Thursday, January 15, 2015

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema),
amemkalia kooni Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, akieleza kuwa
endapo Rais Jakaya Kikwete hatamwajibisha,
anakusudia kupeleka hoja bungeni ya
kushughulikia uongo, udhaifu na utendaji mbovu
katika wizara hiyo.
Mnyika , anakuwa mbunge wa pili kuahidi
kutumia Bunge kumng’oa Mhongo akitanguliwa
na mbunge wa Simanjiro (CCM) Mkoani
Manyara, Christopher Ole Sendeka, aliyesema
endapo Rais hatamuwajibisha atapaleka hoja
binafsi bungeni ya kutokuwa na imani na
viongozi hao.
Sendeka alisema hayo juzi katika mkutano mkuu
wa mwaka wa Chama cha Wachimbaji wadogo
na wamiliki wa migodi, uliofanyika mjini
Mererani.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana, Mnyika
alisema kuwa, kiporo cha Kikwete kuhusu
Muhongo kinaendelea kuleta athari ndani ya
wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapo tuhuma
za kujipendelea kwenye uteuzi wa viongozi
wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ndani
ya wizara hiyo.
Mbunge huyo alisema anazo taarifa za ndani za
wizara kuwa Shirika la Umeme (Tanesco),
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
na Taasisi ya Uchunguzi wa Madini (MRI)
kutumika kuficha udhaifu na ufisadi ukiwamo
uteuzi wa watendaji.
Alisema zipo tuhuma mbalimbali alizipata
kuhusu teuzi zilizofanywa kabla na baada ya
kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow , ambako
zaidi ya Shilingi bilioni 300 zilichotwa na
kusababisha taharuki na chuki.
Alisema anakusudia kuchukua hatua kwa mujibu
wa sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge
kupata ushahidi wa uteuzi uliofanyika.
“Kabla ya uteuzi huo, Profesa Muhongo
alitangaza kwamba timu za wataalamu
zimeundwa kuchambua mabadiliko ya muundo
wa Tanesco, TPDC na MRI na kufanya uteuzi
wa watendaji kwa ushindani.
Mnyika alisema kuna tuhuma za upendeleo
katika mashirika na taasisi hizo zote tatu za
wizara hiyo.
“Nitatoa kauli na kuchukua hatua baada ya
kupata maelezo na vielelezo vyote kupitia vikao
vya kamati za bunge hilo vinavyoanza kesho na
mkutano wa Bunge unaotarajia kuanza Januari
27, mwaka huu,” alisema na kuongeza:
Wakati Mnyika akiyasema hayo, yapo madai
kuwa, wajumbe wa bodi ya Tanesco iliyoteuliwa
wiki iliyopita ina wajumbe wengi kutoka ukanda
mmoja wa Tanzania.
Wajumbe wa bodi hiyo iliyoteuliwa na Profesa
Muhongo ni Kissa Kilindu, Juma Mkobya, Dk.
Haji Semboja, Shabaan Kayungilo, Dk.
Mutesigwa Maingu, Boniface Muhegi, Felix
Kibodya na Dk. Nyamajeje Weggoro.
Kadhalika kuna madai ya kuteuliwa kwa
Mkurugenzi wa taasisi moja ya wizara kwa
upendeleo akitoka kanda hiyo.
Kutokana na madai hayo, NIPASHE ilimtafuta
Naibu Waziri, Charles Kitwanga, ambaye
alishangaa Watanzania kuhoji ukabila badala ya
vigezo walivyonavyo wateule hao.
“Karne ya 21 bado tunahoji ukabila, nilitegemea
watu wangeuliza watu hawa waliopewa nafasi
hizi wanavigezo gani, wengine hapa wameingia
kwa vyeo vyao,” alisema.