Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Humphrey Polepole akitoa ufafanuzi juu ya muundo wa Serikali katika Rasimu ya Katiba Mpya
Polepole: Serikali mbili hazitekelezeki
MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humprey Polepole, ameapa kuwa muundo wa Muungano wa serikali mbili hautekelezeki.
Amesema, “Mpango wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuingiza ajenda ya serikali mbili ndani ya rasimu ya katiba, utaweza kuingiza nchi katika matatizo. Hii ni kwa sababu, serikali mbili ndani ya Muungano hazitekelezeki.”
Amesema kupenyeza muundo wa serikali mbili kwenye Bunge la Katiba, ni kiyume cha utaratibu na kuonya kuwa kwa vyovyote itakavyokuwa, “muundo wa serikali mbili ni mgumu na hauwezi kutekelezeka.”
Amesema, “Huwezi kwenda kuwaambia Wanzanzibar wafute vipengele kwenye katiba yao inayotambua Zanzibar ni nchi kamili na Rais wao sio mkuu wa nchi. Halafu wakakuelewa.”
Akizungumza kwa hisia kali kwenye kongamano lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Mtandao wa Wanawake na Katiba Mpya.
Alisema, katiba ya Jamhuri ya Muungano ina muundo wa serikali mbili. Kwa namna matatizo yalivyo, hakuna njia ya kutatua matatizo yaliyosababishwa na muundo huo.
“Zanzibar walitaka Muungano wa mkataba….maana yake ni kuvunja muungano. Lakini baada ya kujadiliana nao, wamesogea kwenye tatu na tunawasihi wengine wasogee hapa kwenye tatu tujadiliane…kitendo cha kubaki huko ni kutaka kuvunja Muungano,”amesisitiza.
Amesema, “Nchi mbili zinapoungana na kuwa na nchi moja; nchi mpya inayozaliwa huwa inapewa mamlaka na madaraka fulani. Nchi mbili zilizoungana zinabaki maeneo ya nchi iliyozaliwa, ambayo huwa yanawekewa utawala wa ndani na sio kuwa na dola huru.
Mkataba huo ulitamka kwamba “ Zanzibar ibaki ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, lakini itapewa vyombo vya kuratibu masuala ya watanzania waishio Zanzibar kwa ndani. Harafu Jamhuri ya Muungano itashughulika na mambo ya muungano na mambo ya Tanzania bara.”
“Zanzibar na Tanganyika ni maeneo ya Jamhuri . katiba ya Zanzibar ibara ya 1 inasema “ Zanzibar ni nchi” hivi unaweza kuwa na nchi ndani ya nchi nyingine,” amesisitiza