Serikali inangoja nini kusaini Mkataba wa Demokrasia Afrika?
waziri wa Katiba na Sheria, Dr.Asha-Rose Migiro.
Serikali inahojiwa ni kipi kinachoizuia kukukubali kusaini mkataba wa Demokrasia Barani Afrika (ACD)? Pamoja na hayo inahimizwa na wadau wa maendeleo na utawala bora kusaini ili kukuza kiwango cha demokrasia, uwajibikaji, utawala bora na uwazi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba, anasema katika mahojiano maalumu mapema wiki hii Jijini Dar es Salaam kuwa, Tanzania ni mojwapo ya nchi zinazounda Umoja wa Afrika (AU) ambayo haijasaini mkataba huo tangu mwaka 2007.
Kutosainiwa kwa mkataba huo, anasema husababisha taifa kuendeshwa na watendaji wasiozingatia sheria, utawala bora, haki za binadamu na za walemavu, uhuru wa taarifa, kukosekana kwa uwazi na wajibikaji hasa nyakati za uchaguzi.
“Tunashuhudia ongezeko la vitendo vya ufisadi vinavyoliabisha taifa hadi ngazi ya kimataifa, baadhi ya viongozi kutumia udhaifu wa kutosainiwa kwa azimio la ACD la mwaka 2007, hivi kuna tatizo gani kutosaini?,”anahoji Kibamba .
Kwa muktadha huo, anasema serikali inatakiwa kujitathimini kupitia sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka huu, kashfa za wizi wa fedha zilizokuwa kwenye akauti ya madeni ya nje (EPA) na tuhuma za Richmond ili kwayo iwe funzo na msukumo wa kuona umuhimu wa kusaini mkataba huo katika mkutano ujao wa AU.
Anasema kusimamishwa , kufutwa kazi na kuonywa kwa baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri hapa nchini ni matokeo ya ukosefu wa utendaji usiokuwa makini kutokana na kukosekana kwa shinikizo la kisheria kama vile mkataba unaotaka utiifu katika masuala mtambuka kama vile uchaguzi.
Mkataba huo pamoja na mambo mengine unazitaka nchi wanachama wa AU kuzingatia haki, uwazi, kupambana na vyanzo na viashiria vya migogoro inayoweza kutokana na uchaguzi, kuboresha taasisi zinazohamaisha uchaguzi na demokrasia.
Pia uchaguzi huru na wa haki katika nchi wanachama,uhuru wa kisheria, utawala wa kiutendaji unaochochea kukua kwa demokrasia na utawala bora pamoja na uwazi kulingana na azimio na kanuni za AU.
Unapofika wakati wa uchaguzi, mkataba huo unaonya nchi wanachama kutoruhusu jeshi kuingilia shughuli za uchaguzi, kuwepo kwa uwazi na upatikanaji wa taarifa za uchaguzi kwa wakati ikiwamo matokeo yaliyotokana na upigaji kura.
Mambo mengine ni kutokuwepo kwa vitendo vya kihuni ambavyo mkataba huo unavitafsiri kuwa ni pamoja na uchakachuaji wa kura, kuharibu uchaguzi kwa makusudi kwa masilahi ya mtu au chama chochote cha siasa na mambo mengine yanayoendana na hayo.
Kadhalka nchi wanachama wanatakiwa unapofika wakati wa uchaguzi kutambua thamani ya haki za binadamu kama vile walemavu, haki za wanawake,makundi yasiyotambulika na maalumu, kuhamasisha utawala bora na haki.
Kibamba ammbaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Taarifa kwa Umma (TCIB) anaona kama Tanzania haijaweza kupelekea bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ya habari licha ya viongozi waandamizi kauhidi mara kwa mara kat ika mikutano ya ndani na nje ya nchi.
Anasema kwa nyakati tofauti Rais Jakaya Kikwete akiwa nchini Uingereza na Marekani, aliahidi kufikishwa bungeni kwa muswada wa habari kabala ya kumaliza kipindi chake cha uongozi, kauli ambayo amewahi kuirudia akiwa hapa nchini pia.
“Ninaamini kwamba kupata, muswada wa habari kabla ya kumaliza muda wake mwaka 2015 ni kama ngamia kupita kwenye tundu la sindano…mimi mwenyewe hivi karibuni nimeshawahi kumuuliza Spika wa Bunge Anne Makinda ikiwa huenda bunge lijalo mwezi Februari, 2015 au kabla ya Bunge la Bajeti 2015/2016 ana mpango wa kupokea muswada wa habari, lakini amenihakikishia kwamba katika orodha yake hakuna kituo kama hicho,”alidai.
Wakati Tanzania ikiendelea kusuasua kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Vyombo vya Habari, Kenya wamepitisha Sheria mpya ya Usalama inayovibana vyombo hivyo na kuzua utata mkubwa na ikiwa ni pamoja na wabunge kuchapana makonde ndani ya mkutano wa bunge.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni bunge nchini humo liligeuka `uwanja wa vita’ kutokana na baadhi ya wabunge kunyukana makonde, kuchaniana nguo na kurushiana matusi, maneno ya kebehi na kukashifiana baada ya kugawanyika kuhusu muswada huo ambao ulipitishwa kwa nguvu.
Tayari muswada huo umesainiwa na Rais Uhuru Kenyatta na sasa ni sheria mpya ya usalama. Serikali ya Marekani imeonyesha kutoridhishwa na namna Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usalama ulivyopitishwa nchini humo.
Kwa upande wa Tanzania imekuwa vigumu kuwa na sheria ama kanuni zinazotekelezeka za kuwabana viongozi wasiowaadilifu kwa kuwa hata ndani ya katiba pendekezwa masuala ya uadalifu kuwa tunu ya taifa yalipingwa hadharani. Hata hivyo sheria ya maadili na utumishi wa umma ni kiini macho kwa kuwa hakuna kinachoweza kumbana au kumuwajibisha kiongozi wa umma anayekiuka maadili ya utumishi.