BVR yaibua hofu bungeni
5th February 2015
Bunge limeonyesha kutoridhishwa na hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuamua kuendesha zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki (BVR), bila kuwashirikisha wadau wakuu, hali ambayo imeelezwa kuwa inaweza kusababisha machafuko katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu nchini.
Hatua hiyo ya Nec inadaiwa kuchukuliwa kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa kati yake na wadau wakuu wa uchaguzi, ambao ni vyama vya siasa.
Kutokana na hatua hiyo ya Nec, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, aliitisha kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge jana asubuhi ili kujadili suala hilo kabla ya Bunge kuishauri serikali nini kifanyike.
Uamuzi huo wa Zungu ulitokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, bungeni jana, ambaye alitaka Bunge lisimamishe shughuli zake za jana asubuhi ili kujadili suala hilo aliloliita kuwa ni la ‘dharura.’
Mbatia alisema Nec juzi ilikutana na kuamua kuanza kundesha zoezi hilo katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Njombe bila wadau wakuu kushirikishwa kama walivyokubaliana kwenye meza ya mazungumzo.
Alisema makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao cha wadau wakuu kilichofanyika Januari 8, mwaka huu, kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) chini ya Mwenyekiti wake, John Cheyo, ambacho Nec walialikwa.
Mbatia alisema katika kikao hicho, Nec iliwahakikishia kuwa zoezi hilo lina changamoto kubwa na kwamba, lingeanza upya Januari 15, mwaka huu.
Alisema zoezi hilo lilianza mwanzoni mwa Juni, mwaka jana, lakini halikufanikiwa, pia likafanyika tena mwishoni mwa mwezi huo, katika maeneo ya mkoa wa Rukwa, vilevile likafeli. Alisema wakakubaliana kuwa Nec na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) wakutane na kujadili kwa pamoja kisha wawaelimishe wadau namna zoezi hilo litakavyofanyika kwa kutumia BVR ili wakubaliane kama lina maslani kwa taifa au la.
Mbatia alisema walifikia makubaliano hayo kwa kuwa iwapo jambo hilo halitaendeshwa vizuri nchi inaweza kuingia kwenye machafuko.
Hata hivyo, alisema juzi Nec ilikutana na kuanza kufanya utaratibu wa kuendesha zoezi hilo katika mikoa hiyo bila wadau wakuu kushirikishwa kama walivyokubaliana kwenye meza ya mazungumzo.
Alisema katika kikao hicho, walikubaliana kuwa zoezi hilo lihakikishe linafanyika kwa uadilifu, uaminifu na kwa pande zote kushirikishwa.
Mbatia alisema wadau waliokutana katika kikao hicho, wanatoka vyama vyote vya siasa, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kiliwakilishwa na Makamu wake Tanzania Bara, Philip Mangula.
Alivitaja vyama vingine vilivyoshiriki kikao hicho cha wadau kuwa ni pamoja na Chadema, iliyowakiloshwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, CUF (Prof. Ibrahim Lipumba), NCCR-Mageuzi (James Mbatia), TLP (katibu mkuu wake) na vyama vingine visivyokuwa na uwakilishi bungeni.
Alisema jambo hilo lina maslahi mapana kwa umma na kwamba, katika kikao hicho, Nec ilieleza mambo mengi sana.
"Tukawashauri kwa nia njema kwamba, ni bora tukae, tuzibe ufa kabla ya kujenga ukuta tuaminiane," alisema Mbatia.
Alisema pia waliisisitiza kuwa Nec ulazima wa kulifanya jambo hilo ili kuhakikisha kwenye uchaguzi mkuu malalamiko yanapungua na kuhakikisha yaliyotokea katika uchaguzi mkuu wa Kenya, Ghana, Msumbiji na Malawi yasitokee nchini.
Kutokana na hali hiyo, alisema kwa mujibu wa kanuni ya 47, Bunge linapaswa kutekeleza matakwa ya ibara ya 63 (2) ya katiba ya nchi inayotambua kazi ya Bunge kuwa ndiyo chombo kikuu cha kuisimamia na kuishauri serikali ili zoezi hilo lifanyike kwa uadilifu na kwa ufanisi mkubwa kuepuka mtatizo yaliyotokea katika nchi hizo yasitokee hapa nchini.
"Na hakuna jambo jema kama kuaminiana katika jambo lenye maslahi kwa taifa," alisema Mbatia.
Akijibu hoja hiyo, Zungu alisema anakubaliana kwamba, jambo hilo ni la muhimu, kukaa pamoja na Bunge kuwa ni chombo cha kuishauri serikali.
Hivyo, akaiagiza serikali kuanzia wakati huo kukaa pamoja na Mbatia wakalijadili kwenye Kamati ya Bunge ya Uongozi.
Hata hivyo, Kamati ya Uongozi, imelipeleka suala hilo kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ili likafanyiwe kazi.
Katika kikao hicho, serikali imesisitiza kuwa imeshatoa fedha za kutosha kwa ajili ya BVR.