Thursday, March 12, 2015

Zitto: Mimi bado mbunge.

12th March 2015
Chapa
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Zitto amesema hajapewa taarifa rasmi, hivyo ataendelea kuwa mbunge.
 
Pamoja na kauli hiyo ya Zitto, viongozi wa Chadema wamesema hawatahangaika kumwandikia barua kumjulisha hatua zilizochukuliwa na chama hicho dhidi yake.
 
Zitto akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, alisema ataendelea na kazi yake ya ubunge kwasababu hajapewa taarifa rasmi na Chadema kuhusu uamuzi uliochukuliwa wa kumvua uanachama.
 
“Sina taarifa rasmi kilichotokea na kama mnavyoona naendelea na vikao vya kamati kama kawaida na leo (jana) nitakuwa na watu wa Benki Kuu (BoT), TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na AG  (Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Ijumaa nitakwenda Kigoma jimboni kwangu kwa ajili ya kazi zangu, niliwahidi wananchi wangu nitakwenda kabla ya kwenda bungeni, kimsingi mimi bado ni mbunge,” alisema.
 
Licha ya Chadema kutangaza kumvua uanachama, Zitto jana aliendesha vikao vya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kama kawaida.
 
Zitto alisema hawezi kujibishana na chama chake kwani hajalelewa katika maadili kama hayo na kwamba kitu muhimu kwake ni kazi ya kuwatumikia Watanzania.
 
“Mimi huwezi ukanilinganisha na mbunge yeyote katika kazi ambazo nimekuwa nikizifanya, siasa kwangu ni ‘issues’ tofauti na watu wengine ambao siasa zao ni kugombana na watu, kwangu hizi ni changamoto, nakomazwa,” alisema.
 
Alisema ifahamike kuwa maamuzi yoyote lazima yafanywe kwa kikao na hayawezi yakaamuliwa na mtu mmoja.
 
“Maamuzi yoyote yanayotolewa ni ‘process’ (mchakato) kwa sababu hata kwa maamuzi ya chama kuna suala la kumwandikia barua Spika wa Bunge naye ajiridhishe, kwa hiyo mimi bado ni mbunge ambaye nilichaguliwa kuanzia mwaka 2005 hadi sasa na nitaendelea kuwatumikia Watanzania,” alisema. 
 
LISSU; HATUTAMWANDIKIA BARUA ZITTO 
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema chama hicho hakitahangaika kumwandikia barua Zitto kumjulisha uamuzi wake kwa kuwa anajua alishakiuka Katiba ya chama kwa kushtaki hivyo uanachama wake unakoma mara moja.
 
Lissu alisema jana kuwa: “Sisi hatuhitaji kumfahamisha kwa sababu anajua adhabu ya kukiuka Katiba, tutaandika barua kwenye mamlaka husika siyo kwake.”
 
Alisema Chadema kitamwandikia barua Katibu wa Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuwafahamisha uamuzi huo.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alipoulizwa na NIPASHE jana alisema, hadi jana jioni alikuwa hajapokea barua ya Chadema juu ya kumtimua uanachama Zitto.
 
 WABUNGE WAMLILIA
Baadhi ya wabunge wamezungumzia kuvuliwa uanachama kwa Zitto, wengine wakimshauri kuwa kama hajaridhika anaweza kukata rufaa zaidi mahakamani.
 
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema hawezi kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kuwa ndiyo mhimili wa kutoa haki.
 
Hata hivyo, alisema Zitto ana nafasi ya kukata rufaa ngazi ya juu ya Mahakama kama hajaridhika na uamuzi huo. 
 
LUGOLA: CHADEMA WAMEKOSEA  
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema amepokea kwa mshtuko taarifa za Mahakama kutupa shauri la Zitto, akieleza kuwa Chadema nayo haijatumia busara kumfukuza. 
 
“Nimeshtushwa na kusikitishwa zaidi kwa kitendo cha Chadema kumvua uanachama kwa sababu mahali ambapo sisi CCM tumefika tulikuwa tunahitaji upinzani imara ambao unatunyima usingizi ili  tuisimamie vyema serikali, katika mazingira ambayo tunahitaji upinzani imara kama Chedema sidhani kama wamechukua uamuzi wa busara,” alisema. 
 
Lugola alisema uimara wa Chadema hautapatikana kwa kumfukuza Zitto, bali kwa kuvumiliana na kutafuta muafaka ndani ya chama hicho pale zinapotokea. 
 
Alisema CCM inahitaji Chadema imara ili iwe makini katika kuwatumikia wananchi na kwamba kwa kumfukuza Zitto, Chadema na CCM vitadhohofika kwa kuwa vitakosa mtu makini wa kuikosoa.
 
“Mchango wake ulikuwa ni mkubwa na wangeweza kuiga CCM ambayo ina watu ambao walianza kampeni za urais mapema, lakini hatujawafukuza, tumewaonya. Chadema isiangalie mabaya ya CCM iyachukue mazuri tuliyonayo,” alisema. 
 
SERUKAMBA: INADIDIMIZA DEMOKRASIA 
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Peter Serukamba, alisema uamuzi wa Chadema unadhohofisha demokrasia nchini.  
 
Alisema Katiba ya nchi ilipaswa kuyatazama ili kukomesha udikteta wa demokrasia nchini, akisema kwa Zitto ni miongoni mwa wabunge wenye ushawishi mkubwa, hivyo Chadema walipaswa kutomtimua. 
 
MWIGULU: NIMESIKITISHWA
 Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema amesikitishwa na taarifa za kuenguliwa uanachama Zitto ndani ya chama alichoanzia siasa, alichokitumikia kwa jasho na mali, alichowekeza muda na akili yake kwa zaidi ya miaka 19.
 
Mwingulu ambaye aliandika taarifa hiyo katika mtandao wake wa Facebook, alisema Zitto amekuwa chachu ya mabadiliko kwa vitendo kwa Taifa.
 
“Uwezo wa kisiasa wa Zitto adhabu yake siyo kumfukuza, demokrasia ni lazima itumike, nakusihi kijana mwenzangu, mwanasiasa mwenzangu na mchumi mwenzangu kuwa, Taifa linakuhitaji sana wakati huu tunapopambana na ufanyaji kazi kwa mazoea na kuleta mabadiliko kwa vitendo, usikate tamaa Watanzania watakuhesabia mema kwa yote unayoyafanya kwa ajili ya Taifa letu,” alisema Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi.
 
MZIRAY: CHADEMA WAMEFANYA MAAMUZI YA JAZBA
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Kuga Mziray, alisema Chadema imefanya maamuzi ya kumvua uanachama Zitto kwa jazba kwa sababu hali hiyo haiwezi kusaidia kuviimarisha vyama vya upinzani kupambana na chama tawala.
 
“Inaonekana kumekuwa na jazba na kutafutana katika maamuzi haya, siasa za kuviziana na kukomoana siyo nzuri, Zitto amefanya kazi nzuri sana ndani ya Chadema kulikuwa na sababu gani kufanya maamuzi haraka ya kumvua uanachama,” alisema
Mziray  pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha APPT Maendeleo.
 
 ADC : CHADEMA WANGEMSAMEHE ZITTO
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Change (ADC), Doyo Hassan Doo, alisema uamuzi uliochukuliwa na Chadema ni wa haraka kwani wangeweza kulitazama suala hilo kibinadamu na kumsamehe.
 
“Hatukatai  Chadema wamefuata katiba yao kumfukuza Zitto, lakini si vibaya kama wangemsamehe, sisi hatuungi mkono hii tabia mbaya iliyoanza kujengwa na baadhi ya vyama vya siasa kufukuzana fukuzana,” alisema.
 
ACT: TUNAMKARIBISHA ZITTO 
Katibu Mkuu wa Chama cha  Alliance for Change and Transparency (ACT- Tanzania), Samson Mwigamba, alimshauri Zitto asikate rufaa kwa kuwa atapoteza muda, badala yake achukue uamuzi wa kujiunga na ACT.
 
 “Tunatambua mchango wa Zitto katika Taifa hili, siasa zake ni tofauti na siasa za watu wengine, ni za kistaarabu, uzalendo na anapenda maelewano na watu wote, hivi sasa kila chama kitapenda kumkimbilia ila atambue kwamba ACT pekee ndiyo chama kinachoweza kumfanya atimize ndoto zake za kisiasa,” alisema Mwigamba.
 
Juzi Lissu, alitangaza Zitto kuvuliwa uanachama kwa madai ya kukiuka katiba ya chama kifungu cha 8(a) (x) ambacho kinaeleza kuwa, mwanachama yeyote akifungua kesi mahakamani dhidi ya chama akishindwa katika kesi hiyo anakuwa amejifukuzisha uanachama.
 
CHANZO: NIPASHE