Thursday, January 15, 2015

Viongozi wanafunzi Udom watimuliwa.

Viongozi wanafunzi Udom watimuliwa.

16th January 2015





























Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), umemfukuza Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi Kitivo Cha Sayansi ya Elimu ya Jamii, na wenzake wawili kupewa barua ya kusimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kosa la kuhamasisha mgomo.

Aliyefukuzwa na Waziri Mkuu, Philipo Mwakimbinga, na waliosimamishwa kwa muda usiojulikana ni Rais wa kitivo hicho, Masatu Kiabweni na Katibu Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi, Ismail Chande.

Akizungumza na NIPASHE, Afisa Uhusiano mwandamizi wa chuo hicho, Beatrice Baltazary, alithibitisha waziri huyo kufukuzwa na wengine kupewa barua ya kusimamamishwa.

Alisema wanafunzi hao wamechukuliwa hatua hiyo baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chuo kukaa na kwamba pamoja na mambo mengine, walizungumzia hatua za kuwachukulia wanafunzi hao.

Afisa huyo alisema Mwakibinga amefukuzwa kabisa kwa kuwa alishawahi kujihusisha na mgomo wa mwaka 2010/2011 akafukuzwa, lakini akakata rufaa na kuomba msamaha kwenye Kamati  ya Nidhamu.

“Baada ya kukata rufaa, Kamati ikamuonea huruma ikamrudisha kabla ya kurudi alitakiwa aje na kiapo kutoka kwa mwanasheria kwamba hatajihusisha na mgomo tena, lakini kwa sasa amerudia kosa hivyo kajifukuzisha mwenyewe moja kwa moja,” alisema.

Alisema wanafunzi waliosimamishwa wataitwa na Kamati ya Nidhamu ya chuo kwa ajili ya kuhojiwa ambayo ndiyo itaamua kama wataendelea na chuo au la.

“Kutokana na barua walizopatiwa, watatakiwa kujibu tuhuma zao ndani ya mwezi mmoja wataitwa kwa ajili ya kujitetea na kama ikitokea kuna wengine walijihusisha nao pia watafanyiwa utaratibu wa kisheria kwa kuwa uchunguzi unaendelea,” alisema.

Kwa upande wake, Mwakibinga alisema uongozi wa chuo uliwapatia barua zao jana mchana ambazo zilisainiwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Utawala, Fedha na Mipango, Prof.  Shaban Mlacha.

Alibainisha kuwa barua yake ilieleza kumfukuza chuo kabisa na wenzake wamesimamishwa kwa muda usiojulikana huku wakitakiwa kujibu tuhuma mbalimbali.

84 KIZIMBANI
Katika hatua nyingine, wanafunzi 84 wa programu maalum ya Stashahada ya ualimu Udom waliofanya mgomo na kuandamana kushinikiza kulipwa madai yao, jana walipandishwa kizimbani kwa kosa la kukusanyika bila kibali maalum.

Wanafunzi hao ni wa programu maalumu katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknohama iliyoanza mwaka jana, walifanya mgomo huo juzi na kuandamana  kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuwasilisha madai yao.

Mbele ya mbele ya Hakimu Mkazi, Kabate Richard, Mwendesha Mashitaka Lopa, aliiambia Mahakama kuwa wanafunzi hao walitenda kosa hilo Januari 14, mwaka huu, majira ya saa 11:30 alfajiri.

Wanafunzi hao wamegawanywa katika makundi manne ya kesi namba 5, 6,7 na 8 ya mwaka 2015.

Mara baada ya kusomewa mashataka, washtakiwa hao waliachiwa kwa dhamana ya kujidhamini wenyewe kwa dhamana ya maneno ya Sh. 20,000 kila mmoja.

Kesi hizo zimepangwa kusikilizwa Februari 16 hadi 19, mwaka huu.

UDOM: HATUJAPOKEA FEDHA ZA WANAFUNZI
Uongozi wa Udom umesema  bado haujapokea malipo ya awamu ya pili ya mikopo kwa wanafunzi  wa programu maalum ya Stashahada ya ualimu katika Chuo hicho ambao walifanya mgomo.

Baltazary alisema malipo hayo yalitakiwa kulipwa Januari 10, mwaka huu, lakini Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HELSB), haijawasilisha fedha hizo.

“Sisi kama chuo tumefanya mawasiliano na HELSB kuhusu malipo ambayo yalitakiwa kulipwa lakini siku zimepita, tumejibiwa wanapeleka hundi benki, hivyo siwezi kuwajibia Bodi kuwa lini wanafunzi watapata, sisi tunachoahidi mara baada ya fedha zao kuingizwa watalipwa,” alisema.

Alisema fedha ambayo imelipwa hadi sasa kwa wanafunzi hao ni ya awamu ya kwanza na kwamba program hiyo ina jumla ya wanafunzi 2,174  lakini mpaka sasa wamesajiliwa 2016.

“Wanafunzi ambao wameingiziwa malipo yao kwa awamu ya kwanza ni 1,626 ambapo zimeingizwa jumla ya Sh. milioni 597.5 na waliobaki 390 wameingiziwa fedha zao juzi, hivyo kwa awamu ya kwanza malipo yamekamilika isipokuwa kwa wanafunzi 102 hawajaingiziwa kutokana na wao bado hawajasaini,” alisema.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idrisa Kikula, alisema utaratibu wa kupatiwa fedha za kujikimu kwa wanafunzi hao chuo hakihusiki.

 “Tunachohusika ni kuletewa hizo hela halafu tunawapa na hizo hela zimekuwa zikija wanapewa sasa wale wenyeji ambao ni wanafunzi wa Shahada ya kwanza sasa sijui kwa kutafuta umaarufu wa nini wakaanza kuwashawishi na kuwaambia nyie mnapata hela ndogo Sh. 6,000 kwa siku, lazima mpate Sh. 10,000 kama wengine,”alisema Prof. Kikula na kuongeza:


“Kwanza wamekuwa wakifanya vikao visivyo halali na kufanya maandamano na hiyo hiyo jana (juzi) wakawa wamechachamaa hao wakubwa (Shahada) wakaanza kuwashawishi wenzao hawataki na hii imetokea katika kitivo kimoja siyo chuo kizima.”

Akizungumza kuhusu madai ya wanafunzi hao kupatiwa fedha tofauti na wanayoisaini, Profesa Kikula alisema halijui hilo na kuahidi kufuatilia.

 Aidha, aliwataka wanafunzi kufuata taratibu za chuo wanapokuwa na madai mbalimbali na siyo kufanya fujo.

UPINZANI: WANAFUNZI WASIFUKUZWE
Wakati huo huo, Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo, ameitaka serikali na uongozi wa Udom kutowafukuza wanafunzi walioandamana kudai haki yao ya kupatiwa mikopo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni jijini Dar es Salaam, alisema tatizo kubwa lipo kwenye Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HELSB) kutokana na kushindwa kutoa mikopo kwa wakati na kwa usawa.

Alisema serikali inastahili lawama zote kwa kuwa wakati inapanga kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Stashahada wa masomo ya Hisabati na Sayansi, hakukuwa na bajeti iliyotengwa kwa ajili yao na ndiyo maana wamekosa fedha za kuwalipa.

“Ni vigumu kumwambia mtu mwenye njaa aendelee kusoma na kuishi chuoni bila fedha ya chakula na kujikumu, tuna taarifa wapo wanafunzi wameshaondoka na wengine walishindwa kuvumilia na kuandamana, tangu Novemba, mwaka jana, hawajapata fedha zozote,” alisema.

Naibu Waziri, Joshua Nassari, alisema iwapo wanafunzi hao watafukuzwa au kusimamishwa masomo, ataongoza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu kudai haki yao.

Alisema HELSB inastahili kuvunjwa na mikopo hiyo kutolewa na taasisi za fedha ili kila Mtanzania aweze kukopa kwa kuwa kigezo kwa sasa si familia duni bali ni aina ya mchepuo anaosoma mwanafunzi.

Nassari alisema ana mifano hai ya wanafunzi mapacha waliosomoa pamoja tangu darasa la kwanza hadi kitacho cha sita ambao walipangiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini mmoja alipewa mkopo asilimia 80 na mwingine asilimia 40, jambo ambalo alisema linaonyesha HELSB haiko makini.