mzigo wa madeni, likiwamo mkopo kutoka Benki ya CRDB.
Taarifa zinasema, benki hiyo ilitoa kiasi
cha sh. 12 bilioni kwa mwanasiasa huyo mwaka 2009, lakini hadi mauti
yanamkuta, alikuwa hajaweza kulipa deni hilo. Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).
Habari zinasema, wakati Komba akihaha kuokoa nyumba yake kutokana na tanganzo la benki ya CRDB kwenye vyombo vya habari; huku akiwa tayari ameonekana kukata tamaa; ghafla Jumamosi jioni alipatwa na shinikizo la damu na kufariki dunia.
Mamilioni hayo ya shilingi yalitolewa na
CRD Benki kwa mbunge huyo kwa ajili ajili ya kuendeleza shule zake mbili
alizokuwa akizimiliki – shule ya Sekondari ya Bakili Muluzi na Shule ya
Msingi ya Coletha – zilizoko jijini Dar es Salaam.
Hadi anafariki dunia, Komba alikuwa
amebakiza kiasi cha zaidi ya sh. 78.5 milioni. Deni la Benki linatokana
na mkopo pamoja na riba ya asilimia 17 katika kipindi cha miaka mitano
ya uhai wa mkopo.
Komba amefariki dunia Jumamosi iliyopita, miezi mitatu baada ya Benki ya CRDB kuuza shule zake.
Mbali na kuuza shule, benki iliuza vifaa
mbalimbali, likiwamo eneo la ukubwa wa mita za mraba zaidi ya 34,000
lililotumika kutoa mkopo wa sh. 900 milioni mwaka 2009.
Shule za Komba pamoja na vifaa vyake, vimenunuliwa na mfanyabiashara mmoja mmoja.
Gazeti hili limeelezwa kuwa Komba
alijaribu, bila mafanikio, kushawishi serikali kununua shule yake; na
kwamba alitinga hadi ikulu na makao makuu ya CCM kuomba msaada ili shule
na nyumba yake visiuzwe.
Hata hivyo, taarifa zinasema, Komba
hakufanikiwa kupata msaada wa kuzuia shule kuuzwa. Hadi anafariki dunia
benki ilikuwa inajiandaa kuuza nyumba yake.
“Yule bwana alifika hadi ikulu kuomba
msaada ili nyumba yake isiuzwe. Alitaka serikali imsaidie kununua shule
yake; au kuomba benki izuie kwa muda uuzaji kwa kuwa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT) lilikuwa limekubali kununua eneo hilo kwa
bei ya soko,” ameeleza mtoa taarifa.
Baada ya shule kuuzwa na deni kushindwa
kumalizika, mtoa taarifa anasema, Komba alirudi tena ikulu na CCM kuomba
msaada wa kukwamua nyumba yake.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alijaribu
kunusuru shule ya Komba kupigwa mnada kwa kuiandikia benki ya CRDB kumpa
mwanasiasa huyo muda zaidi wa nyongeza ili kulipa deni lake.
Hata hivyo, pamoja na maombi ya Pinda kupewa nafasi, bado Komba alishindwa kulipa deni hilo.
Komba aliyekuwa anajulikana kwa jina
maarufu la “Mzee wa kutoa mitaji kwa vimwana,” alizikwa juzi Jumanne,
katika jimbo lake la uchaguzi la Mbinga Magharibi.
Chanzo cha habari mwanahalisi online