Ewura yazidi kushusha bei ya mafuta
4th February 2015
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza kushusha bei za mafuta ya taa, petroli, dizeli nchi nzima kuanzia leo.
Aidha, kushuka kwa bei hizo kutapelekea kushuka kwa gharama za umeme na wapo kwenye mchakato wa uratibu kati ya Ewura na Wizara ya Nishati na Madini, ili kuangalia gharama za uzalishaji na namna ya kupunguza bei ya umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema mabadiliko hayo yametokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Alisema bei ya mafuta masafi katika soko la dunia kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa asilimia 35 hadi 40, kuanzia Julai na Desemba, mwaka jana.
Alisema mafuta hayo yameshuka kwa takribani dola 440 kwa tani kwa mafuta petroli, dizeli imeshuka kwa dola 304 kwa tani na mafuta ya taa kwa dola 324 kwa tani.
Akizungumzia kushuka kwa bei hizo katika soko la ndani, alisema petroli imeshuka kwa Sh. 187 kwa lita sawa wakati dizeli imeshuka kwa Sh. 139 kwa lita na mafuta ya taa yameshuka kwa Sh.177.
“Mabadiliko haya ya bei yametokana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kupungua kwa gharama za uagizaji mafuta, bei za mafuta katika soko la ndani zingepungua zaidi,” alisema na kuongeza kuwa
“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta kwenye mabango yanayoonekana bayana na yakionyesha bei ya mafuta punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika na ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika.”
Alisema bei za petroli kwa Dar es Salaam imeshuka kutoka Sh. 1,955 hadi 1,768, dizeli Sh. 1,846 hadi 1,708 na mafuta ya Sh. 1,833 hadi 1657.
Arusha petroli imeshuka hadi 1,852, dizeli Sh. 1,791 na mafuta ya taa Sh. 1,741.
Dodoma bei ya petroli sasa itakuwa Sh. 1,827, dizeli Sh. 1,766 na mafuta ya taa Sh. 1,715