Friday, January 23, 2015

Ni majanga tena Polisi

Ni majanga tena Polisi

23rd January 2015

  Wengine hoi kwa kipigo


   Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda.

Jeshi la Polisi limekubwa na dhahama nyingine baada ya  askari wake wawili wa mkoani Tabora, kupewa kipigo kwa madai ya kusababisha kifo cha kijana mmoja wa mjini humo.
 
 Tukio hilo lilitokea juzi sambamba na tukio la kuuawa kwa askari wawili wa kituo polisi cha Ikwiriri, wilayani Rufiji, Pwani.
 
 Aidha, Jeshi la Polisi limeungana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuwasaka watu waliovamia Kituo cha Polisi Ikwiriri wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani na kuwaua askari hao na kupora silaha mbalimbali zikiwamo bunduki na risasi.
 
 Katika tukio la Tabora, kijana huyo anadaiwa kufa wakati akifukuzwa na askari hao wa Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Tabora kwa lengo la kutaka kumtia mbaroni kwa tuhuma za  kushiriki mchezo wa kamari.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, akizungumza na NIPASHE alisema tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu  saa 10.30 jioni katika mtaa wa Kadinya kata ya Ng’ambo.
 
Kamanda Kaganda aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni  PC Yohana na MW Daniel Isonda na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kitete  kutokana na kujeruhiwa kwa kipigo na wananchi.
 
Alisema wananchi walianza kuwashambulia askari hao walipotaka kuwakamata vijana watatu waliokuwa wakicheza kamari kijiweni katika eneo la Ng’ambo mjini Tabora.
 
Vijana hao baada ya kubaini wanataka kukamatwa na polisi walianza kukimbia na bahati mbaya mmoja wao alitumbukia ndani ya dimbwi la maji na kuzama.
 
Kaganda alisema kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Edwin Kefa (19), baada ya kutumbukia katika dimbwi hilo,  alishindwa kuogelea na hivyo askari waliokuwa wakimfukuza walimuokoa akiwa katika hali mbaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Kitete, lakini alifariki  wakati akipatiwa matibabu.
 
Alisema pamoja na askari hao kushambuliwa, Jeshi hilo litaendelea kufanya msako mkali ili kuvunja vijiwe vyote vya wacheza kamari, wavuta bangi na wanaotumia dawa za kulevya mkoani Tabora.
 
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa wananchi walichukua uamuzi wa kuwashambulia askari hao baada ya kuona wakimpiga  kijana aliyepoteza maisha kabla ya kufikwa na mauti.
 
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Kitete, Dk. Yusuph Bwire, alisema hali za askari hao zinaendelea vizuri na kwamba  Isonda alijeruhiwa begani na kichwani.
 
Dk. Bwire alisema Yohana alijeruhiwa kichwani na kwamba aliruhisiwa jana asubuhi  baada ya hali yake kuwa nzuri.
 
JWTZ YAJITIOSA RUFIJI
Wakati hayo yakitokea, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu waliokiteka na kukivamia kituo cha polisi Ikwiriri na kuwaua askari wawili na kuiba silaha.
 
Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, akizungumza katika mahojiano na Redio One katika kipindi cha Kumepambazuka, alisema wanashirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kuhakikisha waliofanya tukio hilo wanatiwa mbaroni.
 
Kamishna Chagonja alisema hadi kufikia jana jioni hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa na wamebaini kuwa bomu lililorushwa katika kituo hicho halikuwa moja bali yalikuwa mengi.
 
“Uvamizi ulikuwa mkubwa na inaonekana waliofanya tukio hilo  walikuwa si chini ya 15 na baada ya kufanya tukio hilo waliondoka kwa kutumia Noah,” alisema.
 
Alisema mabaki ya bomu lililorushwa yamepekwa kwa wataalam kubaini ni bomu la aina gani.
 
Juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Urich Matei, alisema tukio la kuvamiwa kituo hicho lilitokea saa 8:00 usiku.
 
Kamanda Matei alitaja askari waliouawa kuwa ni PC Judith Timoth na  Koplo Edga Mlinga ambaye ni askari wa kikosi cha usalama barabarani na kwamba miili ya askari  imehifadhiwa katika kituo cha afya Ikwiriri.
 
Alisema baada ya kukivamia kituo hicho waliiba bunduki aina ya SMG mbili, SAR mbili, Shotgun moja, risasi zaidi ya 60 na bunduki mbili za kulipulia mabomu ya machozi.
 
 Matei alisema baadaye walilipua bomu kituoni hapo ambalo liliharibu gari lenye namba PT 1965 linalotumiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kituo hicho (OCCID) kisha kutokomea kusikojulikana.
 
Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alisema jeshi hilo lina idara nyingi, hivyo taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kushirikiana katika uchunguzi wa tukio hilo zinaweza kuwa za kweli

Mwenyekiti kwa Pinda ala kipigo

Mwenyekiti kwa Pinda ala kipigo

23rd January 2015


























Uapishaji wenyeviti wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine umekumbwa na vurugu zilizosababisha aliyekuwa mgombea uenyekiti kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupewa kipigo na wananchi mbele ya askari polisi na kuchaniwa nguo zake kwa madai alitaka kuapishwa kinyemela.
 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda , ametajwa na kulalamikiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo kwa kudaiwa kutoa maagizo ya kuapishwa kada kutoka CCM katika mtaa wake bila kushinda uchaguzi.
 
 Aidha,Mwenyekiti wa mtaa wa Migombani kata ya Segerea, Japhet Kembo, hivi karibuni aliapishwa na wananchi kupitia wakili wa kujitegema baada ya uongozi wa manispaa kushindwa kumuapisha kwa wakati, jana aliapishwa rasmi na Mwanasheria wa Manispaa hiyo.
 
Mwingine aliyeapishwa ni Mwenyekiti mteule wa mtaa Minazi mirefu, Ubaya Chuma.
 
 Wakati wa zoezi hilo, Mariano Bungala ambaye aligombea mtaa wa Kigogo Fresh ‘B’ kata ya Pugu, anakoishi Waziri Mkuu, alipewa kichapo na wananchi wakiwamo wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa madai kuwa hakushinda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini kwa sababu anatoka mtaa anakoishi Pinda, hivyo ulifanyika ujanja ili aapishwe kinyemela.
 
Vurugu hizo ziliibuka katika ofisi za Manispaa ya Ilala saa saa 3:30 asubuhi muda mfupi baada ya Bungala kuitwa na maofisa wa manispaa ili kuingia ukumbini kuapishwa, lakini alipotaka kuingia tu alidakwa na wananchi na kuanza kupewa kichapo.
 
Vurugu hizo zilisababisha watumishi wa Manispaa hiyo kusitisha kwa muda kazi hiyo katika ofisi zao kushudia vurugu hizo ambazo zilizimwa baada ya polisi kumuokoa Bungala aliyekuwa akiendelea kupewa kipigo.
 
Mgombea wa Chadema katika mtaa huo, Patricia Mwamakula, ambaye alipambana na Bungala katika uchaguzi huo, alisema wakati wa uchaguzi Desemba 14, mwaka jana hakuna mshindi aliyetangazwa baada ya kutokea vurugu.
 
Alisema kutotangazwa kwa matokeo hayo kulifuatia wanachama wa CCM kuchoma masanduku baada ya kubaini kadri kura zilivyokuwa zinaendelea kuhesabiwa ushindi ulikuwa unaelekea kwa mgombea wa upinzani.
 
“Hakuna aliyeshinda kwenye uchaguzi kwenye mtaa wetu, tatizo tunakaa mtaa anaoishi Waziri Mkuu ambaye amesema kuwa hawezi akaongozwa na mwenyekiti anayetoka chama cha upinzani,” alisema.
 
Mwanachama mwingine wa Chadema, Mayama Mkwizu, alisema wananchi wa mtaa wa Kigogo Fresh “B” hawako tayari kuongozwa na mwenyekiti wa CCM ambaye hakushinda kwenye uchaguzi kwa sababu tu ya shinikizo la Waziri Mkuu.
 
“Kura zilipigwa vizuri, lakini CCM walichoma masanduku kabla ya matokeo kutangazwa, kutaka kuapishwa Bungala, ni shinikizo la Waziri Mkuu, kama wanataka kusema alishinda wa CCM walete majivu hapa yaliyotokana na kuchomwa kwa masanduku ya kura au kama Pinda anaona chama chake kimeshinda aje yeye aapishwe,” alisema.
 
Hata hivyo, Bungala akizungumza na waandishi wa habari huku akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa wamemzunguka huku mkono wa shati lake ukiwa umechanwa na kuondolewa kabisa, alisema ana uhakika alishinda uchaguzi huo.
 
KAULI YA BUNGALA
“Nilishinda kwa kupata kura 233 na matokeo yalitangazwa na Afisa Mtendaji Kata ya Pugu ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi na ndiye aliyeniambie nije niapishwe,” alisema Bungala huku akichechemea kutoka na kipigo alichokipata.
 
Bungala alisema tukio lililompata la kupigwa na ataliwasilisha kwa viongozi wake wa chama na kwamba waliomfanyia vurugu hizo ni wahuni ambao wanataka kuendesha siasa za vurugu.
 
Alipoulizwa kama kuna shinikizo kutoka kwa Waziri Mkuu na kuamua kuja kuapishwa wakati anafahamu kuna utata katika matokeo kwenye mtaa wake, alisema hizo taarifa ni za uongo. 
 
MWANASHERIA WA MANISPAA ANENA
Naye Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Mashauri Musimu, alisema licha ya mwenyekiti wa mtaa Kigogo Fresh “B’ kupigwa na kusababisha asiapishwe, lakini manispaa itahakikisha inafanya kila liwezekanalo aapishwea kwa sababu ndiye mshindi halali katika uchaguzi huo.
 
“Anayetambuliwa na Manispaa kuwa ndiye mshindi ni Mariano Bungala na kama kuna mtu hajaridhika anaruhusiwa kwenda mahakamani kudai haki,” alisema.
 
Nao wananchi na wafuasi wa Chadema walitoa thadhari kwamba kama viongozi wa Manispaa watamuapisha mgombea wa CCM na wao watamuapisha  wa Chadema ili mtaa huo uwe na wenyeviti wawili kutoka vyama tofauti.
 
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Kigogo Fresh  ‘B’ kata ya Pugu ambayo NIPASHE ilionyeshwa na  maofisa wa Manispaa ya Ilala yanaonyesha kuwa katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM alipata kura 134, Chadema 127, CUF 17 na mgombea wa NCCR-Mageuzi alipata kura tisa.
 
OFISI YA WAZIRI MKUU
Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Waziri Mkuu, Irene Bwire, alipoulizwa kuhusu madai dhidi ya Waziri Mkuu, hakutaka kueleza zaidi ya kusema kuwa ofisi ya Tamisemi ndiyo inayosimamia masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa hivyo ndiyo inayoweza kutoa jibu kuhusu utata wa matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Kigogo Fresh ‘B’.
 
“Uchaguzi wa serikali za mitaa unasimamiwa na Tamisemi, wasiliana na Katibu Mkuu wa Tamisemi au Waziri watakupa majibu, kwanza mimi sipo ofisini tangu jana,” alisema Irene.
 
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia alipotafuta simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
 
MGOMBEA CCM  SEGEREA  ALALAMIKA
Wakati huo huo;  aliyekuwa  mgombea wa serikali ya mtaa wa Migombani Jimbo la Segerea kupitia CCM, Uyeka Idd, amemtupia lawama Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, kwa kupingana na tangazo lake la kuahirisha uchaguzi.
 
Tangazo hilo la kuahirisha uchaguzi ambao ulitakiwa kufanyika Desemba 14, mwaka jana  lilitaka uahirishwe kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza katika kituo hicho zikiwamo vurugu.
 
Alisema Desemba 16, tangazo lilitoka kwa Mkurugenzi kuwa uchaguzi uairishwe, lakini jana walishangazwa na kitendo cha kuapishwa kwa mgombea wa Chadema kuwa ndiye mshindi wa mtaa huo.
 
“Tangazo lilisema marudio ya uchaguzi ni Desemba 21, uchaguzi ulifanyika, lakini ulifanyika ndani ya dosari za awali na kukwamisha baadhi ya wananchi kupiga kura, ” alisema Idd alipozungumza na waandishi wa habari.
 
Januari 20, mwaka huu, wananchi walimwapisha Japhet Kembo wa Chadema kuwa ndiye mshindi wa mtaa huo  baada ya ukimya wa serikali kitomwapisha.
 
Aliongeza kuwa madai ya shinikizo toka kwa wananchi kuapishwa kwa kiongozi huyo hayana tija kwani cha msingi ni uchaguzi kufanyika na ushindi upatikane kwa haki.
 
“Madai ya wananchi kwamba kuna shinikizo la Mbunge wa Segerea,  Dk. Makongoro Mahanga, kuhusu ushindi wa CCM katika Mtaa huo sio kweli kwani mbunge (Mahanga) anakaa mtaa tofauti na huo,” alisema Idd. Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Christina Mwakangale na Adela Josephat

Thursday, January 15, 2015

PAC yawabana Bandari kujilipa posho kubwa za safari

PAC yawabana Bandari kujilipa posho kubwa za safari




Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac), Zitto Kabwe.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac), imeagiza Mamlaka ya Bandari (TPA), kurejesha Sh. milioni 62.8 ambazo wamelipana kama posho za safari kwa viwango vipya kabla ya kuidhinishwa na Msajili wa Hazina (TR).

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe, akitoa maamuzi ya kamati iliyokutana na uongozi wa TPA na Wizara ya Uchukuzi, kupitia hesabu zao za mwaka 2011/12 pamoja na ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Agizo hilo limekuja baada ya kamati kutaka maelezo ya viwango vipya vya posho ya safari kwa watumishi wa Bandari kwa kudai kuwa wanalipana fedha ya kujikimu nyingi kuliko wabunge.

Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Madeni Kipande, alifafanua kuwa malipo hayo baada ya kupendekezwa yaliwasilishwa kwenye Bodi ya Bandari ambao walipitisha na kuanza kulipwa kabla ya kuidhinishwa na TR.

“Tunakiri tulikosea kwenye hilo kwa kuwa malipo yoyote kabla ya kulipwa, ni lazima yaidhinishwe na TR baada ya Bodi kupitishwa, tulilipa viwango vipya bila kupata kibali cha Hazina,” alisema Kipande.

Zitto alisema fedha iliyotumika ni mali ya umma, hivyo ni lazima ikatwe kwenye mishahara ya watumishi wote waliosafiri na kulipwa viwango hivyo kuanzia Januari mwaka huu, kwa kuwa ni fedha ya umma iliyolipwa kinyume cha taratibu na sheria.

“Naagiza fedha zote zilizotumika kwa safari za ndani na nje ya nchi na kutolewa bila ‘approval’ ya TR zirudishwe na tupewa taarifa ya utekelezaji…hamkuwa na sababu ya kukimbilia kulipana fedha hizo bila kuwa na idhini ya TR,” aliagiza Zitto.

Mwenyekiti huyo aliagiza TR kufanya ukaguzi katika taasisi za umma kujua viwango vinavyotakiwa kulipwa kwa watumishi wanaposafiri ndani na nje ya nchi kwa kuwa TPA inaonekana mtumishi wa kawaida anaposafiri analipwa Sh. 123,000 kwa siku huku kiwango kinachojulikana ni Sh. 80,000 kwa siku.

Kwa mujibu wa taarifa ya TPA kwa kamati inaonesha kuwa mfanyakazi wa ngazi za juu anaposafiri ndani ya nchi alitakiwa kulipwa Sh. 270,000 na kwa viwango vipya ni Sh. 500,000 kwa siku, huku mtumishi wa ngazi za chini akilipwa Sh. 320,000.

Viongozi wanafunzi Udom watimuliwa.

Viongozi wanafunzi Udom watimuliwa.

16th January 2015





























Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), umemfukuza Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi Kitivo Cha Sayansi ya Elimu ya Jamii, na wenzake wawili kupewa barua ya kusimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kosa la kuhamasisha mgomo.

Aliyefukuzwa na Waziri Mkuu, Philipo Mwakimbinga, na waliosimamishwa kwa muda usiojulikana ni Rais wa kitivo hicho, Masatu Kiabweni na Katibu Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi, Ismail Chande.

Akizungumza na NIPASHE, Afisa Uhusiano mwandamizi wa chuo hicho, Beatrice Baltazary, alithibitisha waziri huyo kufukuzwa na wengine kupewa barua ya kusimamamishwa.

Alisema wanafunzi hao wamechukuliwa hatua hiyo baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chuo kukaa na kwamba pamoja na mambo mengine, walizungumzia hatua za kuwachukulia wanafunzi hao.

Afisa huyo alisema Mwakibinga amefukuzwa kabisa kwa kuwa alishawahi kujihusisha na mgomo wa mwaka 2010/2011 akafukuzwa, lakini akakata rufaa na kuomba msamaha kwenye Kamati  ya Nidhamu.

“Baada ya kukata rufaa, Kamati ikamuonea huruma ikamrudisha kabla ya kurudi alitakiwa aje na kiapo kutoka kwa mwanasheria kwamba hatajihusisha na mgomo tena, lakini kwa sasa amerudia kosa hivyo kajifukuzisha mwenyewe moja kwa moja,” alisema.

Alisema wanafunzi waliosimamishwa wataitwa na Kamati ya Nidhamu ya chuo kwa ajili ya kuhojiwa ambayo ndiyo itaamua kama wataendelea na chuo au la.

“Kutokana na barua walizopatiwa, watatakiwa kujibu tuhuma zao ndani ya mwezi mmoja wataitwa kwa ajili ya kujitetea na kama ikitokea kuna wengine walijihusisha nao pia watafanyiwa utaratibu wa kisheria kwa kuwa uchunguzi unaendelea,” alisema.

Kwa upande wake, Mwakibinga alisema uongozi wa chuo uliwapatia barua zao jana mchana ambazo zilisainiwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Utawala, Fedha na Mipango, Prof.  Shaban Mlacha.

Alibainisha kuwa barua yake ilieleza kumfukuza chuo kabisa na wenzake wamesimamishwa kwa muda usiojulikana huku wakitakiwa kujibu tuhuma mbalimbali.

84 KIZIMBANI
Katika hatua nyingine, wanafunzi 84 wa programu maalum ya Stashahada ya ualimu Udom waliofanya mgomo na kuandamana kushinikiza kulipwa madai yao, jana walipandishwa kizimbani kwa kosa la kukusanyika bila kibali maalum.

Wanafunzi hao ni wa programu maalumu katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknohama iliyoanza mwaka jana, walifanya mgomo huo juzi na kuandamana  kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuwasilisha madai yao.

Mbele ya mbele ya Hakimu Mkazi, Kabate Richard, Mwendesha Mashitaka Lopa, aliiambia Mahakama kuwa wanafunzi hao walitenda kosa hilo Januari 14, mwaka huu, majira ya saa 11:30 alfajiri.

Wanafunzi hao wamegawanywa katika makundi manne ya kesi namba 5, 6,7 na 8 ya mwaka 2015.

Mara baada ya kusomewa mashataka, washtakiwa hao waliachiwa kwa dhamana ya kujidhamini wenyewe kwa dhamana ya maneno ya Sh. 20,000 kila mmoja.

Kesi hizo zimepangwa kusikilizwa Februari 16 hadi 19, mwaka huu.

UDOM: HATUJAPOKEA FEDHA ZA WANAFUNZI
Uongozi wa Udom umesema  bado haujapokea malipo ya awamu ya pili ya mikopo kwa wanafunzi  wa programu maalum ya Stashahada ya ualimu katika Chuo hicho ambao walifanya mgomo.

Baltazary alisema malipo hayo yalitakiwa kulipwa Januari 10, mwaka huu, lakini Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HELSB), haijawasilisha fedha hizo.

“Sisi kama chuo tumefanya mawasiliano na HELSB kuhusu malipo ambayo yalitakiwa kulipwa lakini siku zimepita, tumejibiwa wanapeleka hundi benki, hivyo siwezi kuwajibia Bodi kuwa lini wanafunzi watapata, sisi tunachoahidi mara baada ya fedha zao kuingizwa watalipwa,” alisema.

Alisema fedha ambayo imelipwa hadi sasa kwa wanafunzi hao ni ya awamu ya kwanza na kwamba program hiyo ina jumla ya wanafunzi 2,174  lakini mpaka sasa wamesajiliwa 2016.

“Wanafunzi ambao wameingiziwa malipo yao kwa awamu ya kwanza ni 1,626 ambapo zimeingizwa jumla ya Sh. milioni 597.5 na waliobaki 390 wameingiziwa fedha zao juzi, hivyo kwa awamu ya kwanza malipo yamekamilika isipokuwa kwa wanafunzi 102 hawajaingiziwa kutokana na wao bado hawajasaini,” alisema.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idrisa Kikula, alisema utaratibu wa kupatiwa fedha za kujikimu kwa wanafunzi hao chuo hakihusiki.

 “Tunachohusika ni kuletewa hizo hela halafu tunawapa na hizo hela zimekuwa zikija wanapewa sasa wale wenyeji ambao ni wanafunzi wa Shahada ya kwanza sasa sijui kwa kutafuta umaarufu wa nini wakaanza kuwashawishi na kuwaambia nyie mnapata hela ndogo Sh. 6,000 kwa siku, lazima mpate Sh. 10,000 kama wengine,”alisema Prof. Kikula na kuongeza:


“Kwanza wamekuwa wakifanya vikao visivyo halali na kufanya maandamano na hiyo hiyo jana (juzi) wakawa wamechachamaa hao wakubwa (Shahada) wakaanza kuwashawishi wenzao hawataki na hii imetokea katika kitivo kimoja siyo chuo kizima.”

Akizungumza kuhusu madai ya wanafunzi hao kupatiwa fedha tofauti na wanayoisaini, Profesa Kikula alisema halijui hilo na kuahidi kufuatilia.

 Aidha, aliwataka wanafunzi kufuata taratibu za chuo wanapokuwa na madai mbalimbali na siyo kufanya fujo.

UPINZANI: WANAFUNZI WASIFUKUZWE
Wakati huo huo, Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo, ameitaka serikali na uongozi wa Udom kutowafukuza wanafunzi walioandamana kudai haki yao ya kupatiwa mikopo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jijini Dar es Salaam, alisema tatizo kubwa lipo kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HELSB) kutokana na kushindwa kutoa mikopo kwa wakati na kwa usawa.

Alisema serikali inastahili lawama zote kwa kuwa wakati inapanga kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Stashahada wa masomo ya Hisabati na Sayansi, hakukuwa na bajeti iliyotengwa kwa ajili yao na ndiyo maana wamekosa fedha za kuwalipa.

“Ni vigumu kumwambia mtu mwenye njaa aendelee kusoma na kuishi chuoni bila fedha ya chakula na kujikumu, tuna taarifa wapo wanafunzi wameshaondoka na wengine walishindwa kuvumilia na kuandamana, tangu Novemba, mwaka jana, hawajapata fedha zozote,” alisema.

Naibu Waziri, Joshua Nassari, alisema iwapo wanafunzi hao watafukuzwa au kusimamishwa masomo, ataongoza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu kudai haki yao.

Alisema HELSB inastahili kuvunjwa na mikopo hiyo kutolewa na taasisi za fedha ili kila Mtanzania aweze kukopa kwa kuwa kigezo kwa sasa si familia duni bali ni aina ya mchepuo anaosoma mwanafunzi.

Nassari alisema ana mifano hai ya wanafunzi mapacha waliosomoa pamoja tangu darasa la kwanza hadi kitacho cha sita ambao walipangiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini mmoja alipewa mkopo asilimia 80 na mwingine asilimia 40, jambo ambalo alisema linaonyesha HELSB haiko makini.

Kina Lowassa, Membe kuonyeshana kazi ITV

Kina Lowassa, Membe kuonyeshana kazi ITV

 Ni mdahalo kwa wanaotajwa urais 2015.
























Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

(Udasa) kwa kushirikiana na kituo cha kurusha matangazo ya runinga na redio cha ITV/Radio One, wametangaza kuandaa midahalo itakayotoa fursa kwa wagombea urais wa vyama vyote vya siasa kuelekea katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika nchini kote mwaka huu.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Udasa na ITV/Radio One kufikia makubaliano kuandaa midahalo hiyo, ikiwa ni sehemu ya mchango wao muhimu wa kijamii katika kufanikisha uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Udasa, Prof. Kitila Mkumbo na Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Radio One, Joyce Mhavile, walisema kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kuwa vyama vyote vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo na ambavyo vitasimamisha wagombea wa urais, vitaalikwa kushiriki katika midahalo hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa wagombea wote watakaojitokeza kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huo, wataalikwa kushiriki midahalo hiyo.

Ilieleza kuwa midahalo hiyo itaanza kwa kushirikisha wagombea ndani ya vyama vyao pale chama kitapokuwa na wagombea zaidi ya mmoja na baadaye kati ya wagombea watakaokuwa wameteuliwa na vyama vyao.

“Utaratibu kamili wa midahalo hii utatolewa baadaye,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Iliviomba vyama vya siasa na wagombea wote watakaojitokeza kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huo kushiriki katika midahalo hiyo ili kuwapa wananchi fursa ya kuwajua na wao kuwaeleza falsafa, sera na mikakati yao na ya vyama vyao katika kukabiliana na matatizo yanayoikabili nchi sasa na baadaye.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa katika nchi za kidemokrasia, midahalo ya wagombea imekuwa ni sehemu muhimu katika kufanikisha uchaguzi ulio huru, haki, wazi na amani.

“Midahalo hutoa fursa muhimu kwa wagombea kueleza falsafa, sera na mikakati yao ya kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi na nchi zao,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa midahalo huwapa fursa ya kipekee wapigakura na wananchi kwa jumla katika kuwajua na kupima umahiri na weledi wagombea na vyama vyao.

Kwa sababu hiyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa midahalo imekuwa ni sehemu muhimu ya uchaguzi katika nchi zinazoamini na kuzingatia misingi ya demokrasia.

“Tafiti zinaonyesha kuwa midahalo ya wagombea urais ina nafasi ya kipekee katika kuwawezesha wapigakura kuamua mgombea gani wamchague na kwamba midahalo imekuwa ni chombo muhimu katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kwa wingi,” ilieleza.

Hadi sasa ni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako baadhi ya makada wake wametangaza nia ya kugombea huku wengine wakitajwa kuwa wana nia hiyo.

Waliotangaza nia ni pamoja na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.

Wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na mawaziri  wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Wanatajwa pia Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Prof. Mark Mwandosya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

VIONGOZI WA DINI
Wakati Udasa na ITV/Radio One wakitangaza hilo, Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Dar es Salaam imetangaza azma yake ya kukutana na wagombea watakaoteuliwa na vyama vyao na kupitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuwania urais katika uchaguzi huo, ili kuzungumza nao kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki na amani.

Pia imetangaza azma ya kutoa semina kwa wagombea wa nafasi hiyo, ili kuwaandaa kisaikolojia kukubaliana na matokeo yatakayotangazwa na Nec wanakuwa waadilifu na kuweka utaratibu mzuri kipindi cha uchaguzi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sheikh Alhaad Musa Salum, alisema hayo alipozungumza katika mkutano wa kuratibu mipango ya mwaka 2015 katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu pamoja na upigaji wa kura wa ama kuikubali au kuikataa katiba iliyopendekezwa.

Alisema azma ya kutaka kukutana na wagombea hao kabla ya uchaguzi na kuwapa semina hiyo, inatokana na mitiririko wa matukio ya mara kwa mara ya upingaji wa matokeo, ambao umekuwa ukisababisha uvunjifu wa amani.

Aliwataka viongozi wa dini nchini kuepuka kujidhalilisha kwa kutumiwa na wanasiasa, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi huo, kwani ni hatari kwa nchi.

Alisema viongozi wa dini wanapaswa kuwa makini na kuacha kuonyesha uelekeo  na masuala ya itikadi, kwani jambo hilo linaweza kuleta mkanganyiko na kuwagawa Watanzania kutokana na imani zao.

Hata hivyo, kamati hiyo pia imepanga kukutana na wahariri wa vyombo vya habari kote nchini ili kuhakikisha wanaripoti habari za uchaguzi pasipo kuelemea upande mmoja ili kuepusha kuigawa nchi.

“Kamati yetu imejipanga vizuri kuhakikisha nchi inakuwa na amani, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na upigaji kura wa kuichagua katiba iliyopendekezwa kwa kuwahubiria wagombea wa nafasi ya urais juu ya amani, kwani wao ndiyo chanzo cha machafuko ya nchi,” alisema Alhaad ambaye ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema wakati wa uchaguzi, hasa kwa wagombea wa nafasi za urais, huwa chanzo cha kutokea vurugu pale matokeo yanapotangazwa kwa aliyeshindwa kutokukubaliana nayo.

Sheikh Alhaad alisema katika kuhakikisha nchi inakuwa salama na amani, kamati itawafuata wabunge bungeni na kuwapa semina ili wafahamu dhamana ya nchi ipo mikononi mwao, kwani wamekuwa wakiwagawa wananchi kutokana na vurugu wanazozizua bungeni.

Imam wa Msikiti wa Kigogo, Sheikh Jalala Mwakindenge, alisema jambo la uongozi wa dini ni kubwa sana, kwani wanashinda na waumini wao kwenye nyumba za ibada.

Kwa maana hiyo, alisema Taifa linahitaji sana viongozi wa dini kuliko wanasiasa, kwani ndiyo wahubiri wakuu wa amani kwa muda mrefu wakiwa makanisani.

“Kitendo cha kulingania amani ni kitendo cha ujasiri sana, kwa maana hiyo nawaomba mapadri, masheikh na maaskofu tuwe na msimamo mmoja wa kutetea nchi yetu isipoteze amani iliyopo,” alisema Mwakindenge.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Dar es Salaam, Mchungaji Aman Lyimo, alisisitiza kuwa viongozi wa dini kuwa na kauli moja, hasa kipindi hiki, kwani kuna baadhi ya viongozi wameanza kujigawa kutokana na itikadi za vyama kitu ambacho ni chukizo mbele za Mungu.

Hatua ya kamati hiyo imekuja baada ya kuwapo kwa historia ya  vurugu na uvunjifu wa amani nchini, hasa kipindi cha uchaguzi mkuu kuibuka hisia za udini.

Maalim Seif: Ukawa tishio kwa CCM

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema matokeo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika mwezi uliopita ni somo kwa vyama vya upinzani kuwa vitakaposhikamana hakuna nguvu ya Polisi wala Jeshi itakayowazuia wasikamate dola.

Maalim Seif alisema hayo jana wakati  akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Tandale Kwa Tumbo, ulioandaliwa kwa ajili ya kuwashukuru wanachama wa CUF na wananchi kwa kujipa ushindi chama hicho.

Maalim Seif alisema ni dhahiri matokeo mazuri ya wapinzani yalitokana na uamuzi wa vyama vinne vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuunganisha nguvu zao na kushindana na CCM, pamoja na kujidhatiti kulinda kura zao zisiibwe.

Alisema CUF pamoja na vyama vinavyounda UKawa kusimama imara kuhakikisha mapandikizi hawaingizwi katika maeneo wasiyohusika, lakini pia walihakikisha wale walioshindwa hawaapishwi kushika nyadhifa hizo.

“Suala la kuendelea na Ukawa halina mjadala kama kweli tunataka tuichimbie kaburi CCM, pale tulipokuwa kila mtu na lake, hatukuwa na nguvu kama tulizonazo sasa,” alisema Maalim Seif.

Katika uchaguzi huo Kata ya Tandale, CUF kilishinda mitaa mitatu kati ya sita, na mtaa mmoja hadi sasa matokeo yake yana utata.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kwatumbo, Mohammed Kassim alisema ushindi huo unatokana na umakini wa wana-CUF kuhakikisha wanadhibiti ujanja wote wa CCM katika hatua zote za uchaguzi.

Hata hivyo aliwataka wanachama wa CUF na wananchi wa Tandale wasiridhike na wasijisahau kwa ushindi huo, lakini wahakikishe wanajiimarisha zaidi na kuhakikisha wote wanajiandikisha katika daftari la kura, ili washiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Dk. Slaa aeleza alivyomnasa anayedaiwa kujiita Jaji Samatta

Dk. Slaa aeleza alivyomnasa anayedaiwa kujiita Jaji Samatta

















Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai kwamba, kabla ya kuchukua hatua ya kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk. Edward Hosea, akimuomba ofisi yake ifanye uchunguzi wa kina kumbaini mtu anayejiita Jaji Barnabas Samatta, alimpa mkewe achunguze jina la mtu huyo.

Alidai kwamba aliamini mkewe, Josephine Mushumbuzi, angeweza kumtambua kwa haraka mtumiaji wa simu namba (0754 013237) anayejiita Jaji Samatta kwa kuwa mkewe ni mtaalam mbobezi wa Teknolojia ya Mawasiliano ya Kompyuta na aliweza kumjua mtu huyo baada ya kumtumia mhamala wa Sh. 500 kwa njia ya M-Pesa.

Jaji Samatta feki, anadaiwa alitumia jina hilo kutafuta nauli ya kwenda Dar es Salaam kuzungumza na Dk. Slaa ili aisaidie Chadema ishinde kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ya kuvuliwa ubunge wake kupitia rufaa namba 47 ya mwaka 2012 iliyofunguliwa na Lema dhidi ya Mussa Hamis Nkanga na wenzake. Lema alikuwa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu ya Arusha kumvua ubunge.

“Mke wangu alinipa mrejesho baada ya kutuma Shilingi 500 kwa njia ya M-Pesa kwenda namba (0754 013237) na akanitaarifu kwamba namba hiyo imesajiliwa kwa jila la Abeid Abeid na siyo Barnabas Samatta. Nikaamua kumtumia (Abeid anayejiita Jaji Samatta) ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwa kutumia simu yangu (0783 967519) Mr. Abeid the game is over, naamini kwamba upo mzima. (yaani bwana Abeid, mchezo umekwisha),” alidai.

Dk. Slaa alidai kwamba muda huo huo, Abeid anayejiita Jaji Samatta, alimjibu kwa kumtumia ujumbe mfupi, “Nimeamini chama chenu (Chadema), ni chama kinachofuata haki bila ya kununua. Natangaza kuwaunga mkono kuanzia leo. Na akajitambulisha mwisho wa ujumbe huo kwamba yeye ni Afisa wa Takukuru, Wilaya ya Ulanga, lakini kwa sasa yupo Arusha.

Mshitakiwa huyo, (Abeid Abeid) anakabiliwa na kesi ya jinai namba 117 ya mwaka 2013 ya jaribio la kumtapeli  Dk. Slaa, akitumia jina la Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta kujipatia fedha.

Mwendesha Mashitaka wa  Takukuru mkoa wa Kilimanjaro, Susan Kimaro, aliyekuwa akisaidiwa na wakili Furahini Kibanga,, alimtaka Dk. Slaa kuieleza mahakama hiyo kama aliwahi kuzungumza na Jaji Samatta ambaye si aliyeko mahakamani hapo, na Slaa akaieleza mahakama kwamba alizungumza naye baada ya Jaji, Thomas Mihayo, kumpatia namba halali ya Jaji Mkuu mstaafu (Samatta.

“Nilimtafuta siku hiyo hiyo, lakini hakupatikana na asubuhi ya Aprili 12 mwaka 2012, Jaji Samatta halisi na si huyu feki ninayemuona hapa, alinipigia simu akaniambia hajawahi kufanya mawasilino na Godbless Lema wala Profesa Abdallah Safari ambaye wakati huo alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.  Alishtuka sana nilipomueleza kuna kesi kama hiyo ya yeye kutaka apewe fedha za nauli ili aje Dar es Salaam kusaidia kutoa mbinu ili Lema ashinde kesi yake iliyopo Mahakama ya Rufaa,” alidai Dk. Slaa.

Slaa aliendelea kudai kwamba baada ya kumjibu Samatta feki ujumbe huo, alimtumia ujumbe mwingine unaosema: “Baba nakushukuru sana, lakini kwa sababu namna  namna misingi ya Chadema ilivyo; hatuwezi kufanya kitu hicho, lakini pia Lema amefungua kesi
namba 47 ya mwaka 2012 katika Mahakama ya Rufaa.”

Alidai kuwa baada ya kumueleza Jaji Samatta kuhusu sakata hilo, alimjibu kwamba muelekeo wa hayo mawasiliano kati ya Samatta feki na yeye (Dk. Slaa) yanaakisi kwamba Chadema nayo, inataka kuingia kwenye mkumbo wa rushwa na kumshauri  kufanya kazi ya kuvisaidia vyombo vya dola kuanza kuchunguza mawasiliano hayo.

Hatma kina Lowassa, Membe, Sumaye, Wasira, Makamba, Ngeleja mwezi ujao

Hatma kina Lowassa, Membe, Sumaye, Wasira, Makamba, Ngeleja mwezi ujao

Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ‘waliohukumiwa’ kutumikia ‘kifungo’ cha kutogombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuanza kampeni za kusaka urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kabla ya wakati, wanakabiliwa na hatari ya kuongezewa zaidi adhabu hiyo.

Makada hao ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

 Wengine ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, ambao wote mbali ya ‘kuhukumiwa’ kutumikia adhabu hiyo, pia wako chini ya uangalizi wa chama.

 Uwezekano wa makada hao kuongezewa zaidi adhabu hiyo, ni moja ya maazimio yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya CCM katika kikao chake kilichofanyika juzi mjini Unguja, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.

 Kikao hicho kilichofanyika kwa zaidi ya saba, kilijadili mambo matatu ya msingi, ikiwamo kuhusu adhabu dhidi ya makada hao, maadili ya chama na kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited  (IPTL) ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Azimio hilo lilitangazwa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya Nec jana.

Nape alisema baada ya muda kwisha, itafanyika tathmini kuona kama walizingatia masharti ya adhabu zao au la.

“Na kama kuna, ambao watakutwa hawakuzingatia masharti ya adhabu zao wataongezewa adhabu,” alisema Nape.

Alisema chama hicho kitajadili mwenendo wao na kupitisha maazimio baada ya adhabu yao kumalizika mapema mwezi ujao.

Makada hao waliwahi kuitwa na Kamati Ndogo ya Nidhamu iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula na kuwahoji.

Baada ya mahojiano hayo, Februari, mwaka jana, Kamati Kuu ya CCM ilitangaza uamuzi huo mzito dhidi yao.

KUHUSU ESCROW
Kuhusu uchotwaji wa fedha hizo katika akaunti hiyo, kamati kuu imeiagiza kamati hiyo ndogo ya maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili katika kashfa hiyo.

Nape alisema vikao vya kuwajadili waliohusika katika kashfa hiyo vitaanza rasmi Jumatatu ijayo.

Alisema tayari barua zimeshapelekwa kwa wahusika katika kashfa hiyo kuwataka wafike kwenye kikao hicho.

Nape alisema CCM imesikitishwa na kashfa hiyo jinsi ilivyowahusisha wanachama wake waandamizi.

Kutokana na hali hiyo, alisema CCM inaunga mkono maazimio yote yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya wote waliohusika na kashfa hiyo.

“Kamati kuu imejadili na kuamua waliohusika na sakata hilo kuwaondoa katika vikao vya maamuzi,” alisema Nape.

Hivyo, akasema kamati kuu imeitaka serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea kutekeleza maazimio ya Bunge juu ya suala hilo baada ya kuanza kuyatekeleza.

 Pia iliwataka wote wanaopewa dhamana kujenga utamaduni wa kuwajibika, vinginevyo waliowapa dhamana wachukue hatua za kuwawajibisha.

“Kamati Kuu ya CCM baada ya kukaa kujadili suala hili kwa muda mrefu na kwa kina, imesikitishwa sana na sakata hili. Na kamati imetoa maazimio hayo, ambayo kamati ndogo ya maadili itafanya kikao tarehe 19/01/2015 kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo,” alisema Nape.

 Mbali na hayo, alisema Kamati Kuu pia ilipitisha ratiba ya shughuli mbalimbali za kamati kuu za chama kwa mwaka 2015.

 Pia walipanga ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM ndani ya dola, ambao utapangwa na vikao vijavyo vya chama.

Akizumnguzia hali ya uchaguzi mkuu ujao, Nape alisema CCM imejipanga vizuri na kwamba, ina uhakika wa asilimia 100 kupata ushindi wa kishindo.

Alivishauri vyama vya upinzani kujipanga vyema ili navyo viambulie viti vichache ili kuimarisha demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.

APINGA UTARATIBU WA CUF
Hata hivyo, alipinga vikali hatua ya Chama cha Wananchi (CUF) kuondoa utaratibu wa kura za maoni katika kuwatafuta wagombea katika uchaguzi mkuu.

 Alisema CUF imeonyesha nia yake ya kutozingatia misingi ya demokrasia ya kuwapa uhuru wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka katika hatua za awali.

“CCM kamwe hata siku moja hatutawatoa wagombea mfukoni. Tuna utaratibu wetu wa kura ya maoni, ambao tutaufuata ili kuwapa nafasi wanachama kumchagua kiongozi wanayemtaka,” alisema Nape.

Alisema CCM ni taasisi inayoendeshwa kwa misingi ya demokrasia na maamuzi ya walio wengi na siyo kama Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos) kama vilivyo vyama vya upinzani, ambavyo maamuzi hutolewa na mtu mmoja, ambaye ni kiongozi mkuu.

Alisema wapinzani wasahau kuwa ipo siku ccm itang’oka madarakani na badala yake itaendelea kushinda chaguzi na kuliongoza taifa la Tanzania.

“Kama Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, anasema CCM tujiandae kuondoa virago vyetu Ikulu, tunamwambia hayo ni maneno ya mfamaji, haachi kutapatapa. Na maneno kama hayo ameshazowea kuyasema mara nyingi tangu alivyofukuzwa CCM,” alisema Nape.

SOKO LA MAHINDI
Alisema kamati kuu pia ilijadili suala la soko la mahindi na kuiagiza serikali kuangalia upya mfumo unaotumiwa na Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) katika ununuzi wa zao hilo.

Nape alisema utaratibu wa sasa, ambao kwa kiasi kikubwa unanufaisha zaidi mawakala badala ya wakulima moja kwa moja, unatakiwa ubadilishwe ili uwanufaishe zaidi wakulima.
DR Slaa kugombea Ubunge Mkoa wa Arusha Uchaguzi mkuu 2015
Taarifa zilizopo kutoka makao makuu ya chama cha Demokrasia Chadema hapo Kinondoni ni kwa Katibu wa chama hicho taifa Dr Slaa anajiandaa kugombea ubunge katika mkoa ya majimbo ya mkoa wa Arusha .
Huu umeeelzwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa UKAWA kupata nguvu na ushawishi ndani ya kanda ya Kasikazini hususani mkoa wa Arusha katika uchaguzi mkuu ujao.
Taarifa zaidi zinabainisha kuwa timu ya watu watano kutoka makao makuu ya Chadema imeshaundwa na kutumwa Arusha kwa ajili ya kifanya utafiti juu ya jimbo lipi hasa litafaa kwaDr Slaa kugombea ubunge. Itakumbukwa kuwa Dr Slaa alikuwa mbunge wa KARATU

Maofisa wa serikali kortini mgawo Tegeta Escrow

Maofisa wa serikali kortini mgawo Tegeta Escrow

Mkurugenzi wa Huduma ya Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma (kulia) na picha ya kushoto, Mhandisi wa Mamlaka ya Umeme Vijijini (Rea),Theophillo Bwakea, wakifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana kujibu mashtaka ya rushwa baada ya kudaiwa kupokea mgao wa fedha zinazohusiana na akaunti ya Tegeta Escrow. PICHA: TRYPHONE MWEJI
Maofisa wawili wa serikali,  Rugonzibwa Mujunangoma na Theophillo Bwakea,  wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kujibu mashitaka ya rushwa baada ya kudaiwa kupokea mgao wa Sh. Milioni 485.1 kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  walizohamishiwa na James Rugemalira.

Katika kesi ya kwanza, aliyekuwa Mwanasheria wa Mamlaka ya Vizazi na Vifo (Rita), Mujunangoma ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara Ardhi, Nyumba na  Maendeleo ya Makazi, alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emmilius Mchauru.

 Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, akisaidiana na Max Ari, ulidai  kuwa Februari 5, mwaka jana katika Benki ya Mkombozi iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo akiwa Mkuu wa Sheria wa Wizara hiyo, alipokea rushwa.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alipokea rushwa ya Sh. milioni 323.4 kama zawadi kupitia akaunti yake namba 00120102062001  kutoka Rugemalira ambaye ni  Mshauri wa kimataifa binafsi na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL baada ya kuwa mjumbe katika manejimenti ya Rita wakati wa machakato wa kuipitisha IPTL kuliuzia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) umeme.

 Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kama zawadi hiyo akiwa ofisa wa muda wa kushughulikia masuala ya IPTL.
 Mshtakiwa huyo alikana mashtaka.

Swai alidai  upande wa Jamhuri hauna pingamizi la dhamana kwa mshtakiwa huyo, hivyo mahakama ijielekeze katika hati ya mashtaka ya fedha anazodaiwa kuchotewa mshtakiwa huyo kutoka kwenye akaunti hiyo ya Tegeta Escrow.

 Hakimu Mchauru alisema mshtakiwa huyo atakuwa nje kwa dhamana endapo atatimiza mashrti kwa kujidhamini kwa fedha taslimu Sh. milioni 160  au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani kiasi hicho cha fedha.

Vilevile alisema  awe na  wadhamini wawili wanaofanyakazi serikalini, watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 10 kila mmoja na mshtakiwa asitoke nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama hiyo.

 Mshtakiwa huyo alitimiza baadhi ya masharti ya dhamana, hivyo Hakimu huyo kumpa muda wa kukamilisha hati za mali zake na kuziwasilisha keshi (Ijumaa) mahakamani hapo kuhakikiwa.

 Katika kesi ya pili; aliyekuwa Mjumbe wa Kitengo cha kuidhinisha Tanesco kununua umeme wa IPTL katika Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Bwakea ambaye kwa sasa Mtumishi wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo,  Frank Moshi.

Swai alidai kuwa Februari 12, mwaka jana mshtakiwa huyo  akiwa Mhandisi  Mkuu wa Rea, alipokea rushwa ya Sh. milioni 161.7 kupitia akaunti namba 00410102643901  kutoka kwa Rugemalira ikiwa ni mgao wake kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kama zawadi.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha  baada ya kuwa mjumbe aliyeandaa sera zinazohusu sekta binafsi kuzalisha na kuuza umeme kwa Tanesco.

Mshtakiwa huyo naye alikana mashtaka yake.

Upande wa Jamhuri ulidai hauna pingamizi la dhamana na kwamba upelelezi dhidi yake umekamilika.

Hakimu Moshi alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili kutoka serikalini au wanaofanyakazi katika taasisi zinazotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. Milioni 20 kila mmoja.

Pia alisema mshtakiwa huyo hatakiwi kutoka  nje ya Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

Mshtakiwa aliachiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana na kesi yake kuahiridhwa hadi Januari 26, mwaka huu itakapotajwa tena.

Jana majira ya  saa 2:00 asubuhi, wafanyakazi na watu mbalimbali waliingia kwenye viunga vya mahakama hiyo, huku kukiwa na minong’ono kuwa  wanaotuhumiwa ufisadi wa Escrow watafikishwa mahakamani hapo.

Pia waandishi wa habari waligawanyika katika makundi tofauti huku wakijadili na kutafatuta wadau wao kujua kuhusu ujio wa watuhumiwa hao.
 Saa 5:42 asubuhi washtakiwa hao walitinga mahakamani hapo na kwenda kusomewa mashitaka yao yanayowakabili.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema),
amemkalia kooni Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, akieleza kuwa
endapo Rais Jakaya Kikwete hatamwajibisha,
anakusudia kupeleka hoja bungeni ya
kushughulikia uongo, udhaifu na utendaji mbovu
katika wizara hiyo.
Mnyika , anakuwa mbunge wa pili kuahidi
kutumia Bunge kumng’oa Mhongo akitanguliwa
na mbunge wa Simanjiro (CCM) Mkoani
Manyara, Christopher Ole Sendeka, aliyesema
endapo Rais hatamuwajibisha atapaleka hoja
binafsi bungeni ya kutokuwa na imani na
viongozi hao.
Sendeka alisema hayo juzi katika mkutano mkuu
wa mwaka wa Chama cha Wachimbaji wadogo
na wamiliki wa migodi, uliofanyika mjini
Mererani.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana, Mnyika
alisema kuwa, kiporo cha Kikwete kuhusu
Muhongo kinaendelea kuleta athari ndani ya
wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapo tuhuma
za kujipendelea kwenye uteuzi wa viongozi
wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ndani
ya wizara hiyo.
Mbunge huyo alisema anazo taarifa za ndani za
wizara kuwa Shirika la Umeme (Tanesco),
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
na Taasisi ya Uchunguzi wa Madini (MRI)
kutumika kuficha udhaifu na ufisadi ukiwamo
uteuzi wa watendaji.
Alisema zipo tuhuma mbalimbali alizipata
kuhusu teuzi zilizofanywa kabla na baada ya
kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow , ambako
zaidi ya Shilingi bilioni 300 zilichotwa na
kusababisha taharuki na chuki.
Alisema anakusudia kuchukua hatua kwa mujibu
wa sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge
kupata ushahidi wa uteuzi uliofanyika.
“Kabla ya uteuzi huo, Profesa Muhongo
alitangaza kwamba timu za wataalamu
zimeundwa kuchambua mabadiliko ya muundo
wa Tanesco, TPDC na MRI na kufanya uteuzi
wa watendaji kwa ushindani.
Mnyika alisema kuna tuhuma za upendeleo
katika mashirika na taasisi hizo zote tatu za
wizara hiyo.
“Nitatoa kauli na kuchukua hatua baada ya
kupata maelezo na vielelezo vyote kupitia vikao
vya kamati za bunge hilo vinavyoanza kesho na
mkutano wa Bunge unaotarajia kuanza Januari
27, mwaka huu,” alisema na kuongeza:
Wakati Mnyika akiyasema hayo, yapo madai
kuwa, wajumbe wa bodi ya Tanesco iliyoteuliwa
wiki iliyopita ina wajumbe wengi kutoka ukanda
mmoja wa Tanzania.
Wajumbe wa bodi hiyo iliyoteuliwa na Profesa
Muhongo ni Kissa Kilindu, Juma Mkobya, Dk.
Haji Semboja, Shabaan Kayungilo, Dk.
Mutesigwa Maingu, Boniface Muhegi, Felix
Kibodya na Dk. Nyamajeje Weggoro.
Kadhalika kuna madai ya kuteuliwa kwa
Mkurugenzi wa taasisi moja ya wizara kwa
upendeleo akitoka kanda hiyo.
Kutokana na madai hayo, NIPASHE ilimtafuta
Naibu Waziri, Charles Kitwanga, ambaye
alishangaa Watanzania kuhoji ukabila badala ya
vigezo walivyonavyo wateule hao.
“Karne ya 21 bado tunahoji ukabila, nilitegemea
watu wangeuliza watu hawa waliopewa nafasi
hizi wanavigezo gani, wengine hapa wameingia
kwa vyeo vyao,” alisema.

Monday, January 5, 2015

Wale makamanda walio toka geita mpaka dar es salaam wakiwa na nia ya kwenda ikulu kuonana na rais wa jamuhuri ya muungano wa tanzania.
Wakiwa watatu mara tu baada ya kuwasili jiji la dar es salaam safari yao ya kwenda kumfikishia rais ujumbe wao na kuidai Tanganyika na wakiwa na ujumbe mwingine mzito walio toka nao geita hatimaye wali shindwa kufika magogoni  na safari yao ikaishia kwa mkuu wa wilaya ya kinondoni. Mbali na safari kuishia kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya huyo bali mkuu wa wilaya huyo wa kinondoni ali watolea maneno yaliyo jaa uzalilishaji na unyanyasaji wa kila namna na matusi makubwa pasipo kujali lolote na kuamua kuseama yeye ni Rais na vile vile ikulu ipo wilayani kwake yani kinondoni kitu ambacho ni uongo uliokithiri na kuwaita vijana hao niwachafu kwaiyo hawastaili kwenda ikulu na hata pale ofisini kwake aliwaamuru vijana hao wasikalie viti vya ofisini kwake na kuwaamuru wakae chini kwenye sakafu.
Baada ya mazungumzo ya muda mrefu mkuu wa wilaya huyo aliawamuru vijana hao wampe ujumbe waliokuwa wanataka kumpelekea rais Jakaya Mrisho kikwete ikulu ndipo vijana hao walipo goma na kumjibu kuwa nia yao ni kuonana na rais na sio mkuu wa wilaya wanatakabkumwona raisi alie chaguliwa  na wananchi wabjumuhurinya muungano wa tanzania.
Baada ya kutoka ofisini kwa mkuu huyo wa wilaya vijana hao waliendelea na dhamira yao ya kuelekea magogoni ndipo mkuu wa wa wilaya alipo amuruvijana hao wakamatwe na polisi.
Hivi leo mapema asubuhi wamerudi tena polisi kuripoti na bado nia yao ipo palepale ya kwenda ikulu