Friday, January 23, 2015

Mwenyekiti kwa Pinda ala kipigo

Mwenyekiti kwa Pinda ala kipigo

23rd January 2015


























Uapishaji wenyeviti wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine umekumbwa na vurugu zilizosababisha aliyekuwa mgombea uenyekiti kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupewa kipigo na wananchi mbele ya askari polisi na kuchaniwa nguo zake kwa madai alitaka kuapishwa kinyemela.
 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda , ametajwa na kulalamikiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo kwa kudaiwa kutoa maagizo ya kuapishwa kada kutoka CCM katika mtaa wake bila kushinda uchaguzi.
 
 Aidha,Mwenyekiti wa mtaa wa Migombani kata ya Segerea, Japhet Kembo, hivi karibuni aliapishwa na wananchi kupitia wakili wa kujitegema baada ya uongozi wa manispaa kushindwa kumuapisha kwa wakati, jana aliapishwa rasmi na Mwanasheria wa Manispaa hiyo.
 
Mwingine aliyeapishwa ni Mwenyekiti mteule wa mtaa Minazi mirefu, Ubaya Chuma.
 
 Wakati wa zoezi hilo, Mariano Bungala ambaye aligombea mtaa wa Kigogo Fresh ‘B’ kata ya Pugu, anakoishi Waziri Mkuu, alipewa kichapo na wananchi wakiwamo wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa madai kuwa hakushinda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini kwa sababu anatoka mtaa anakoishi Pinda, hivyo ulifanyika ujanja ili aapishwe kinyemela.
 
Vurugu hizo ziliibuka katika ofisi za Manispaa ya Ilala saa saa 3:30 asubuhi muda mfupi baada ya Bungala kuitwa na maofisa wa manispaa ili kuingia ukumbini kuapishwa, lakini alipotaka kuingia tu alidakwa na wananchi na kuanza kupewa kichapo.
 
Vurugu hizo zilisababisha watumishi wa Manispaa hiyo kusitisha kwa muda kazi hiyo katika ofisi zao kushudia vurugu hizo ambazo zilizimwa baada ya polisi kumuokoa Bungala aliyekuwa akiendelea kupewa kipigo.
 
Mgombea wa Chadema katika mtaa huo, Patricia Mwamakula, ambaye alipambana na Bungala katika uchaguzi huo, alisema wakati wa uchaguzi Desemba 14, mwaka jana hakuna mshindi aliyetangazwa baada ya kutokea vurugu.
 
Alisema kutotangazwa kwa matokeo hayo kulifuatia wanachama wa CCM kuchoma masanduku baada ya kubaini kadri kura zilivyokuwa zinaendelea kuhesabiwa ushindi ulikuwa unaelekea kwa mgombea wa upinzani.
 
“Hakuna aliyeshinda kwenye uchaguzi kwenye mtaa wetu, tatizo tunakaa mtaa anaoishi Waziri Mkuu ambaye amesema kuwa hawezi akaongozwa na mwenyekiti anayetoka chama cha upinzani,” alisema.
 
Mwanachama mwingine wa Chadema, Mayama Mkwizu, alisema wananchi wa mtaa wa Kigogo Fresh “B” hawako tayari kuongozwa na mwenyekiti wa CCM ambaye hakushinda kwenye uchaguzi kwa sababu tu ya shinikizo la Waziri Mkuu.
 
“Kura zilipigwa vizuri, lakini CCM walichoma masanduku kabla ya matokeo kutangazwa, kutaka kuapishwa Bungala, ni shinikizo la Waziri Mkuu, kama wanataka kusema alishinda wa CCM walete majivu hapa yaliyotokana na kuchomwa kwa masanduku ya kura au kama Pinda anaona chama chake kimeshinda aje yeye aapishwe,” alisema.
 
Hata hivyo, Bungala akizungumza na waandishi wa habari huku akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa wamemzunguka huku mkono wa shati lake ukiwa umechanwa na kuondolewa kabisa, alisema ana uhakika alishinda uchaguzi huo.
 
KAULI YA BUNGALA
“Nilishinda kwa kupata kura 233 na matokeo yalitangazwa na Afisa Mtendaji Kata ya Pugu ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi na ndiye aliyeniambie nije niapishwe,” alisema Bungala huku akichechemea kutoka na kipigo alichokipata.
 
Bungala alisema tukio lililompata la kupigwa na ataliwasilisha kwa viongozi wake wa chama na kwamba waliomfanyia vurugu hizo ni wahuni ambao wanataka kuendesha siasa za vurugu.
 
Alipoulizwa kama kuna shinikizo kutoka kwa Waziri Mkuu na kuamua kuja kuapishwa wakati anafahamu kuna utata katika matokeo kwenye mtaa wake, alisema hizo taarifa ni za uongo. 
 
MWANASHERIA WA MANISPAA ANENA
Naye Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Mashauri Musimu, alisema licha ya mwenyekiti wa mtaa Kigogo Fresh “B’ kupigwa na kusababisha asiapishwe, lakini manispaa itahakikisha inafanya kila liwezekanalo aapishwea kwa sababu ndiye mshindi halali katika uchaguzi huo.
 
“Anayetambuliwa na Manispaa kuwa ndiye mshindi ni Mariano Bungala na kama kuna mtu hajaridhika anaruhusiwa kwenda mahakamani kudai haki,” alisema.
 
Nao wananchi na wafuasi wa Chadema walitoa thadhari kwamba kama viongozi wa Manispaa watamuapisha mgombea wa CCM na wao watamuapisha  wa Chadema ili mtaa huo uwe na wenyeviti wawili kutoka vyama tofauti.
 
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Kigogo Fresh  ‘B’ kata ya Pugu ambayo NIPASHE ilionyeshwa na  maofisa wa Manispaa ya Ilala yanaonyesha kuwa katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM alipata kura 134, Chadema 127, CUF 17 na mgombea wa NCCR-Mageuzi alipata kura tisa.
 
OFISI YA WAZIRI MKUU
Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Waziri Mkuu, Irene Bwire, alipoulizwa kuhusu madai dhidi ya Waziri Mkuu, hakutaka kueleza zaidi ya kusema kuwa ofisi ya Tamisemi ndiyo inayosimamia masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa hivyo ndiyo inayoweza kutoa jibu kuhusu utata wa matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Kigogo Fresh ‘B’.
 
“Uchaguzi wa serikali za mitaa unasimamiwa na Tamisemi, wasiliana na Katibu Mkuu wa Tamisemi au Waziri watakupa majibu, kwanza mimi sipo ofisini tangu jana,” alisema Irene.
 
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia alipotafuta simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
 
MGOMBEA CCM  SEGEREA  ALALAMIKA
Wakati huo huo;  aliyekuwa  mgombea wa serikali ya mtaa wa Migombani Jimbo la Segerea kupitia CCM, Uyeka Idd, amemtupia lawama Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, kwa kupingana na tangazo lake la kuahirisha uchaguzi.
 
Tangazo hilo la kuahirisha uchaguzi ambao ulitakiwa kufanyika Desemba 14, mwaka jana  lilitaka uahirishwe kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza katika kituo hicho zikiwamo vurugu.
 
Alisema Desemba 16, tangazo lilitoka kwa Mkurugenzi kuwa uchaguzi uairishwe, lakini jana walishangazwa na kitendo cha kuapishwa kwa mgombea wa Chadema kuwa ndiye mshindi wa mtaa huo.
 
“Tangazo lilisema marudio ya uchaguzi ni Desemba 21, uchaguzi ulifanyika, lakini ulifanyika ndani ya dosari za awali na kukwamisha baadhi ya wananchi kupiga kura, ” alisema Idd alipozungumza na waandishi wa habari.
 
Januari 20, mwaka huu, wananchi walimwapisha Japhet Kembo wa Chadema kuwa ndiye mshindi wa mtaa huo  baada ya ukimya wa serikali kitomwapisha.
 
Aliongeza kuwa madai ya shinikizo toka kwa wananchi kuapishwa kwa kiongozi huyo hayana tija kwani cha msingi ni uchaguzi kufanyika na ushindi upatikane kwa haki.
 
“Madai ya wananchi kwamba kuna shinikizo la Mbunge wa Segerea,  Dk. Makongoro Mahanga, kuhusu ushindi wa CCM katika Mtaa huo sio kweli kwani mbunge (Mahanga) anakaa mtaa tofauti na huo,” alisema Idd. Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Christina Mwakangale na Adela Josephat