Tuesday, December 30, 2014

Kiporo cha prof. Muhongo chakaribiakuchacha

Muhongo siku zahesabika wizara ya nishati na madini


Shinikizo dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, limezidi kushika kasi baada ya Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), kumuomba Rais Jakaya Kikwete, kumwajibisha ili kupisha nafasi hiyo ichukuliwe na mtumishi mwenye sifa ya kuutumikia umma.

Desemba 22, mwaka huu, Rais Kikwete alisema katika hotuba yake kwa taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es salaam kwamba amemuweka kiporo Profesa Muhongo kwa siku mbili hadi tatu kwa kuwa uchunguzi dhidi yake ulikuwa unaendelea.

Hata hivyo, tangu wakati huo, zimeshapita takriban siku tisa bila Rais Kikwete kutangaza hatima ya Profesa Muhongo kama anatimuliwa ama kubaki katika nafasi yake.

Jukata wanamuomba Rais Kikwete kuchukua hatua hiyo kutokana na Profesa Muhongo kuhusishwa katika kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Limesema hatua hiyo inapaswa kuchukuliwa na Rais Kikwete haraka dhidi ya waziri huyo kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali ya nchi kwa sasa.

Masuala hayo yanayohusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu akaunti hiyo kutokana na taarifa zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mengine yanahusu zoezi la uandikishaji wa Watanzania katika daftari la kudumu la wapigakura katika mfumo mpya wa BVR, uandikishaji wa vitambulisho vya taifa, ambayo alisisitiza yakamilike kabla ya uchaguzi mkuu mwakani.

Mwakagenda alisema iwapo Rais Kikwete anaona utendaji wa Profesa Muhongo unafaa, ampe kazi binafsi ya kusimamia mashamba na siyo kuutumikia umma wa Watanzania.

Hatua ya Jukata ya kutaka Profes. Muhongo kuondolewa katika wadhifa huo kwa hoja kwamba hana tena sifa za kushika nafasi hiyo ya utumishi wa umma, ni mwendelezo wa mashinikizo yanayotolewa na makundi kadhaa ya jamii kufuatia maazimio ya Bunge ya mikutano ya 16 na 17 lililoahirishwa Novemba 29, mwaka huu.

Mbali na Rais Kikwete kumfukuza kazi Profea Tibaijuka, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ameshamsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake za kuhusika na sakata la akaunti ya Tegeta Escrow.

Alimshauri Rais Kikwete kujipa muda wa kusikiliza ushauri wa wataalam walioko nje ya serikali, ambao watamuonyesha nia ya kutaka kunyoosha maadili ya uongozi wa kisiasa na utumishi wa umma.

“Kwa hivi sasa, wasaidizi wake wanashindwa kumshauri Rais kwa kuogopa kubanwa wao wenyewe, hivyo wameweka wigo na kuzuia ushauri huru kumfikia Rais. Na hii ni hatari kwa ustawi wa nchi yetu,” alisema Mwakagenda.

Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, Mwakagenda alisema Katiba inayopendekezwa haina uhalali wala sifa.

Alisema katiba hiyo imependekezwa kwa ajili ya viongozi wachache, kwani kimeondolewa kipengele cha wananchi kuwadhibiti viongozi.

Aliongeza kuwa katiba hiyo pia ilipitishwa bila ya kuwapo kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kukosekana kwa theluthi mbili kutoka Zanzibar.

“Bunge la Katiba halikufanya vizuri na kulitokea mgawanyiko. Maridhiano hayakuwapo. Katiba hii ni mbaya. Ni ya viongozi. Haimfai mwananchi,” alisema Mwakagenda.

Kutokana na hali hiyo, alipendekeza kuahirishwa upigaji kura ya maoni ya Katiba mpya uliopangwa kufanyika Aprili, mwakani.

Badala yake, alishauri kuitishwa mkutano mkuu wa taifa kuhusu Katiba utakaoshirikisha wadau na vyama vya siasa na kutoa mwongozo wa masuala yenye utata.

“Mchakato usimamishwe, Rais ajaye ataundeleza, tayari Rais Kikwete ameshajijengea sifa na heshima kwa kuuanzisha mchakato huu. Pia Watanzania wengi hawajafahamu kilichopendekezwa, kwani bado hawajapata nakala ya Katiba na Wizara ya Katiba na Sheria imeshasema haijachapisha nakala,” alisema Mwakagenda.

MNYIKA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitawahamasisha wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuibana serikali bungeni kulieleza Bunge sababu za kushindwa kuwafungulia mashitaka ‘wapambe’ wa watu wanaotuhumiwa kuiba nyaraka za Bunge.

Nyaraka za Bunge zilizoibwa ni zile zinazohusu ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu miamala, iliyofanyika katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Tukio hilo lilitangazwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma Novemba 23, mwaka huu, ambalo katika taarifa yake, lilisema kuwa limewatia mbaroni vijana wawili kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka za ofisi ya Katibu wa Bunge isivyo halali.

Mbali na kuiba nyaraka hizo, vijana hao wanadaiwa kuzichakachua na kisha kusambaza mitaani ripoti ‘feki’ ya CAG.

Kauli hiyo ya Chadema ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Tanzania Bara), John Mnyika, wakati akihutubia mkutano wa hadhara juzi jioni, katika eneo la Pasua Sokoni, Manispaa ya Moshi.

Alisema kwa kuwa mamlaka ya uteuzi haijafanya uamuzi kwa ukamilifu kuhusu maazimo manane ya Bunge, Chadema itawahamasisha wabunge hao kuishinikiza serikali kueleza kwa nini inachelea kuwafikisha mahakamani wanaodaiwa kuiba nyaraka hizo.

Mnyika alisema hadi kufikia Januri 27, mwakani, kama serikali itakuwa haijawafungulia mashitaka walioiba nyaraka hizo na kuzisambaza mitaani kinyume cha sheria, atawahamasisha wabunge kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa maelezo inakuwaje inawalinda hadi sasa watuhumiwa hao.

“Wangapi mko tayari kupiga kura na kusimama upande wa haki? Wanyooshe vidole. Bunge linalokuja tutawahamasisha wabunge wa pande zote kuhoji ni kwa nini serikali inachelea kuwafikisha mahakamani wale walioiba nyaraka za ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya wizi wa mabilioni ya fedha hizi,” alisema Mnyika.

Awali, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa na Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffari Michael, alimweleza Mnyika kwamba manispaa hiyo itaunda mabaraza ya maendeleo ya kata 11 kutokana na kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji.

“Mheshimiwa Naibu Katibu Mkuu, sisi tuko vizuri katika agizo la Rais Jakaya Kikwete, kuhusu ujenzi wa maabara. Hadi sasa Manispaa ya Moshi tumefanikiwa kukamilisha maabara 40 kati ya 49,” alisema Michael.

Aliongeza: “Hii ni hatua kubwa na ambayo wenzetu wanajiuliza, inakuwaje wapinzani wanafanikiwa kuliko maeneo yanayoongozwa na chama tawala.”

Akihutubia mikutano ya hadhara iliyofanyika Shule ya Msingi Chombo kata ya Uru Kusini na Kirima Kati, Jimbo la Moshi Vijijini, Mnyika aliwataka viongozi wa Chadema kuanza operesheni maalum ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura kwa kuwa vitambulisho walivyonavyo havitatumika katika kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa pamoja na uchaguzi mkuu.

“Lazima muwaambie ukweli wananchi wa majimbo ya Siha, Moshi Vijijini, Moshi Mjini, Same Mashariki, Same Magharibi, Mwanga na Hai wajitokeze, wasiache kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura, kwa sababu vitambulisho walivyonavyo havitatumika katika kura ya maoni wala uchaguzi mkuu ujao,” alisema Mnyika.